Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maeneo ya ndani zaidi ndio yanatupatia changamoto kwenye Ebola, DRC

Maeneo ya ndani zaidi ndio yanatupatia changamoto kwenye Ebola, DRC

Pakua

Tuna matumaini lakini tuko makini zaidi katika kukabiliana na Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, anayehusika na masuala ya dharura, Peter Salama, amesema hayo leo mjini Geneva, Uswisi ikiwa ni mwezi mmoja tangu kutangazwa kwa mlipuko wa Ebola huko DRC.

Bwana Salama ambaye amerejea leo kutoka DRC,  ikiwa ni ziara yake ya pili tangu mlipuko huo wa Ebola, amesema kuna kazi kubwa ya kufanya na hawapaswi kupuuzia ugonjwa huo.

 “Huu ni mlipuko unaohitaji kiasi kikubwa cha vifaa na uwepo nchini humo ili kufuatialia kila kisa kinachoripotiwa na watu ambao wamekutana nao, na kazi hii ngumu itaendelea kwa wiki kadhaa kwa kuzingatia kuwa kuna mgonjwa mpya amethibitishwa jana.”

Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO akasema hivi sasa wanajikita zaidi maeneo ya vijijini ambayo ni magumu kufikika..

“Hatua hivi sasa tumezielekeza vijijini huko Iboko na Itipo. Maeneo haya yote yako chini ya ukanda wa afya wa Iboko. Changamoto ni tofauti kabisa hapa. Tunazungumzia maeneo yaliyo ndani zaidi duniani. Maeneo yenye misitu ambapo zaidi ya asilimia 50 ya wakazi wake ni wa jamii ya asili na tayari wako pembezoni, hivyo wahamasishaji wa kijamii lazima waje na mkakati wa kuwajumuisha na kuwaelimisha.”

Alipoulizwa kuhusu matumaini waliyo nayo , Bwana Salama amesema yanatokana na ukweli kwamba hivi sasa wamepatia chanjo asilimia 98 ya watu wote waliokuwa na makaribiano na wagonjwa waliothibitishwa.

“Chanjo hiyo kwa watu hao imekamilika siku 10 zilizopita na hivyo wanaamini kuwa kundi hilo lina kinga thabiti dhidi ya Ebola,” amesema Bwana Salama.

 

Chanjo hiyo ikiwa imetolewa kwa watu hao, serikali ya DRC nayo wiki hii iliridhia wagonjwa wa Ebola kupatiwa matibabu kwa kutumia dawa tano zilizo kwenye majaribio.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'56"
Photo Credit
WHO/Oka