Pongezi IOC kwa kuendelea kujumuisha wanariadha wakimbizi kwenye Olimpiki- Guterres
Pongezi IOC kwa kuendelea kujumuisha wanariadha wakimbizi kwenye Olimpiki- Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye yuko Paris Ufaransa kuhudhuria ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ya majira ya joto mwaka 2024 amezungumza katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach na kuipongeza kamati hiyo kwa kuendelea kuwajumuisha wakimbizi wanamichezo.
Hakika Leah! Hotuba ya Katibu Mkuu imeoanisha michezo ya Olimpiki na amani na jinsi ilivyoweza kuwapatia fursa wanamichezo waliofurushwa makwao kutokana na vita kuweza kuonesha vipaji vyao kwenye michezo hiyo.
Guterres amesema napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kile ambacho Kamati hii ya Olimpiki imefanya kwa kuruhusu timu ya wakimbizi kushindana kwa mara nyingine tena kwenye michezo ya Olimpiki.
Amesema yeye alikuwa Kamishna Mkuu wa wakimbizi kwa miaka 10 na ni muhimu sana kutomwacha mtu yeyote nyuma, na zaidi kutowaacha nyuma wale waliolazimika kukimbia, kuacha nchi zao na wana haki sawa ya kushiriki michezo kama raia wengine wa dunia.
Amezungumzia pia umuhimu wa nchi zilizo kwenye mizozo kuzingatia sitisho la kwanza kabisa la mapigano wakati wa michezo ya Olimpiki karne ya 8 huko Ugiriki ili kuepusha mashambulizi wakati wa michezo.
Guterres amesema tunaishi katika dunia iliyogawanyika, ambako mizozo inaendelea kwa kiasi kikubwa kuanzia Ukraine hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Hivyo amesema katika zama kama hizo, ni muhimu kusema kuzingatia sitisho hilo la mapigano la kwanza duniani.
Amesisitiza kuwa michezo ya Olimpiki inapoanza ni wakati wa kukumbusha dunia kuzingatia sitisho hilo la mapgano ili kuifanya dunia itambua umuhimu wa kunyamazisha silaha.
Katibu Mkuu ametaka nchi zote duniani zishikamane pamoja kama ilivyo kwa wanamichezo wa Olimpiki ambao wanacheza bila kujali tofauti zao.
Michezo ya olimpiki ya majira ya joto inaanza Julai 26 hadi tarehe 11 Agosti, ikifuatiwa na ile ya watu wenye ulemavu itakayoanza tarehe 28 Agosti hadi tarehe 8 Septemba nchini Ufaransa.