Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yasaidiana na serikali ya Congo-Brazaville kudhibiti homa ya manjano

WHO yasaidiana na serikali ya Congo-Brazaville kudhibiti homa ya manjano

Pakua

Nchini Jamhuri ya Congo, serikali kwa kushirikiana na shirika la afya duniani, WHO na wadau wengine wameendesha kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa homa ya manjano kwenye mji wa bandari wa Pointe Noire na maeneo ya jirani.  Grace Kaneiya na ripoti kamili.

Katika moja ya kliniki mjini Pointe Noire, jamhuri ya Congo, watu wamepanga foleni kupata chanjo dhidi ya homa ya manjano.

Watu hawa wakiwem watoto ni miongoni mwa zaidi ya watu milioni moja wenye umri wa kuanzia miezi Tisa waliopatiwa chanjo katika kampeni hiyo ya siku sita iliyochochewa na kuthibitishwa kwa mgonjwa mmoja wa homa ya manjano tarehe 21 mwezi Agosti mwaka huu.

Kisa hicho kimoja ni kati ya visa shukiwa 200 tangu mwanzoni mwa mwaka huu ambapo Dkt. Ibrahima Socé Fall, mkurugenzi wa WHO barani Afrika akihusika na dharura amesema..

“Homa  ya manjano ni ugonjwa unaoibuka Afrika na watu milioni 400 hivi wako hatarini. Mwelekeo wetu ni kuzuia kabisa ugonjwa huo barani Afrika. Kwa hiyo Congo ni moja ya nchi 27 zilizo hatarini na tangu kisa kimoja kilipothibitishwa Pointe Noire tunaendesha kampeni kusaidia serikali kulinda raia walio hatarini kwa sababu kiwango cha utoaji wa chanjo dhidi ya homa ya manjano bado ni kidogo Congo.”

Ametaja vichochezi vya kuenea kwa homa hiyo barani Afrika kuwa ni kasi kubwa ya kupanuka kwa miji sambamba na usimamizi duni wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambayo huweka mazingira kwa mbu wanaoeneza ugonjwa huo kushamiri.

“Homa ya manjano ni ugonjwa unaoua lakini kwa bahati nzuri tuna chanjo thabiti ambayo inaweza kumpatia mtu kinga maisha yake yote. Kinga ya maisha, kwa hiyo kuchukua hatua haraka kumlinda kila mtu ni mkakati bora zaidi tunaoweza kutekeleza.”

 

Ugonjwa wa homa ya manjano unaenzwana mbu aina ya Aedes aegypti. Kwa mujibu wa WHO mlipuko wa ugonjwa huo maeneo ya mijini hutia hofu kubwa.

Audio Credit
Grace Kaneiya
Audio Duration
2'4"
Photo Credit
Chanjo dhidi ya homa ya manjano.(Picha:WHO)