Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mambo 8 unayohitaji kufahamu kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu katika karne ya 21

Usafirishwaji haramu wa binadamu.
IOM
Usafirishwaji haramu wa binadamu.

Mambo 8 unayohitaji kufahamu kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu katika karne ya 21

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Usafirishaji haramu wa binadamu ni tatizo kubwa la kimataifa ambalo linaendelea kuathiri mamilioni ya watu, licha ya juhudi kubwa za kukabiliana nalo.

Ili kuangazia suala hili lililoenea, hapa kuna mambo manane muhimu kuhusu biashara haramu ya binadamu katika karne ya 21 ambayo yanasaidia kuelewa vyema kwa nini uhalifu huu hutokea, jinsi waathiriwa husajiliwa na kudhulimiwa, na uhusiano kati ya biashara haramu ya binadamu na uhamiaji, mabadiliko ya tabianchi au migogoro.

1. Usafirishaji haramu wa binadamu hutokea katika maeneo yote ya dunia

Usafirishaji haramu wa binadamu hutokea kila mahali, lakini mara nyingi watu husafirishwa kutoka kwa walio na kipato cha chini kuelekea nchi zenye kipato cha juu.

Huku waathiriwa wengi, (asilimia 60), wakigunduliwa ndani ya nchi, wenzao waliovukishwa mipaka hugunduliwa zaidi katika eneo moja (asilimia 18) au katika mikoa ya karibu (asilimia 6). Ni asilimia 16 pekee ndio hugunduliwa katika mtiririko wa kimataifa na kuishia katika maeneo ya mbali.

Waathiriwa wengi wa biashara haramu ya kuvuka mipaka wanatoka Afrika, hasa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, na kutoka Kusini na Mashariki mwa Asia.

2. Usafirishaji haramu wa binadamu ni uhalifu ulioenea na ni biashara yenye faida kubwa

Usafirishaji haramu wa binadamu ni kusajili, kusafirisha, kuhamisha, kuhifadhi au kupokea watu kwa nguvu, ulaghai au udanganyifu ili kuwadhulumu kwa faida.

Ni vigumu kubaini kiwango cha kweli cha uhalifu huu. Takriban kesi 50,000 ziliripotiwa katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa na Uhalifu (UNODC) mwaka 2020 na nchi 141. Hii ni kiasi cha watu milioni 50 duniani ambacho ni sawa na idadi ya watu wa Korea Kusini au Uganda wanaoweza kukumbwa na aina mbalimbali za dhuluma.

Usafirishaji haramu wa binadamu ni mojawapo ya uhalifu unaokua kwa kasi zaidi , pamoja na madawa ya kulevya na ulanguzi wa silaha, pia ni biashara yenye faida kubwa (isiyo halali) inayozalisha wastani wa faida ya dola bilioni 150 kila mwaka.

"Walk For Freedom" ni siku ya uhamasishaji duniani na upiganaji wa hatua za ndani katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu. (Maktaba)
© Unsplash/Hermes Rivera
"Walk For Freedom" ni siku ya uhamasishaji duniani na upiganaji wa hatua za ndani katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu. (Maktaba)

3. Usafirishaji haramu wa binadamu unastawi kutokana na umaskini, migogoro na mabadiliko ya tabianchi

Usafirishaji haramu wa binadamu unaendeshwa na mchanganyiko tata wa mambo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Migogoro na mateso, umaskini na ukosefu wa utulivu wa kisiasa, ukosefu wa fursa ya elimu na kazi, uhamiaji na uhamisho, ukosefu wa usawa wa kijinsia na ubaguzi, majanga ya asili na mabadiliko ya hali ya tabianchi, yote yanajenga hali zinazochochea usafirishaji haramu wa binadamu.

Huku takribani nusu ya watu duniani wakiishi chini ya dola 6.85 kwa kila mtu kwa siku, au kwa uchache watu bilioni tatu duniani kote wanaishi katika maeneo yaliyoathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira usiohusishwa na tabianchi, mamilioni ya watu wamekuwa kwenye hatari ya kudhulumiwa.

