Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usitishaji uhasama ni lazima Gaza kutokana na ongezeko la hali za dharura

Usitishaji uhasama ni lazima Gaza kutokana na ongezeko la hali za dharura

WHO na UNRWA yasisitiza umuhimu wa sitisho la mapigano Gaza
 
Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la afya duniani, WHO na lile la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina UNRWA, yamezungumzia umuhimu wa sitisho la mapigano huko Gaza ili kufanikisha utoaji wa chanjo kwa watoto dhidi ya magonjwa hatarishi kama vile polio. Assumpta Massoi na taarifa zaidi.
 
(Taarifa ya Assumpta Massoi)
 
Mkurugenzi wa WHO kanda ya Mediteranea ya Mashariki Dkt. Hanan Balkhy akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video kutokea Cairo, Misri amesema hofu yao kubwa ni ugonjwa wa polio aina ya 2 ambao umebainika kwenye sampuli zilizochukuliwa kwenye mazingira huko Gaza. Ingawa hakuna mgonjwa aliyethibitishwa, hatari kwa watoto kuambukizwa ni kubwa hivyo ni vema kuchukua hatua haraka kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.
 
Ndio maana WHO inashirikiana na Wizara ya Afya na UNICEF kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kampeni za chanjo. Hebu nieleweke, tunahitaji sitisho la mapigano hata la muda mfupi ili kuendesha kampeni hizo kwa mafanikio. La sivyo hatari ya virusi kusambaa nje ya Gaza ni kubwa.”
 
 
Mkurugenzi Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini naye kupitia ukurasa wake wa X, zamani Twitter amesema hatari ikiongezeka, chanjo ndio kinga kuu dhidi ya magonjwa.
 
Hivyo kwa ushirikiano na wadau, wahudumu wa afya wa UNRWA wamejizatiti kuongoza kampeni ya chanjo dhidi ya poli kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 8 huko Gaza inayotarajiwa kuanza tarehe 17 mwezi huu wa Agosti.
 
Bwana Lazzarini amesema sitisho la mapigano linahitajika haraka ili kufanikisha upelekaji wa chanjo kwa haraka na kwa usalama Gaza.
 

Pakua
Audio Credit
UN News/ Assumpta Massoi
Sauti
1'33"
Photo Credit
© UNRWA