Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufadhili zaidi kwa tabianchi unahitajika ili 'kuhama kutoka mazungumzo hadi hatua madhubuti'

Wafanyakazi hujenga vizuizi ili kukabiliana na mmomonyoko wa bahari kwenye ufukwe wa Tuvalu.
© UNICEF/Lasse Bak Mejlvang
Wafanyakazi hujenga vizuizi ili kukabiliana na mmomonyoko wa bahari kwenye ufukwe wa Tuvalu.

Ufadhili zaidi kwa tabianchi unahitajika ili 'kuhama kutoka mazungumzo hadi hatua madhubuti'

Ukuaji wa Kiuchumi

Hatua dhidi ya tabianchi iliyochukuliwa kufikia sasa kusaidia kufadhili juhudi katika Nchi za Visiwa vidogo vinavyoendelea (SIDS) "hailingani na kile ambacho kimesemwa" kufuatia Mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 uliofanyika huko Dubai mwaka jana 2023.

Huo ulikuwa ujumbe mzito kutoka kwa Rais wa taifa kutoka Pasifiki ya Magharibi, Palau, Surangel Whipps akizungumza katika Mjadala wa leo Jumatano Mei 29 wakati wa Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa SIDS (SIDS4), unaofanyika tangu tarehe 27 Mei nchini Antigua na Barbuda katika Visiwa vya Karibe.
 
Amewaambia wajumbe kuna haja ya kuwa na "mabadiliko kutoka katika maneno matupu hadi hatua madhubuti".
 
Awali wawakilishi kutoka mataifa mawili ya Ulaya waliojitolea kutoa ufadhili wa tabianchi wamesema kwamba jumla ya dola bilioni 115.9 zilikusanywa mwaka 2022 kwa ajili ya hatua dhidi ya tabianchi katika nchi zinazoendelea, zilionesha kuwa maendeleo makubwa yamefanyika.
 
Mnamo mwaka 2009, COP15 ilianzisha lengo la kuhamasisha dola bilioni 100 za Kimarekani kwa mwaka kwa ajili yah atua dhidi ya tabianchi katika ulimwengu unaoendelea hadi kufikia mwaka 2020.
 
Kikao cha leo kimeundwa ili kuzingatia ahadi zilizotolewa huko Dubai ambazo zilianzisha Hazina muhimu ya Hasara na Uharibifu kusaidia SIDS na mataifa mengine yaliyo hatarini kukabiliana na athari za hali mbaya ya hewa, kuongezeka kwa viwango vya bahari na mmomonyoko wa pwani.
 
Rais Whipps amesema kuongeza msaada kwa SIDS sio tu muhimu kwa maisha yao "lakini ni muhimu kwa kutatua changamoto za tabianchi duniani."
Ameongeza kuwa "tunahitaji mifumo thabiti na inayowajibika ya kifedha ya kimataifa ya tabianchi ambayo inatoa matokeo halisi."