Wasafirishaji haramu hufaidika na hali ya watu kukata tamaa, kutofautiana na kupungukiwa katika maisha; inayolenga watu walio hatarini, waliotengwa au walio katika hali ngumu, ikiwa ni pamoja na wahamiaji wasio wa kawaida au waliosafirishwa kwa njia ya magendo na wale wanaohitaji kazi kwa dharura.

4. Wasafirishaji haramu hutumia kila mbinu kuanzia udanganyifu hadi ukatili kuwasajili na kuwadhulumu waathiiriwa wao

Kwa sababu usafirishaji haramu wa binadamu mara nyingi hauripotiwi una sifa ya mapato makubwa na hatari ndogo kwa wahalifu wake, ambao hupata faida kubwa bila woga wa adhabu.

Wakitumia fursa ya mahitaji makubwa ya kazi nafuu, ngono ya kibiashara au huduma nyinginezo, wahalifu hutumia mapungufu katika sheria na utekelezaji wake, pamoja na watendaji wafisadi na utawala dhaifu, kutekeleza shughuli zao haramu.

Kwa ulaghai wanaahidi maisha bora katika nchi mpya, wanatoa kazi za kusisimua zenye manufaa makubwa, au hutumia ukatili wa moja kwa moja dhidi ya watu walio katika mazingira magumu ili kuwashurutisha katika vitendo vya dhuluma, kama vile unyanyasaji kingono au kazi ya kulazimishwa.

5. Huenda ikawa vigumu sana kuepuka kudhulumiwa

Waathiriwa mara nyingi huvumilia hali zisizo za kibinadamu na hupata ugumu kutoroka kutoka katika mikono ya watekaji wao, ambao hutumia mbinu na hila nyingi kuwandamiza.

Waathiriwa wanaweza kupigwa, kutishiwa na kutumiwa vibaya. Wanaweza kudhalilishwa, kunyanyaswa au kukosa mahali pengine pa kwenda. Pasipoti zao na hati zingine zinaweza kuchukuliwa. Wengi wanaweza hata wasijitambulishe kuwa waathiriwa - jambo ambalo hujitokeza mara nyingi  wanapolaghaiwa na mwenzi au jamaa.

Hofu ya kulipizwa kisasi mara nyingi huzuia waathiriwa kutafuta msaada, na wanaweza kupendelea kwa pakubwa kujiokoa kuliko kuokolewa na mamlaka. Ingawa asilimia 41 ya waathiriwa huripoti wenyewe kwa mamlaka, ni asilimia 28 tu ya kesi ambazo huanza kwa unchunguzi wa moja kwa moja wa polisi.

6. Aina za kawaida za usafirishaji haramu wa binadamu ni unyanyasaji wa kingono na kazi ya kulazimishwa

Usafirishaji haramu wa binadamu unajidhihirisha kwa njia nyingi . Utafiti wa hivi karibuni wa UNODC unaonesha kuwa asilimia 38.7 ya waathiriwa wanasafirishwa kwa ajili ya unyonyanyasaji wa kingono, unaofanyika mitaani, kwenye madanguro, vituo vya masaji, hoteli au baa. Mara nyingi waathiriwa, haswa wanawake na wasichana hupitia ukatili na unyanyasaji uliokithiri.

Asilimia 38.8 zaidi wanadhulumiwa kwa kazi ya kulazimishwa. Watu wengine hufanya kazi katika viwanda kwa muda mrefu, kwa malipo kidogo au bila malipo yoyote; kutengeneza nguo, kompyuta au simu. Wengine hufanya kazi nyanjani, mashambani au katika boti za uvuvi. Mara nyingi wanafanya kazi za kulima mahindi, mchele au ngano, kuvuna kahawa na maharagwe ya kakao au kuvua samaki na dagaa katika hali mbaya ya hewa.

Takriban asilimia 10 wanalazimishwa kujihusisha na shughuli haramu, kama vile wizi, kunyang'anya mifuko, kuombaomba au kuuza dawa za kulevya. Aina nyingine za dhuluma ni pamoja na ndoa ya kulazimishwa, kuondolewa kwa viungo na utumwa wa nyumbani.

