Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati kuivusha Afrika – Guterres

Profesa Amivi Kafui Tete-Benissan (kushoto) ambaye anafundisha biolojia na kemia kwenye chuo kikuu cha Lomé, Togo, pia ni mwanaharakati ambaye anachagiza wasichana kushirika kazi za sayansi.
World Bank/Stephan Gladieu
Profesa Amivi Kafui Tete-Benissan (kushoto) ambaye anafundisha biolojia na kemia kwenye chuo kikuu cha Lomé, Togo, pia ni mwanaharakati ambaye anachagiza wasichana kushirika kazi za sayansi.

Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati kuivusha Afrika – Guterres

Utamaduni na Elimu

“Afrika Tuitakayo” haina budi kuungwa mkono na mifumo ya elimu ambayo Afrika inahitaji, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati wa moja ya kikao cha ngazi ya juu cha Mlolongo wa Mijadala ya Afrika iliyokunja jamvi hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Mlolongo huo wa mijadala uliofanyika kwa mwezi mzima ukiwa umeandaliwa na Ofisi ya Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Afrika, UNOSAA, ulijikita katika marekebisho ya mfumo wa elimu ambapo Guterres amesema maudhui hayo yanakumbusha kuwa kuwezesha bara la Afrika kustawi, kiambato muhimu ni elimu.

Katika kikao hicho cha leo kilichomulika Elimu kupitia Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kuelekea Afrika Tuitakayo, Guterres amesema elimu ni kichocheo cha ustawi na maendeleo ya Afrika na ndio injini ya fursa kwa vijana wa kiafrika na zaidi ya yote elimu inaunganisha waafrika na urithi wa utamaduni wa zamani huku ikiwaandaa kwa siku zijazo.

Hata hivyo amesema mizozo na majanga yahusianayo na tabianchi yamefanya elimu kusalia ndoto kwa mamilioni ya watoto na vijana barani Afrika, huku kukiwa hakuna walimu wenye sifa zinazotakiwa na mbinu za kufundishia zinashindwa kuwaandaa wanafunzi kwa ajira kwenye zama za dunia ya sasa hasa kwa kuzingatia umuhimu wa masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati au STEM.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia Kikao cha ngazi ya juu cha kisera cha mlolongo wa mijadala ya Afrika kwa mwaka huu wa 2024 kikimulika Kufikia Afrika tuitakayo kupitia Sayansi, Teknolojoia, na Ugunduzi.
UN Video
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia Kikao cha ngazi ya juu cha kisera cha mlolongo wa mijadala ya Afrika kwa mwaka huu wa 2024 kikimulika Kufikia Afrika tuitakayo kupitia Sayansi, Teknolojoia, na Ugunduzi.

Guterres anapigia chepuo ufadhili zaidi kwenye mifumo ya elimu na zaidi ya yote msingi wa mifumo ya elimu barani Afrika ijikite kwenye STEM.

“Kuongeza idadi ya watoto shuleni pekee haitoshelezi, kinachohitajika ni stadi na ufahamu zaidi wa kuweza kushindana kwenye uchumi wa kisasa wa dunia,” amesema Guterres.

Rais wa Baraza Kuu naye apazia sauti Sayansi, Teknolojia na Ugunduzi

Balozi Dennis Francis ambaye ni Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na kuunga mkono hoja ya kusongesha STEM na ubia katika kuimarisha mfumo wa elimu Afrika, yeye ametanabaisha kuwa sayansi, teknolojia na ugunduzi (STI)  vitaziba pengo la kidijitali  na hivyo kuchochea suala la kupata elimu bora Afrika, na kuimarisha tafiti na kupunguza kasi ya wasomi wa Afrika kukimbia bara lao.

“Tukiwa na mwelekeo tulioazimia, STI inaweza kuchochcea maendeleo ya viwanda Afrika na kuleta mabadiliko mapana ya kiuchumi ambayo yanaweka fursa zaidi na bora za ajira kwa watu wote,” amesema Balozi Francis.

Amenukuu maneno ya Hayati Nelson Mandela ya kwamba Elimu ndio silaha yenye nguvu zaidi tunayoweza kuitumia kubadilisha dunia.”

Fahamu kuhusu Mwezi wa AFRIKA UN mwaka 2024

Mfululuzo wa majadiliano ya Afrika kwa mwaka 2024 yanayofanyika ana kwa ana Kwenye Umoja wa Mataifa na kupitia katika njia ya mtandao mwaka huu yamejikita katika maadhui ya ‘elimu kupitia sayansi, teknolojia na ubunifu kwa ajili ya Afrika tunayoitaka”

Kwa mujibu wa UNOOSA idadi ya watoto wasio shulen iimepungua katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, kazi inaendelea barani kote kuchagiza maendeleo. Majadiliano haya yanafanyika wakati juhudi za pamoja za kisera barani Afrika za kubadili mwelekeo na kurekebisha mfumo wa elimu zikiendelea. Mfumo wa elimu unaotakiwa ni ule unaotokana na mazingira ya Afrika.

Hiyo ni kwa mujibu wa wito aliotoa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kwenye ripoti yake iitwayo “Ajenda yetu ya Pamoja”akitaka ubunifu na ugunduzi viwe kitovu cha utungaji wa sera na kuondokana na kufanya kazi kwa mazoezi pindi linapokuja suala la kutatua changamoto za zama za sasa.

Msaidizi wa Katibu Mkuu na MShauri Maalum kuhusu Afrika, Cristina Duarte, akizungumza na waandishi wa habari jijini New York kuhusu Mazungumzo kuhusu Afrika au ADS2024
UN Photo/Manuel Elías
Msaidizi wa Katibu Mkuu na MShauri Maalum kuhusu Afrika, Cristina Duarte, akizungumza na waandishi wa habari jijini New York kuhusu Mazungumzo kuhusu Afrika au ADS2024

Kwa hiyo, wakati huu ambapo dunia inajiandaa kwa ajili ya  Mkutano wa viongozi wa zama zijazo kuonesha kwamba ushirikiano wa kimataifa unaweza kutatua changamoto za sasa, viongozi wa Afrika na washirika wao duniani kote wamekutana mwezi huu wa Mei kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York, Marekani kushiriki kwenye Mwezi wa Afrika ndani ya UN kupitia mijadala ya Afrika.

Mjadala huo ndio unakamilishwa na kikao cha ngazi ya juu cha mashauriano kuhusu sera.

Kwenye kikao hicho cha ngazi ya juu, washiriki wakiwemo mawaziri wanatoa mapendekezo ya jinsi ya kufanikisha ajenda 2030 ya SDGs halikadhalika ile ya Muungano wa Afrika iitwayo Ajenda 2063.

Washiriki wamemulika maudhuri yam waka huu wakijikita katika STEM, ubunifu na ufadhili, elimu kwenye maeneo ya mizozo.

Mijadala hii imeandaliwa na UNOSAA kwa kushirikiana na Ujumbe wa kudumu wa Muungano wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa, AUPOM, halikadhalika mashirika ya  Umoja wa Mataifa likiwemo la Kazi duniani ILO, lile la mawasiliano, ITU, la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, la kuhudumia watoto, UNICEF, la wakimbizi, UNHCR, Benki ya Dunia na Tume ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika, UNECA.