Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

SIMULIZI: Mafunzo kutoka ILO Côte d'Ivoire yametuepusha kutumikisha watoto - Oumarou

Yabao Oumarou ni mkulima wa kakao anayeishi Bagoliéoua, kwenye mkoa wa Nawa nchini  Côte d’Ivoire.
© ILO/Anders Johnsson
Yabao Oumarou ni mkulima wa kakao anayeishi Bagoliéoua, kwenye mkoa wa Nawa nchini Côte d’Ivoire.

SIMULIZI: Mafunzo kutoka ILO Côte d'Ivoire yametuepusha kutumikisha watoto - Oumarou

Ukuaji wa Kiuchumi

Mimi ni mtoto wa wakulima wa kakao na nimekuwa nikifanya kazi kwenye shamba Côte d'Ivoire. Kama wakulima wengi, nilitaka kusaidia katika mapambano dhidi ajira ya watoto katika jamii yetu. Kupitia mafunzo, niligundua umuhimu wa kuboresha usalama na afya kazini katika mapambano haya.

Jina langu ni Yabao Oumarou na nina umri wa miaka 46. Nimeoa na nina watoto sita. Mimi ni mwanachama wa kikundi cha ushirika cha wakulima huko Bagoliéoua, katika eneo la Nawa nchini Côte d'Ivoire. Nililelewa hapa na mimi ni mtoto wa mkulima. Hapa, sote ni wakulima. Siku moja, ushirika uliniambia kuwa nilichaguliwa kwenda Soubré kwa ajili ya mafunzo ya WIND yaliyoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi duniani (ILO).

Hadi wakati huo, nilikuwa nikifanya kazi kama wakulima wote wa kakao, nikifanya kazi zile zile ambazo wazazi wetu walifanya kabla yetu. Tulifanya kazi bila kujali afya na usalama wetu. Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa hapo awali.

Yabao Oumarou ni mkulima wa kakao anayeishi Bagoliéoua, kwenye mkoa wa Nawa nchini  Côte d’Ivoire.
© ILO/Anders Johnsson
Yabao Oumarou ni mkulima wa kakao anayeishi Bagoliéoua, kwenye mkoa wa Nawa nchini Côte d’Ivoire.

Msukumo wangu wa kufanya mafunzo ulikuwa kusaidia kupambana na ajira ya watoto. Katika ushirika wetu, kumekuweko na kampeni kadhaa za uhamasishaji kuhusu ajira ya watoto, kwa hiyo ni mada muhimu kwa wakulima wote.

Lakini mazoezi hayo yalikuwa uvumbuzi wa kweli kwangu. Hatukujifunza tu kuhusu ulinzi wa watoto. Tulijifunza pia kuhusu afya, usalama na kutoa huduma za ustawi.

Tuligundua kuwa kuna mambo ambayo hatupaswi kufanya kazini na kuna mambo ambayo tunahitaji kuboresha.Zaidi ya yote, mafunzo yalibadilisha mtazamo wangu kuhusu ajira ya watoto.

Nilikuja kuelewa kuwa ikiwa hutajali afya yako, basi hutaweza kufanya kazi. Na ikiwa huwezi kufanya kazi yako ipasavyo, basi utakuwa mzigo kwa mke wako au kwa watoto wako.

Mabadiliko baada ya mafunzo ya WIND

Nilitenga eneo la mapumziko shambani lenye kiti na kiegemeo. Ninapokuwa ninafanya kazi, kuna wakati ninachoka, kwa hiyo sasa niña mahali pa kupumzika kivulini
© ILO/Anders Johnsson
Nilitenga eneo la mapumziko shambani lenye kiti na kiegemeo. Ninapokuwa ninafanya kazi, kuna wakati ninachoka, kwa hiyo sasa niña mahali pa kupumzika kivulini

Baada ya mafunzo kumalizika, ilikuwa ni wakati wa kutenda kile tulichojifunza.

Nilipofika kijijini, nilifunika kisima changu, ambacho kilikuwa wazi. Pia, nilitengeneza uzio kwa ajili yake kwa sababu mara nyingi wanyama walikuwa wakianguka ndani. Nilifanya uzio kwa bidhaa za kienyeji, na sikulipa chochote. Tulijifanyia wenyewe na kile tulichokuwa nacho. Hatukujua kuwa tunaweza kufanya hivyo.Vilevile, nilifunga kapi kwenye kisima. Tulikuwa tukichota maji moja kwa moja na chombo lakini sasa ni rahisi kuchota maji bila kuchoka au kuhatarisha maisha.

Hatukuwa tunajali afya zetu. Tulifanya kazi tu hadi tulipougua. Sasa, kuna mabadiliko halisi - Oumarou

 Kabla ya mafunzo ya WIND, nilikuwa nikifanya kazi kwenye shamba hadi nachoka sana kiasi kwamba nililazimika kurudi kijijini kwa sababu ya uchovu.Sasa, nimeunda eneo la kupumzika shambani na viti vilivyo na sehemu za kuegemeza mgongo. Ninapokuwa kazini na ninahisi nimechoka, naenda kivulini kwenye eneo la kupumzika. Baada ya hapo, naweza kuanza tena kazi na narudi nyumbani bila kuchoka.

 Juzi, mvua ilianza kunyesha tulipofika shambani. Kabla ya kuwa na sehemu hiyo ya kupumzika, tungehitaji kurudi kijijini na kupoteza siku ya kazi. Badala yake, wakati huu, tulikaa chini ya hifadhi hiyo hadi mvua ilipokoma na kisha tukafanya kazi.

