Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili na usafirishaji haramu wa binadamu wafurutu ada Somalia: IOM

Ukatili na usafirishaji haramu wa binadamu wafurutu ada Somalia: IOM

Pakua

Ukatili wa kijinsia na usafirishaji haramu wa binadamu vimekuwa donda ndugu nchini Somalia, sasa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM lmeamua kuvalia njuga changamoto hizo.

Natts-MAMA….

Somalia ,  sauti ya mama aliyejawa na simanzi, ikieleza ukatili wa kijinsia uliomkabili binti yake mdogo aliyekuwa mwanafunzi wa madrasa shule ya Koran ya Dugsi. Kiranja wa shule hiyo alimnajisi na kumuumiza vibaya na alipoteza maisha kutokana na ukatili huo.

Hata hivyo kilichomshangaza zaidi mama huyu ambaye hakutaka jina lake litajwe ni kwamba

(SAUTI YA MAMA)

“Nilidhani huyo kijana atakabiliwa na mkono wa sharía ya Kiislam, kwani serikali awali ilisema hivyo, kesi iko bayana na kijana ana hatia, lakini nikabaini kuwa kijana aliachiwa huru na hakuna aliyefanya chochote kuhusu hilo”

Maryama Wasame mwanafunzi wa chukuo kikuu cha Afrika Mashariki haamini macho na masikio yake kuhusu mkasa huo, anasema

(SAUTI YA MARYAMA WASAME)

“Nahisi vibaya sana kuhusu kisa hiki, alikuwa msichana mdogo tu wa Kisomali kama mimi, sitaki kitu kama hicho kitokee kwangu, hivyo inanihuzunisha sana kikitokea kwa msichana mwingine , ni kitu kibaya kama binadamu na kama Muislam, kinasambaratisha kabisa mustakhbali wa msichana.”

Kwa mujibu wa IOM hiki ni kisa kimoja tu kati ya vingi vinavyotokea kila uchao Somalia, na sasa limeamua kulishikia bango suala hili kwa kuanzisha mradi maalumu, Julia Hartlieb ni afisa mratibu wa mradi huo wa IOM wa kubambana na ukatili wa kijinsia na usafirishaji haramu wa watu Somalia

(SAUTI YA JULIA HARTLIEB)

“Somalia imeshuhudia vita kwa miongo kadhaa na ukame uliokithiri vimewafanya wahamiaji na watu wasiojiweza kuwa katika hatari ya ukiukwaji wa haki za binadamu kama usafirishaji haramu wa binadamu na ukatili wa kijinsia. Kwa ushirikiano na wadau IOM inatekeleza mradi wa miaka mingi ukijikita na masuala haya zaidi Puntiland. Mradi unaitwa kuzuia usafirishaji haramu wa watoto na ukatili wa kijinsia, pamoja na ulinzi na msaada kwa waathirika Somalia.”

Ameongeza kuwa, usafirishaji haramu wa binadamu ni utumwa wa kisasa na kwa ndani na nje ya Somalia biashara hii imeshamiri. 

Audio Credit
Siraj Kalyango
Audio Duration
2'26"
Photo Credit
Picha: UM/Albert González Farran