7. Wanawake ndio wanaogundulika zaidi kama waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu

Hakuna mtu aliye salama dhidi ya biashara haramu. Watu wa jinsia zote, rika, asili na katika maeneo yote ya dunia huwa mateka wa wasafirishaji, ambao hutumia mbinu mbalimbali kuwasajili na kuwadhuluu.

Wengi wa waathiriwa huwa wanawake na wasichana, ambao ni asilimia 42 na 18, mtawalia. Husafirishwa zaidi kwa unyanyasaji wa kijinsia na wana uwezekano mara tatu zaidi wa kuteswa na ukatili wa kimwili au uliokithiri kuliko wanaume na wavulana.

Wakati huo huo, idadi ya waathiriwa wa kiume waliogunduliwa imeongezeka zaidi ya miaka iliyopita: asilimia 23 ya waathiriwa ni wanaume na asilimia 17 ni wavulana ambao husafirishwa zaidi kwa kazi ya kulazimishwa.

Katika miaka 15 iliyopita, idadi ya watoto kati ya waathiriwa waliotambuliwa wa usafirishaji haramu wa binadamu imeongezeka mara tatu hadi asilimia 35, au theluthi moja ya waathiriwa wote.

Msichana wa umri wa miaka nane akiwa kwenye kituo cha kuhudumia watoto waliosafirishwa kwa njia haramu akiwa Haiti.
UNICEF/Marco Dormino
Msichana wa umri wa miaka nane akiwa kwenye kituo cha kuhudumia watoto waliosafirishwa kwa njia haramu akiwa Haiti.

8. Walanguzi wanaweza kuwa mtu yeyote kutoka kwa washiriki wa kikundi cha uhalifu uliopangwa hadi kwa familia ya mwathirika mwenyewe

Takwimu za UNODC zinaonesha kuwa asilimia 58 ya waliopatikana na hatia ya kusafirisha binadamu ni wanaume. Wakati huo huo, ushiriki wa wanawake katika uhalifu huu ni wa juu zaidi kuliko uhalifu mwingine.Wahalifu wa kike huchukua asilimia 40 ya wale waliopatikana na hatia.

Watu wanaojihusisha na usafirishaji haramu wa binadamu ni kati ya vikundi vya wahalifu hadi watu wenye kutumia fursa zilizopo kuendesha shughuli zao binasfi au katika vikundi vidogo.

Mbali na usafirishaji haramu wa watu, mashirika ya uhalifu mara kwa mara yanahusika katika uhalifu mwingine mkubwa, ikiwa ni pamoja na madawa ya kulevya au biashara ya silaha, pamoja na ufisadi na rushwa ya viongozi wa umma. Vikundi kama hivyo vinadhulumu waathiriwa zaidi, mara nyingi kwa muda mrefu, kwa umbali mkubwa na kwa ukatili zaidi kuliko wahalifu wasiopangwa.

Hata hivyo, wasafirishaji haramu wanaweza pia kuwa wanafamilia wa mwathiriwa, wazazi, wapenzi wa karibu au watu wanaofahamiana nao.

TAARIFA ZAIDI

UNODC ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa (UN) ndiyo chombo kinachoongoza katika kushughulikia mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu . Kinatoa utaalamu na maarifa kwa nchi na kuzisaidia kuidhinisha na kutekeleza Itifaki ya Umoja wa Mataifa ya Kuzuia, Kukandamiza na Kuadhibu Usafirishaji Haramu wa Binadamu, hasa Wanawake na Watoto , ndicho chombo kikuu cha kisheria cha kimataifa cha kupambana na uhalifu.

Wataalamu wa UNODC wanaunga mkono uundaji wa sheria na sera za kitaifa kuhusu biashara haramu ya binadamu na kutoa mafunzo kwa maafisa wa umma, wakiwemo maafisa wa polisi, walinzi wa udhibiti wa mpaka, wakaguzi wa kazi na wataalam wa kusaidia wahasiriwa.

Kwa mwongozo uliotolewa na UNODC, nchi zimetayarishwa vyema kuchunguza na kushtaki kesi za usafirishaji haramu wa binadamu, kufuta mitandao ya uhalifu inayofanya uhalifu huu, kufuatilia mapato haramu na kulinda na kusaidia waathiriwa.