Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO Afrika yafanikiwa kuboresha afya ya umma barani Afrika

Wahudumu wa afya Sierra Leone wakifundishwa matumizi ya vifaa vya kielektroniki katika usimamizi na ufuatiliaji wa magonjwa na afya.
WHO/Saffea Gborie
Wahudumu wa afya Sierra Leone wakifundishwa matumizi ya vifaa vya kielektroniki katika usimamizi na ufuatiliaji wa magonjwa na afya.

WHO Afrika yafanikiwa kuboresha afya ya umma barani Afrika

Afya

Jitihada za pamoja za kukabiliana na changamoto za afya ya umma zinazidi kuboresha upatikanaji na utoaji wa huduma za afya. Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika kwa kushirikiana na nchi wanachama na washirika wake linaendelea kutimiza ajenda yake ya mabadiliko ili kuimarisha mifumo ya afya na kuongeza misaada kwa nchi katika ukanda wa Afrika.

Miaka kumi iliyopita, mlipuko wa Ebola ulifichua udhaifu katika mifumo ya afya barani Afrika, kutoka maandalizi na mwitikio wa dharura hadi kudumisha huduma za kawaida za afya.

Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO, Kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amedhibitisha kwamba mafanikio makubwa tayari yamefikiwa katika kuboresha sekta ya afya kwa umma barani Afrika. Akijivunia mafanikio haya amesema,  “tunakuwa WHO ambayo wadau wengi wanataka iwe. Kwa kutumia vyema rasilimali na utaalamu wetu, tunatengeneza mabadiliko endelevu na chanya, kuongeza matokeo na kuzidisha uaminifu kama mshirika wa thamani.”

WHO Afrika, imetoa mifano kadhaa kati ya mafanikio mengi yaliyofikiwa, madhalani muda wa kudhibiti magonjwa ya milipuko umepungua kwa kiwango kikubwa, kutoka siku 418 mwaka 2016, hadi siku 40 kufikia mwaka 2020.

Mapambano dhidi ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele ya kitropiki pia yanaongezeka kasi. Nchi 19 za Afrika zimeondoa angalau ugonjwa mmoja wa kitropiki usiopewa kipaumbele.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa afya kwa umma nchini Uganda Dkt Daniel Kyabanyize,  ametoa ushuhuda wa mafanikio ya ushirikiano na WHO Afrika kwa kusema, “Katika tukio la hivi karibuni, tulikuwa na mlipuko mkubwa wa Ebola nchini Uganda ambao ulianzia katikati ya nchi na tuliweza kushughulikia na kumaliza janga hilo bila ya kuenea katika nchi zilizo jirani yetu.”

Jitihada nyingine ni katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga na mkuu wa mkoa wa Kabadjougou, nchini Côte d'Ivoire Rene Famy amezipokea kwa shukrani kubwa, “Nina furaha kwamba Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni limekubali kutuunga mkono katika mapambano dhidi ya vifo vya akina mama wakati wa kujifungua.”

Wafanyakazi waliopata mafunzo mazuri ni muhimu kwa huduma za afya na WHO Afrika inaweka juhudi za kuimarisha ujuzi wa wafanyakazi wa afya katika ukanda huo kwa kusaidia katika mafunzo.

Profesa Marycelin Baba, Mkurugenzi wa Maabara ya Kitaifa ya Polio Maiduguri, nchini Nigeria ameeleza jinsi kutoa mafunzo kwa wafanyakazi huchangia moja kwa moja katika maendeleo ya nchi, “wanafunzi wengi wamepata ujuzi na maarifa. Wanafunzi wa tiba na wanafunzi wa taaluma za huduma za dharura wote wamefaidika. Hiyo ni maendeleo ya binadamu, ambayo hayawezi kamwe kupuuzwa. Kwa sababu kinachofanya nchi iwe na maendeleo ni binadamu.”

Msaada wa WHO katika ukanda wa Afrika tayari umeimarisha maisha ya watu wengi. Kwa ushirikiano thabiti kutoka kwa nchi wanachama na washirika, ukanda wa Afrika utaendelea kupata mafanikio makubwa zaidi ya afya ya umma.