Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia na Pakistani miongoni mwa wajumbe wapya watano wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la UN

Taswira ya chumba cha Baraza la Usalama la UN wakati wajumbe walipokutana 08 Desemba 2023 kwa kikao cha Mashariki ya Kati hususan suala la Palestina kufuatia Katibu Mkuu kutumia Ibara ya 99 ya Chata kuitisha kikao hicho.
UN /Loey Felipe
Taswira ya chumba cha Baraza la Usalama la UN wakati wajumbe walipokutana 08 Desemba 2023 kwa kikao cha Mashariki ya Kati hususan suala la Palestina kufuatia Katibu Mkuu kutumia Ibara ya 99 ya Chata kuitisha kikao hicho.

Somalia na Pakistani miongoni mwa wajumbe wapya watano wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la UN

Amani na Usalama

Leo katika kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hapa New York Marekani umefanyika uchaguzi wa wajumbe watano wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Wajumbe waliochaguliwa ni Denmark, Ugiriki, Pakistani, Panama na Somalia wataanza kazi zao rasmi Januari 1, 2025 na kufanya kazi hadi Desemba 31, 2026.

Nchi hizo tano zilishindania viti vitano na wajumbe hao wasio wa kudumu waliochaguliwa watajaza viti vilivyoachwa wazi vya Kundi la Afrika ambalo kwa sasa linashikiliwa na Msumbiji, Kundi la Asia-Pasifiki ambalo kwa sasa linashikiliwa na Japan, Kundi la Amerika ya Kusini na Karibea ambalo kwa sasa linashikiliwa na Ecuador na viti viwili vya Vikundi vya Ulaya Magharibi na Vikundi Vingine ambavyo kwas asa vinashikiliwa na Malta na Uswisi.

Wajumbe waliochaguliwa walishawahi kushika wadhifa huo

Tweet URL

Nchi zote tano zilizochaguliwa leo hapo awali ziliwahi kuwa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo Pakistan mara saba, Panama mara tano, Denmark mara nne, Ugiriki mara mbili na Somalia mara moja.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni moja ya vyombo sita vikuu vya Umoja wa Mataifa na linajumuisha nchi 15, ambapo tano kati yake Uingereza, Ufaransa, Uchina, Urusi na Marekani ni wanachama wa kudumu walio na kura ya turufu. Wale kumi waliosalia huchaguliwa na Baraza Kuu kwa kipindi cha miaka miwili.

Kura kwa wajumbe wa Baraza la Usalama

Kila mwanachama wa Baraza la Usalama ana kura moja. Chini ya Chata ya Umoja wa Mataifa, nchi wanachama zinakubali kutii na kutekeleza maamuzi ya Baraza la Usalama.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina nafasi kubwa katika kubainisha iwapo kuna tishio kwa amani au kitendo cha uchokozi. 

Linahimiza wahusika katika mzozo kusuluhisha kwa njia ya amani na kupendekeza njia za utatuzi. 

Katika baadhi ya matukio, Baraza la Usalama linaweza kuwekea vikwazo au hata kuidhinisha matumizi ya nguvu ili kudumisha au kurejesha amani na usalama wa kimataifa. 

Wajumbe wa Baraza la Usalama hubadilishana kuwa mwenyekiti wa Baraza la Usalama kwa muda wa mwezi mmoja mmoja.