Katu Nagasaki na Hiroshima zisitokee tena- UN

9 Agosti 2018

Leo ni miaka 73 tangu  Marekani iangushe bomu la atomiki huko Nagasaki nchini Japani ambapo Umoja wa Mataifa umesema hibakusha, ambao ni manusura wa mashambulio ya bomu ya hilo nyuklia huko wamesalia kuwa viongozi wa amani na udhibiti wa kuenea silaha hizo nchini humo na duniani kwa ujumla. Taarifa zaidi na Flora Nducha.

Kengele ikigongwa saa Nne na dakika tano asubuhi mjini Nagasaki, Japan hii leo, muda ambapo bomu liliangushwa kwenye eneo hilo.! Ilikuwa ni kimya na nyuso za watu zikitatazama chini. Wageni ni kutoka ndani na nje ya nchi akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Kengele hii ilitanguliwa na kuweka mashada ya maua kwenye mnara wa kumbukumbu..

Kwa manusura akiwemo Yamasuki Yamashita kumbukizi ya  kilichotokea siku hiyo ya tarehe 9 Agosti mwaka 1945 bado ni dhahiri..

Lilikuwa na nguvu sana, kwa hiyo mama yangu alinivuta chini kwenye sakafu na kufunika mwili wangu kwa mwili wake.”

Akizungumza kwenye tukio hilo Katibu Mkuu Guterres  amesema..

“Manusura wa Nagasaki na Hiroshima au hibakusha wanatambuliwa siyo kwa miji yao ambayo ilisambaratishwa, bali kwa dunia yenye amani ambayo wanaisaka, wanaendelea kupaza sauti zao kwa niaba ya binadamu wote na hivyo ni lazima kuwasikiliza.”

 

Bwana Guterres amesema licha  ya sauti hizo kupazwa na mikataba ya kimataifa kupitishwa ili kudhibiti kuenea kwa silaha hizo hatari, bado mataifa yanaendelea kutengeneza na kupanua umiliki wao wa silaha hizo.

 

Amesema suala la kuondokana na silaha ni kipaumbele cha juu zaidi cha Umoja wa Mataifa na hivyo ametumia hadhira ya Nagasaki kutoa wito kwa nchi zote kuazimia kuondokana na silaha za nyuklia.

Ametaka kila mtu kuazimia kuwa Nagasaki na Hiroshima yawe maeneo ya mwisho duniani kukumbwa na shambulio la nyuklia akisema yeye atashirikiana nao kufanikisha azma hiyo.

Shambulio la Nagasaki lilifanyika siku mbili baada ya lile la Hiroshima ambapo kumbukizi kama ya leo hutumika kuongeza majina ya watu ambao bado wanaendelea kufariki dunia kutokana na athari za bomu hilo la nyuklia.

 

Audio Credit:
Assumpta Massoi/Flora Nducha
Audio Duration:
2'27"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud