Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haiti: Misheni ya kimataifa na hitaji lisiloweza kubadilika la kurejesha hali ya usalama

Wahaiti wapatao 200,000, hasa katika Port-au-Prince (pichani) wamelazimika kukimbilia maeneo ya muda  kwa sababu ya ukosefu wa usalama..
Giles Clarke
Wahaiti wapatao 200,000, hasa katika Port-au-Prince (pichani) wamelazimika kukimbilia maeneo ya muda kwa sababu ya ukosefu wa usalama..

Haiti: Misheni ya kimataifa na hitaji lisiloweza kubadilika la kurejesha hali ya usalama

Amani na Usalama

Kuanzishwa kwa ujumbe wa kimataifa wa usaidizi wa usalama kwa nchi ya Haiti kunasonga mbele huku taifa hilo la Karibea likiendelea kukabiliwa na mzozo wa ghasia na ukosefu wa usalama unaosababishwa na shughuli za magenge ya uhalifu.

Ripoti za vyombo vya habari zinaonesha kuwa miundombinu ya misheni hiyo inawekwa tayari wakati ambapo vifaa vinawasili kwa njia ya ndege katika mji mkuu, Port-au-Prince.

Hapa ndio unahitaji kujua kuhusu kile kinachofuata:

Kwa nini ujumbe wa Kimataifa wa usalama ni muhimu?

Haiti imekumbwa na ghasia ambazo zimekuwa zikimepanda kwa viwango visicho na kifani. Katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 22 Aprili, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Maifa kwa taifa la Haiti, Maria Isabel Salvador alisema "haiwezekani kupindua ongezeko la shughuli za magenge katika Port-au-Prince na kwingineko, kuzorota kwa hali ya haki za binadamu na kuongezeka kwa mzozo wa kibinadamu," akiongeza kuwa "mara kwa mara ametoa tahadhari kwa hitaji lisiloweza kuepukika la kurejesha hali ya usalama".

Mnamo mwezi Machi 2024, magenge yalianzisha mashambulizi yaliyoratibiwa kulenga miundombinu muhimu ya serikali, ikiwa ni pamoja na vituo vingi vya polisi na magereza mawili makuu huko Port-au-Prince pamoja na maeneo ya shule na afya pamoja na maeneo ya kidini.

"Mashambulizi haya," alisema Bi. Salvador, "yamezidi kudhoofisha taasisi za serikali na kuimarisha changamoto ambazo tayari ziko katika uanzishaji upya wa utawala wa sheria."

Katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka, Umoja wa Mataifa ulisema watu 2,500, ikiwa ni pamoja na angalau watoto 82, waliuawa au kujeruhiwa kutokana na vurugu za magenge.

Takriban nusu ya waathiriika walipigwa risasi wakati wa mashambulizi makali dhidi ya vitongoji vyao au mapigano kati ya magenge na polisi.

Takriban watu 438 walitekwa nyara kwa ajili ya fidia katika kipindi hicho.

Umoja wa Mataifa ulisema kuwa takriban watu 362,000 - nusu yao wakiwa ni watoto - wamelazimika kukimbia makazi yao kwa sababu ni hatari sana kubaki.

Unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana unaongezeka, na makumi ya maelfu ya watoto hawawezi kuhudhuria shule kwa sababu ya ukosefu wa usalama.

Watu waandamana katika mitaa ya Port-au-Prince katika Haiti iliyokumbwa na mzozo.
© UNICEF/Roger LeMoyne and U.S. CDC
Watu waandamana katika mitaa ya Port-au-Prince katika Haiti iliyokumbwa na mzozo.

Nani anaunga mkono msaada wa usalama?

Polisi wa Kitaifa wa Haiti (HNP) hawawezi kudhibiti kikamilifu kuzuka kwa vurugu, na jeshi la Haiti ni ndogo na lina vifaa vya kawaida tu.

Takriban kila mtu anakubali kwamba msaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa unahitajika kusaidia HNP katika juhudi zake za kuleta utulivu wa hali na kuwawezesha Wahaiti kuendelea na maisha yao ya kila siku bila hofu ya kuangukiwa na ghasia za magenge.

Hadi kufikia Oktoba 2022, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alijibu ombi la Waziri Mkuu wa zamani wa Haiti Ariel Henry, akiyataka mataifa kujitokeza kusaidia.

Nchi za Bahamas, Bangladesh, Barbados, Belize, Benin, Chad, Jamaica na Kenya zimemjulisha rasmi Katibu Mkuu kuhusu nia yao ya kuchangia wafanyakazi katika misheni hiyo ya usaidizi.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa alithibitisha kuwa nchi nyingine zimeonesha nia ya kuunga mkono ujumbe huo, lakini Umoja wa Mataifa bado haujapokea taarifa rasmi kuhusu hilo.

Jamii za Port-au-Prince zimeweka vizuizi vya magari yaliyotelekezwa ili kupunguza hatari ya utekaji nyara na mashambulizi ya magenge.
© UNOCHA/Giles Clark
Jamii za Port-au-Prince zimeweka vizuizi vya magari yaliyotelekezwa ili kupunguza hatari ya utekaji nyara na mashambulizi ya magenge.

Kwa nini imechukua muda mrefu kuanzisha misheni hii?

Jambo kuu la kushikilia hapo awali lilikuwa ni nchi gani ingejitokeza kuongoza misheni ambayo inaweza kuwa ngumu na hatari.

Ripoti za vyombo vya habari zinaonesha kuwa magenge yana udhibiti wa juu ya karibu asilimia 80 ya mji mkuu. Makubaliano yaliyoripotiwa hivi karibuni kati ya magenge, ya kuunda umoja dhidi ya misheni hiyo yamesababisha picha kuwa ngumu zaidi.

Kenya itaongoza misheni hiyo. Maafisa wa Kenya walitembelea Haiti kufanya mazungumzo na viongozi wa Haiti na wa kanda, miongoni mwa wengine, kuhusu mamlaka na upeo wake nchini Haiti.

Rais wa Kenya, William Ruto, aliliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Septemba 2023 kwamba Wahaiti "wanateseka sana kutokana na urithi wa utumwa, ukoloni, hujuma na kutelekezwa", na kuongeza kuwa kukabiliana na hali hiyo ni "jaribio la mwisho la mshikamano wa kimataifa." na hatua za pamoja”.

Polisi wa Kitaifa wa Haiti wanahitaji kuimarishwa ili kuweza kukabiliana na changamoto kubwa zinazowakabili, kulingana na UN.
UNDP/Borja Lopetegui Gonzalez
Polisi wa Kitaifa wa Haiti wanahitaji kuimarishwa ili kuweza kukabiliana na changamoto kubwa zinazowakabili, kulingana na UN.

Itakuwa operesheni ya aina gani?

Ni muhimu kutambua kwamba ujumbe wa usalama hautakuwa operesheni ya Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo, Baraza la Usalama liliidhinisha ujumbe huo na kumtaka Katibu Mkuu kuanzisha wakfu wa kupitisha michango ya hiari katika operesheni hiyo.

Mwishoni mwa mwezi Aprili, Msemaji wa Umoja wa Mataifa alithibitisha kuwa dola milioni 18 ziliwekwa kwenye mfuko huo na Canada, Ufaransa na Marekani.

Wakazi wa Cité Soleil nchini Haiti wakiwa kwenye foleni ya kupokea misaada ya Umoja wa Mataifa.
WFP/Theresa Piorr
Wakazi wa Cité Soleil nchini Haiti wakiwa kwenye foleni ya kupokea misaada ya Umoja wa Mataifa.

Nini kinafuata na upi ni ushiriki wa UN?

Katika kuunga mkono ujumbe huo, Baraza la Usalama lilifanya kazi chini ya Sura ya VII ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambayo, pamoja na mambo mengine, inaidhinisha matumizi ya nguvu baada ya hatua nyingine zote za kudumisha amani na usalama wa kimataifa kuwa zimetumika.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa unaendelea kuunga mkono Haiti katika nyanja nyingi. Ujumbe wa kisiasa unaojulikana kwa kifupi cha Kifaransa, BINUH, na unaongozwa na Bi Salvador, unaendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha utulivu wa kisiasa na utawala bora, ikiwa ni pamoja na utawala wa sheria.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanatoa misaada ya kibinadamu kwa Wahaiti walioathiriwa na ghasia na ukosefu wa usalama, lakini pia na majanga ya asili kama vile tetemeko la ardhi la Agosti 2021. Shirika la Umoja wa Mataifa la Huduma ya Ndege ya Kibinadamu (UNHAS) kwa sasa linasafirisha wafanyakazi wa misaada, vifaa muhimu na misaada ya kuokoa maisha ndani na kote Haiti. Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa pia unaendelea kuunga mkono mamlaka katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.