Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya ngazi zote za serikali umeiweka pazuri Rwanda.

Ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya ngazi zote za serikali umeiweka pazuri Rwanda.

Pakua

Wawakilishi wa Rwanda kwenye mkutano wa unaotathmini hali ya wanawake unaoendelea mjini New York, Marekani wamesema tangu wanawake walipoanza kushirikishwa moja kwa moja katika shughuli za serikali, Rwanda imepiga hatua kubwa katika nyanja zote. 

"Sisi kama wanawake tunapokuwa wengi katika ngazi za kufanya maamuzi,  inakuwa rahisi kwetu kwamba kila maamuzi yanayofanywa serikalini basi huwa wanawake wameweka mchango   wao ambao unatoka kwenye kujua matatizo hasa  yanayowakabili wanawake", Ni kauli ya Bi Emma Rubagumya mbunge na  mwanakamati wa Kamati ya masuala ya jinsia katika Bunge la Rwanda  ambaye anaiwakilisha nchi yake katika Mkutano wa 63 wa Kamisheni ya hali ya wanawake CSW ulioingia siku yake ya nne hii leo hapa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani.  

Katika mahojiano na Arnold Kayanda wa UN News Kiswahili, mbunge Emma amenieleza hatua zilizopigwa, "wanawake au watoto wa kike walikuwa hawana sheria ambayo inawasaidia kupata urithi. Sasa hivi ni kwamba watoto wa kike au wa kiume wanaweza kupata urithi kutoka kwa wazazi wao kwasababu wanawake waliokuwepo walisema  kwamba si vizuri urithi uwe kwa watoto wa kiume tu. Mambo ya kumiliki mali kama ardhi , mwanzoni wanawake hawakuwa na sheria inayowaruhusu kumiliki mali au ardhi  lakini sasa hivi  sheria tulizonazo zinawaruhusu wanawake kumiliki ardhi."                        

Na kuhusu hatua iliyofikiwa dhidi ya ukatili wa kijinsia nchini Rwanda, Emma Rubagumya anasema, "hatukuwa na sheria ambazo zinawalinda wanawake au zinatoa adhabu kwa watu ambao wamefanya mambo ya unyanyasaji wa jinsia,  lakini sasa hivi kuna sheria. Sasa hiyo ni mifano tu ambayo nimetoa lakini kuna sheria nyingi, kuna mikakati mingi  ambayo wanawake ambao wako kwenye ngazi za uamuzi wanatoa mchango wao. kwa hiyo faida ya kuwa na wanawake katika ngazi za uamuzi ianonekana kabisa Rwanda."  

Audio Credit
Arnold Kayanda
Audio Duration
1'58"
Photo Credit
UNDP Rwanda/Alice Kayibanda