Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimesikitishwa tulishindwa kulinda watumishi wetu Gaza – Guterres

Mfanyakazi wa UNRWA akihudumia watoto Gaza
© UNRWA
Mfanyakazi wa UNRWA akihudumia watoto Gaza

Nimesikitishwa tulishindwa kulinda watumishi wetu Gaza – Guterres

Masuala ya UM

Hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa leo kumefanyika tukio la kila mwaka la kukumbuka wafanyakazi 188 wa chombo hicho waliouawa mwaka 2023 pekee wakiwemo 135 watumishi wa UNRWA waliouawa ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi yaliyoanza Oktoba 7, 2023 baada ya wanamgambo wa Hamas kushambulia Israeli na ndipo Israeli ikaanza kujibu mashambulizi hadi leo hii.

Tweet URL

Tukio lilianza kwa wimbo wa maombolezo kutoka kwa mpiga fidla na kisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiambatana na Rais wa Baraza Kuu Balozi Dennis Francis na Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingia ukumbini wakiambatana na baadhi ya wanandugu wa watumishi wa Umoja wa Mataifa waliouawa wakiwa kazini.

Baada ya hapo tukio la kuwashwa kwa mshumaa lilifuata na ndipo Katibu Mkuu Guterres akasogelea mimbari na kutoa hotuba yake ya kurasa mbili.

“Leo tunakumbuka na kuenzi wafanyakazi 188 wa Umoja wa Mataifa waliopoteza maisha yao mwaka 2023 wakiwa kazini. Nakaribisha ndugu zao walioungana nasi hapa ukumbini na wanaoungana nasi kwa njia ya mtandao,”  amesema Katibu Mkuu

Miongoni mwa waliouawa ni watumishi wake kwa waume 135 wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA huko ukanda wa Gaza.

“Hiki ni idadi ya juu zaidi ya watumishi kuuawa katika mzozo au janga moja la asili tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, ukweli ambao hatuwezi kuukubali,” amesema Guterres.

Wahusika wa  mauaji  wawajibishwe

Katibu Mkuu amesema narejelea wito wangu wa kutaka uwajibikaji kamilifu wa kila kifo. Tuna deni kwa familia zao, marafiki zao, wafanyakazi wenzao na dunia nzima.

Katika tukio hilo majina na nyadhifa za watumishi hao wote 188 yalisomwa moja baada ya jingine huku yakioneshwa kupitia skrini kubwa iliyokuwa imewekwa kwenye ukumbi wa Baraza la Udhamini la UN kulimofanyika tukio hilo, ukumbi ukiwa umepambwa kwa maua.

Kwa mujibu wa Guterres, watumishi hao walikuwa ni walimu, madereva, madaktari, wahudumu wa huduma za kujisafi na usafi, walinzi, wafamasia, watoa huduma za utawala na kazi nyingine nyingi.

“Walikuwa mama, baba, watoto, waume, wake. Wote walikuwa wafanyakazi wenzetu na marafiki zetu.”

Nimechukizwa hatukuweza kuwalinda

Katibu Mkuu amesema amechukizwa sana kwani licha ya juhudi za Umoja wa Mataifa, walishindwa kuwalinda wafanyakazi hao Gaza.

Guterres amesema licha ya tofauti lazima tukubali kuwa wale wanaohudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa wana haki ya kulindwa.

Kisha ilifuatia dakika moja ya kukumbuka waliopoteza maisha na Katibu Mkuu akatamatisha hotuba yake kwa kusema kuwa “tunawashukuru wenzetu waliopoteza maisha kwa huduma yao. Tutafanya kadri tuwezavyo kusaidia familia zao, tutaendelea kuimarisha kanuni zetu za usalama na tutasongesha kumbukumbu zao.”

Kwa ujumla wafanyakazi wote 188 wanatoka nchi 37 na mashirika na taasisi 18 tofauti za Umoja wa Mataifa.