Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuzo ya Charlemagne kwangu msingi wake ni wanawake na wanaume wa UN- Guterres

Tuzo ya Charlemagne kwangu msingi wake ni wanawake na wanaume wa UN- Guterres

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo amepokea tuzo ya Charlemangne huko mjini Aachen nchini Ujerumani na kusema kuwa ni heshima kubwa sana kwake na kwa chombo anachoongoza. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

Tuzo hiyo ambayo hutolewa kila mwaka tangu mwaka 1950, ni kwa ajili ya watu ambao wanaonekana wako mstari wa mbele kufanikisha muungano wa bara la Ulaya ambapo Guterres katika hotuba yake ya kupokea tuzo hiyo amesema, “ninatambua kuwa mnanituza kupitia mimi kutokana na ahadi, huduma na kujitolea kunakofanywa na wanawake na wanaume walioko Umoja wa Mataifa.”

Amesema kwa kufanya hivyo pia wanatia moyo uimarishaji wa ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Ulaya,” na kwamba kitendo cha kumpatia tuzo kinaonyesha jinsi ambavyo wameona mbali.

Amesema kwa kuzingatia changamoto za dunia ushirikiano kati ya pande mbili hizo kunaweza kuchagiza kukabili changamoto za sasa ambazo ni mabadiliko ya tabianchi, uhamiaji na maendeleo ya teknolojia.

Hata hivyo amesema Ulaya isiyo thabiti itadhoofisha ushirikiano wa kimataifa duniani akienda mbali akieleza kuwa

“Umoja wa Mataifa napenda kurudia unahitaji Ulaya iliyo thabiti na iliyoungana. Hata hivyo ili hilo liwezekane, bara la Ulaya linapaswa kutambua baadhi ya changamoto kubwa ambazo inalikabili. Nafikiri kile kinachodhoofisha bara hili ni suala la wakazi wenyewe kutomiliki masuala  yanayohusu bara la Ulaya. Hata nimeanza kuona dalili ya mabadiliko ya mwenendo huo hivi karibuni kwa kuanzia na ongezeko la idadi ya wapiga kura kwenye chaguzi za Ulaya.”

Mwezi Januari mwaka huu Guterres alitangazwa mshindi wa tuzo hiyo ambapo bodi husika ilisema sababu kubwa ya ushindi wake ni jinsi alivyojitolea kuchechemua na kusongesha ushirikiano wa kimataifa kwa misingi ya maadili na malengo ya Muungano wa Ulaya na Umoja wa Mataifa.

Audio Credit
Flora Nducha/Grace Kaneiya
Audio Duration
1'59"
Photo Credit
UNFCCC/James Dowson