Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yafikisha vifaa tiba Taiz, Yemen baada ya kuzuiwa kwa miezi kadhaa

WHO yafikisha vifaa tiba Taiz, Yemen baada ya kuzuiwa kwa miezi kadhaa

Pakua

Kufuatia miezi ya kuzuiwa kuufikia mji wa Taiz nchini Yemen, Shirika la Afya Duniani hatimaye limeweza kufikisha tani 20 za dawa za kuokoa maisha na vifaa tiba vingine kwa mji huo, katika jitihada za kushughulikia mahitaji yanayoongezeka ya dharura ya afya.

Vifaa tiba hivyo vimeelezwa kuwa muhimu katika kukidhi mahitaji ya dharura katika mji huo ambao watu 200,000 wanaendelea kuzingirwa, wakikumbwa na uwezo mdogo wa kufikia usaidizi wa kibinadamu.

Vifaa tiba hivyo ambavyo vilikuwa vimezuiwa kuingia mji wa Taiz kwa kipindi cha wiki nane, hatimaye vimeweza kuwasilishwa kwa hospitali za Al-Thawra, Al-Jumhoori, Al-Rawdha na Al-Ta'aon.

Tangu Aprili mwaka 2015, machafuko yanayoendelea Yemen na usalama mdogo umeendelea kuzuia ufikishaji misaada kwenye mji wa Taiz, na kufikia sasa, mitaa mitatu ya mji huo - ikiwemo Al Mudhaffar, Al Qahirah na Salah - bado haiwezi kufikiwa, ingawa wakazi wake wanahitaji kwa dharura chakula, maji safi na huduma za afya za kuokoa maisha.

Photo Credit
Utoaji huduma za afya nchini Yemen.(Picha:MAKTABA: WHO/Yemen)