Pamoja na ukarimu wake sasa Afrika yalemewa na mzigo wa wakimbizi:UN
Afrika imepongezwa kwa ukarimu wake hasa wa kupokea mamilioni ya watu wanaosaka usalama wakikimbia vita na utesaji. Hata hivyo idadi ya watu wanaotawanywa na kulazimika kukimbia makwao hadi kufikia mwisho kwa mwaka 2017 ilikuwa milioni 24.2 , na kulibebesha mzigo mkubwa wa kiuchumi bara hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya mshauri maalum kwa ajili ya Afrika UNOSAA nchi kama Uganda, Kenya, Tanzania na Ethiopia zimekuwa zikifungua milango yake kwa kiasi kikubwa kupokea wakimbizi lakini ongezeko la jumla ya wakimbizi milioni 4.6 lililoshuhudiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja wa 2017 limeifanya Afrika kubeba mzigo isiouweza sio tu wa kiuchumi bali pia wa mazingira na mfumo wa maisha hasa kwa jamii zinazowahifadhi.
Katika ufunguzi wa mkutano maalumu wa majadiliano ya Afrika kwa mwaka 2019 yaliyoanza leo kwenye makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York yakibeba kauli mbiu “kuelekea suluhu ya kudumu kwa watu waliolazimika kutawanywa barani Afrika” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema,“njia bora ya kuwalinda wakimbizi na wakimbizi wa ndani ni kuzuia wao kutokimbia makwao, na hii inamaanisha kwamba kushughulikia vyanzo ambavyo ni umasikini, vita, ubaguzi na ubaguzi wa aina zote. Ufadhili wa fedha ni muhimu sana nchi zote hususan zilizoendelea ni lazima zitimeze ahadi zilizozitoa kwenye mpango wa hatua wa Addis Ababa.”
Mkutano huu ulioandaliwa na UNOSAA, Muungano wa Afrika (AU), shirika la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wadau wengine unatoa jukwaa la kujadili njia bunifu za ufadhili wa kutoka msaada wa kibinadamu kuelekea kwenye maendeleo katika nchi za Afrika zinazohifadhi wakimbizi na wakimbizi wa ndani.
Mkutano huu pia unalenga kuchagiza msaada kutoka kwa viongozi wa Afrika katika kuhakikisha uridhiaji na upitishaji wa mikakati muhimu ya Afrika na kimataifa ikiwemo mkataba wa Kampala.
Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa Bience Gawanas akizungumza katika mjadala huo amesisitiza kwamba“hali ya watu kulazimika kukimbia makwao Afrika ni inaleta tishio kubwa kwa maendeleo endelevu SDGs , na pia kufikia ajenda ya Muungano wa Afrika ya 2063. Hatuwezi kufikia lengo la kutomuacha yeyote nyuma endapo hatutotafuta suluhu ya changamoto ya watu kulkazimika kukimbia makwao. Nchi zinazohifadhi watu waliolazimika kukimbia zinabeba mzigo mkubwa na zinaifundisha dunia somo la kuwa na huruma na ukarimu.
Majadiliano hayo ya siku tatu yatakayokunja jamvi Mei 23 yamewaleta pamoja viongozi mbalimbali na wawakilishi kutoka barani Afrika, Umoja wa Mataifa, Muungano wa afrika, mashirika ya kimataifa likiwemo shirika la UNHCR, asasi za kiraia, wakimbizi na wadau wengine wa misaada.
Hali halisi
Afrika ndilo bara pekee duniani lililopitisha mkataba wa 2009 wa muungano wa Afrika (AU) wa ulinzi wa wakimbizi wa ndani barani Afrika ujulikanao kama “Mkataba wa Kampala” ambao unashughulikia tatizo la ukimbizi wa ndani lililosababishwa na vita, majanga ya asili na miradi mikubwa ya maendeleo Afrika.
Hadi sasa nchi 27 za Afrika zimeridhia mkataba huo. Na kusisitiza mtazamo wake kuhusu suala la watu waliolazimika kutawanywa, AU Julai mwaka 2018 ilitangaza kuwa mwaka 2019 utakuwa “mwaka wa wakimbizi, watu wanaorejea makwao na wakimbizi wa ndani” chini ya kaulimbiu ya majadiliano ya mwaka huu .
Na katika kuzingatia utekelezaji wa ajenda ya mwaka 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu SDGs, lengo la Afrika ni kusaka suluhu kwa ajili ya watu wanaotawanywa wakati huohuo ikichagiza kuzuia migogoro na mnepo dhidi ya majanga ya asili.