Hawa ni watoto wangu watatu. Tumewaandikisha shuleni na wanajifunza kila kitu. Watakuwa na uwezo wa kusoma na kuandika, watakuwa na uwezo wa kuwa bora kuliko sisi.
© ILO/Anders Johnsson
Hawa ni watoto wangu watatu. Tumewaandikisha shuleni na wanajifunza kila kitu. Watakuwa na uwezo wa kusoma na kuandika, watakuwa na uwezo wa kuwa bora kuliko sisi.

Mafunzo yameamsha dhamira yangu ya usalama na afya.Niliona kuwa lazima ufikirie kuhusu afya yako na afya ya familia yako kabla ya kuchukua kazi yoyote. Sasa ninajiuliza: "Nataka kufanya hili. Lakini litaniletea nini? Je,litanifanya niwe mgonjwa?". Hapo awali, hatukujali kuhusu hilo.

Ikiwa unaweza kufanya kazi yako ipasavyo, bila uchovu mwingi, basi hutakuwa na tatizo la ajira ya watoto, kwa sababu hutahitaji kuwaleta watoto katika kazi hiyo. Sasa, tunajali afya na usalama wetu wenyewe, na hili linaturahisishia kupeleka watoto shule. Tunaweza kuwapa watoto wetu fursa ya kustawi.

Afya na ustawi wa watoto sasa unapatiwa kipaumbele

Kama kila mtu angefanya mafunzo ya aina hii, maisha yangekuwa rahisi. Tungeweza kufanya kazi zetu kwa urahisi, kwa usalama na bila kuchoka. Tungebakia na muda mwingi na kipato kizuri.Baada ya mafunzo haya, naona kuwa kumekuwa na mabadiliko mengi. Tunawafahamisha watu kuwa watoto wana haki. Mahali pa mtoto ni shuleni. Haupaswi kumtwika mtoto asiye na hatia majukumu yako.

Ikiwa unaweza kufanya kazi yako ipasavyo, bila uchovu mwingi, basi hutakuwa na tatizo la ajira ya watoto, kwa sababu hutahitaji kuwaleta watoto katika kazi hiyo - Oumarou

Sasa, jamii inaweza kuona kuwa afya na usalama ni muhimu. Mwanzoni, baadhi ya watu walichukia kile tulichokuwa tunafanya. Lakini tangu wakati huo, wengi wanakuja kuona maendeleo  ambayo nimeyafanya nakuyaiga nyumbani kwao. Wengine wanakuja kwangu kwa maarifa na pamoja, tunabadilishana uzoefu.

Nitaendelea kufanya maboresho. Nimejenga bwawa ndogo la samaki na pia ninapanga kulima nyanya na bamia. Kwa kweli, nina kazi nyingi za kufanya. Kuna mabadiliko mengi yanayokuja. Natarajia nitakuwa na kipato kizuri baada ya maboresho haya yote. Hali yangu ya maisha itakuwa nzuri zaidi.

Hapo awali, hatukuwa hata na wazo la mseto. Sasa, nina kondoo. Kwanza, ilikuwa moja, kisha mbili na sasa tatu. Naona kuwa nitafaulu. Yote yatakuwa shwari.

FAHAMU 

Tangu nimepata mafunzo, ninaona kuna mabadiliko. Ni kwa sababu ya ujasiri na dhamira nimekuwa na uwezo wa kufanya marekebisho na kila kitu kinakwenda sawa
  •  Mradi wa WIND wa ILO (Work Improvement in Neighborhood Development) umetumika kuwafundisha wakulima wa kakao huko Côte d’Ivoire kuchukua jukumu la kuongeza usalama kazini kwa wafanyakazi wa watu wazima na kupunguza utegemezi wa wazazi juu ya ajira ya watoto.
  •  Yabao Oumarou alipata mafunzo ya WIND kama sehemu ya mradi wa ILO "Kuharakisha hatua za kutokomeza ajira ya watoto katika minyororo ya usambazaji Afrika" (ACCEL Africa) huko Côte d'Ivoire.
  •   Mradi huo unalenga kuharakisha kutokomeza ajira ya watoto Afrika kupitia hatua zilizolengwa katika minyororo ya usambazaji ya kakao, pamba, kahawa, chai na dhahabu huko Côte d'Ivoire, Ghana, Kenya, Mali, Nigeria, na Uganda.
  • Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi ni mshirika wa maendeleo wa ILO kwa ACCEL Africa. Pata maelezo zaidi kuhusu msaada wa Uholanzi kwa ACCEL Africa katika mahojiano ya video hapa chini na Britt Evers, Afisa wa Sera ya Biashara kwa Maendeleo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Uholanzi.
  • Makadirio ya Ulimwengu ya Ajira ya Watoto ya ILO 2020 yanaonyesha kwamba, kwa mara ya kwanza katika miaka 20, idadi kamili ya watoto katika ajira ya watoto imeongezeka kutoka milioni 152 mwaka 2016 hadi milioni 160 mwaka 2020.
  • Mwaka 2020, watoto milioni 92 barani Afrika - takriban mmoja kati ya kila watoto watano wa Kiafrika - walikuwa katika ajira ya watoto. Zaidi ya 80% ya ajira ya watoto inafanyika katika kilimo, hasa ndani ya familia.
  • Mnamo Juni 12, ILO inaadhimisha Siku ya Dunia ya Kupambana na Ajira ya Watoto ili kukuza uelewa na hatua za pamoja za kumaliza ajira ya watoto duniani kote.