Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS: Wananchi wa kaunti ya Nasir watakiwa kuepuka mapigano ili wapelekewe maendeleo

UNMISS: Wananchi wa kaunti ya Nasir watakiwa kuepuka mapigano ili wapelekewe maendeleo

Pakua

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini (UNMISS) umewaeleza wananchi wa Kaunti ya Nasir au Keich Kon iliyoko jimboni Upper Nile nchini Sudan Kusini kuwa ili waweze kurejeshewa huduma za misaada ya kibinadamu ni vyema wakafikia makubaliano ya kusitisha mapigano. 

UNMISS pamoja na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu walifikia uamuzi wa kusitisha huduma zao katika kaunti ya Nasir kutokana nae eneo hilo kutofikika na pia ukosefu wa usalama uliosababishwa na mapigano ya mara kwa mara baina ya wanajamii wa kuanti hiyo, na pia mapigano na kaunti za jirani.

Hata hivyo mwanzoni mwa mwezi huu wa Septemba kilifanyika kikao kilichowaleta pamoja wadau na wananchi baada ya kupatikana uongozi mpya wa kaunti hiyo ambapo katika kikao hicho, wadau wa misaada ya kibinadamu ikiwemo Umoja wa Mataifa waliombwa kurejesha operesheni zao hususan UNMISS, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani (WFP) na wadau wa Sekta ya afya.

Paul Ebikwo ni afisa wa masuala ya kiraia wa UNMISS na akawaeleza anaelewa wasiwasi wao.

“Wasiwasi wenu ni wa halali, ni wa kweli, tunaelewa. Lakini mkiongeza mizozo ndani yake, mnafanya mambo kuwa mabaya zaidi, kwa hivyo hebu tufanye maamuzi ya kuachana, na kuweka kando migogoro na sote tufikirie jinsi ya kutatua maswala haya.”

Bwana Ebikwo aliongeza kuwa suluhu zote za kuzuia ghasia lazima ziongozwe na wanajamii wenyewe huku akitoa wito kwa makundi ya vijana wanaotumia silaha kujiepusha na mapigano na kutafuta amani.

Majadiliano yalihitimishwa kwa wote kukubaliana kuwa na dhamira ya pamoja ya kutafuta njia za kuleta jamii hususani vijana pamoja kwa ajili ya upatanisho na ujenzi wa amani ili kusaidia kurejesha utulivu na kuwezesha jamii katika kaunti ya Nasir kupata ahueni na maendeleo baada ya kuteseka kwa muda mrefu.

Audio Credit
Evarist Mapesa
Sauti
1'56"
Photo Credit
© WFP/Eulalia Berlanga