Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wengi walikosa chanjo muhimu mwaka 2018- Ripoti

Watoto wengi walikosa chanjo muhimu mwaka 2018- Ripoti

Pakua

Makadirio mapya yaliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na shirika la afya duniani WHO kuhusu masuala ya chanjo yanaonesha mwenendo wa hatari wa kuzorota kwa viwango vy utoaji chanjo kote duniani kutokana na vita, kutokuwepo kwa usawa na malalamiko.  Jason Nyakundi na maelezo zaidi.

Katika jimbo la Kayes nchini Mali nje ya kituo cha afya wazazi wakiwa wamebeba watoto wao wanaosubiri kupatiwa chanjo muhimu lakini kwa makadirio ya mashirika hayo mawili UNICEF na WHO watoto milioni 20 kote duniani sawa na zaidi ya mtoto 1 kati ya 10 alikosa chanjo ya kuokoa maisha kama ya surua, dondakoo na pepopunda kwa mwaka 2018.

Kimataifa tangu mwaka 2010 duniani kote dozi tatu za chanjo ya dondakoo na pepopunda na dozi moja ya chanjo ya surua hazijaongezeka zimesalia katika silimia 86 ingawa inaonekana ni ya juu lakini haitoshelezi yamesema makadirio hayo ambayo yamesisitiza asilimia inayotakiwa kwa chanjo ni 95 duniani, katika nchi zote na jamii zote ili kuwalinda watoto dhidi ya milipuko ya magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa chanjo.

Akisistiza hilo mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema “chanjo ni moja ya nyenzo zetu muhimu sana kwa ajili ya kuzuia milipuko ya magonjwa na kuiweka dunia salama.

Wakati watoto wengi wanapatiwa chanjo siku hizi lakini bado kuna wengi wanaoachwa nyuma na walio katika hatari zaidi ni masikini, waliotengwa, walioathirika na vita na waliolazimika kukimbia makwao.”

Watoto wengi ambao hawajachanjwa kwa mujibu UNICEF na WHO wanaishi katika nchi masikini ambazo hazijiwezi na ziko kwenye athari kubwa za vita.Na Karibu nusu ya watoto hao wote wako kwenye nchi 16 zikiwemo Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Chad, Congo DRC, Ethiopia, Niger, Nigeria, Somalia,na  Sudan Kusini,

Pia imedhihirika kuna pengo kubwa katika fursa ya upatikanaji wa chanjo ambalo linaendelea katika nchi zote ikichangia kwa kiasi kikubwa mlipiko wa surua sehemu mbalimbali duniani ikiwemo katika nchi ambazo kwa ujumla zina viwango vya juu vya chanjo.

Mwaka 2018 karibu visa 350,000 vya surau viliripotiwa duniani kote vikiwa ni zaidi ya mara mbili ya ilivyokuwa 2017. Kwa mujibu wa Henrietta Fore mkurugenzi mtendaji wa UNICEF

(SAUTI YA HENRIETTA FORE)

“Tunatoa wito kwa serikali na wahisani kuwekeza kwenye mifumo bora ya afya ambayo itatoa chanjo bora nay a gharama nafuu kwa Watoto wote, bila kujali ni kina nani na wapi wanakoishi nah ii ijumuishe msaada kwa wahudumu wa afya na wa jamii ili kuwapa wazazi wenye hofu taarifa sahihi za kwa nini chanjo inafanya kazi na kwa nini ni muhimu.”

Ameongeza kuwa magonjwa kama surua ni Ishara halisi ya wapi tunakotakiwa kuongeza juhudi ya kupambana na magonjwa yanayoweza kuzuilika. Kwa sasa mashirika hayo yanasema Ukraine inaoongoza orodha ya nchi zilizoripotiwa kuwa na visa vingi vya surua kwa mwaka 2018. Wakati nchi hiyo sasa imeweza kutoa chanjo kwa asilimia 90 ya watoto wote kiwango kimekuwa kidogo kwa miaka mingi na hivyo kuiacha idadi kubwa ya watoto wenye umri mkubwa na watu wazima bila chanjo na katika hatari ya maambukizi.

Na kwa mara ya kwanza UNICEF na WHO wanasema kuna takwimu kuhusu utoaji wa chanjo dhidi ya virusi vinavyosababisha saratani ya shingo ya uzazi HPV chanjo ambayo inawalinda wasicha dhidi ya saratani hiyo katika siku za usoni.

Takwimu hizo zinaonyesha kwamba hadi kufikia mwaka 2018 nchi 90 kote duniani ambazo ni maskani ya msichana 1 kati ya 3 zimeanza kujumuisha chnjo ya HPV katika program zake za afya. Na ni nchi 13 tu kati ya hizo ndio nchi za kipato cha chini hali inayowaacha mamilioni ya walio katika hatari ya athari za saratani ya shingo ya uzazi katika uwezekano wa kutopata chanjo.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Jason Nyakundi
Audio Duration
4'8"
Photo Credit
UNICEF/Mahmood Fadhel