TICADVII: Ushirikiano Afrika na Japan unaleta tija- Guterres

TICADVII: Ushirikiano Afrika na Japan unaleta tija- Guterres

Pakua

Akiwa huko Yokohama nchini Japan akihudhuria mkutano wa 7 wa Tokyo kwa ajili ya maendeleo ya Afrika, TICAD VII, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema analiona bara la Afrika kama bara lililosheheni fursa ambako pepo za matumaini zinavuma kwa kasi kuliko wakati wowote ule. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

(Taarifa ya Grace Kaneiya)

Mikutano ya TICAD ilianzishwa miaka 26 iliyopita, wa mwaka huu ukiwa ni wa 7 ambapo Bwana Guterres amesema ushirikiano huo kati ya Japan na Afrika ni wa mfano wa ukiugwa kwani ni wa wazi, shirikishi na hushajiisha amani, usalama na maendeleo endelevu Afrika.

Ubia huo amesema umekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa Afrika kupitia ujasiriamali na biashara sambamba na kuongeza fursa za huduma za afya, elimu, maji safi, huduma za kujisafi na kusongesha amani na utulivu.

Amepongeza maudhui ya mkutano wa 7 wa TICAD ambayo ni kusongesha Afrika kupitia maendeleo ya watu wake, teknolojia na ubunifu akisema ni ya wakati muafaka.

Hata hivyo ametaja mambo muhimu ya kusongesha zaidi Afrika mbele akisema ni pamoja na teknolojia na ubunifu, elimu, akisema,

(Sauti ya Antonio Guterres)

“TICAD 7 inaweza kuwa na msukumo mkubwa kusaidia Afrika kupata teknolojia na ubunifu kwa ajili ya maendeleo endelevu. Ni muhimu tushirikiane kwa karibu kupunguza pengo la kidijitali na kunufaika na maendeleo ye teknolojia ili mataifa ya Afrika yasonge kiuchumi.”

Katibu Mkuu amesema ingawa nuru inaangazia Afrika lakini bado madhara ya mabadiliko ya tabianchi na mizozo vinakwamisha Afrika kwa hiyo amesema,

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Mambo ni magumu lakini tunapaswa kuangalia kwa umakini uhusiano baina ya  amani, usalama, maendeleo, utawala bora, ujumuishaji na ujenzi wa mnepo na mabadiliko ya tabianchi.” 

 

Ametoa wito kwa ubia katika kuunga mkono mpango wa Afrika kukomesha mapigano huku akishukuru Japan kwa ukarimu wake wa kusaidia mradi wa ubia wa utatu tangu mwaka 2015 kupitia upelekaji wa wakufunzi wa uhandisi kwenye ofisi za mashinani za Umoja wa Mataifa zinazohusika na ulinzi wa amani.

Audio Credit
ARnold Kayanda/Grace Kaneiya
Audio Duration
2'9"
Photo Credit
UN Japan/Ichiro Mae.