Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili na uhalifu wa kivita umetekelezwa Myanmar: HRC

Kijana wa umri wa miaka 15 akiwa na magongo. Alikatika mguu baada ya kukanyaga bomu la kutegwa ardhini
© UNICEF/Minzayar Oo
Kijana wa umri wa miaka 15 akiwa na magongo. Alikatika mguu baada ya kukanyaga bomu la kutegwa ardhini

Ukatili na uhalifu wa kivita umetekelezwa Myanmar: HRC

Haki za binadamu

Kuna ushahidi wa kutosha ya kwamba uhalifu wa kikatili wa kivita dhidi ya binadamu uliotekelezwa na jeshi la Myanmar na huenda upinzani na ulisambaa kwa kiasi kikubwa nchini kote, imesema ripoti ya uchunguzi ya jopo huru lililoundwa na Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu kuchunguza matukio ya kipindi cha Julai mosi 2023 hadi Juni 30 wakati upinzani dhidi ya utawala wa kijeshi Myanmar uliposhamiri.

Ripoti hiyo inasema mzozo kati ya jeshi la serikali na vikosi vya upinzani nchini humo unazidi kuwa wa kikatili, na pande zote mbili zina uwezekano wa kuwajibika kwa uhalifu wa kimataifa ikiwa ni pamoja na mauaji ya kiholela,

Katika wito kwa kanda ya ASEAN kusaidia kukomesha ghasia na kuunga mkono juhudi za kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria, mkuu wa uchunguzi wa Baraza la Haki za Binadamu aliyeteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu kuhusu hali ya dharura ya Myanmar Nicholas Koumjian ameelezea halii inayozidi kuwa ya kukatisha tamaa ya Junta ambayo mbinu zake za kijeshi zilikuwa zikitumika zilikwenda sanjari na za wapiganaji wa upinzani bila kuawajibishwa.

Ongezeko la mashambulizi

Bwana Koumjian amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba "Mashambulio ya mabomu ya angani yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika mwaka huu uliopita. Katika jimbo la Kayah mwezi Februari mwaka huu, watoto wanne waliuawa na karibu 10 walijeruhiwa wakati ndege za kivita zilipoangusha mabomu na kufyatua risasi kwenye shule."

Ameongeza kuwa wachunguzi wake pia wameona video "iliyoonyesha vikosi vya upinzani vikiwakata vichwa wanajeshi wawili waliokamatwa huko Loikaw katika jimbo la Kayah mwezi Novemba na Desemba mwaka jana pamoja na video nyingine iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii ya vijana wawili wakichomwa moto hadi kufa katika mkoa wa Magway. Kwa hivyo, aina hii ya ukatili wa kutisha unaendelea".

Mfumo muru wa uchunguzi kwa ajili ya Myanmar (IIMM) uliundwa na Baraza la Haki za Kibinadamu mwaka wa 2018 ili kukusanya ushahidi wa uhalifu mbaya zaidi wa kimataifa uliofanywa nchini Myanmar tangu 2011na leo imetoa ripoti yake ya hivi karibuni ya kila mwaka.

Raia hulengwa mara kwa mara

Bwana Koumjian amebainisha kuwa "Kwa bahati mbaya, kile ambacho ripoti yetu inaeleza ni kwamba kiwango cha uhalifu huu kinaongezeka tkwa kasi na mzozo wa silaha unaongezeka huku ukatili na uhalifu ukitokea mara kwa mara,"

Nicholas Koumjian, mkuu wa IIMM
UN News/Vibhu Mishra
Nicholas Koumjian, mkuu wa IIMM

Mtaalamu huyo mkongwe wa haki za binadamu na mwendesha mashitaka wa zamani wa kimataifa wa haki ya jinai ametoa maoni yake kwamba jeshi ambalo lilichukua mamlaka nchini Myanmar tarehe 1 Februari 2021 lilikuwa linazidi kuwa na tamaa katika kipindi kilichoangaziwa na ripoti hiyo kuanzia tarehe 1 Julai 2023 hadi 30 Juni 2024 wakati ambapo migogoro ya silaha iliongezeka kote Myanmar huku changamoto za utawala wa kijeshi zikiongezeka.

"Walengwa wa milipuko hiyo huwa ni raia mmara nyingi . Shule, makanisa na hospitali mara nyingi ndizo miundo mbinu pekee katika eneo hilo na hiyo ndiyo inayopigwa mabomu."

Ushawishi wa ASEAN

Katika ombi la moja kwa moja kwa ASEAN, Bwana Koumjian ameisihi kuchukua hatua kutokana na ushahidi mkubwa kwamba jeshi la Myanmar lilitekeleza uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa kasi cha kutisha kwa kuweka shinikizo kwa serikali ya kijeshi kusitisha mzozo.

Amesema “ASEAN ni mdau muhimu sana nchini Myanmar, kulingana na uchunguzi wa haki za binadamu imeandaa makubaliano ya vipengele vitano vya kumaliza mapigano ambayo yametiwa saini na jeshi lenyewe".

Hata hivyo, amesema "tunaona badala yake ongezeko la ghasia na ongezeko la machafuko yanayolenga raia. Kwa hivyo, nadhani ni wakati wa ASEAN kuweka kutia sauti katika makubaliano hayo. Haitoshi tu kusema tunaunga mkono kukomesha ghasia, lazima kuwe na hatua zilizochukuliwa kuhakikisha kwamba, kwa kweli, ghasia hizo zimekwisha.”

Ushahidi uliokusanywa

Mkuu wa IIMM alibainisha kuwa ripoti ya jopo hilo imetokana na taarifa na ushahidi uliokusanywa kutoka vyanzo zaidi ya 900, ikiwa ni pamoja na zaidi ya mashahidi 400 walioshuhudia, pamoja na ushahidi wa ziada kama vile picha, video, nyenzo za sauti, hati, ramani, picha za kijiografia, machapisho ya mitandao ya kijamii na ushahidi wa kimahakama.

Ameongeza kuwa kupambana na ukwepaji  wa sheria bado ni lengo kuu la IIMM ambalo limewasilisha matokeo yake na ushahidi kwa mamlaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, Mahakama ya Kimataifa ya Haki na nchini Argentina.