Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa FAO ulivyosaidia wafugaji nyuki na wazalishaji wa asali nchini Rwanda

Patrick Uwingabire, mfugaji nyuki nchini Rwanda.
©FAO/Olivier Mugwiza
Patrick Uwingabire, mfugaji nyuki nchini Rwanda.

Mradi wa FAO ulivyosaidia wafugaji nyuki na wazalishaji wa asali nchini Rwanda

Tabianchi na mazingira

Patrick Uwingabire alianza kujifunza kuhusu ufugaji nyuki alipokuwa na umri wa miaka kumi na moja tu. Katika kijiji chao huko Huye, katika Mkoa wa Kusini wa Rwanda, mjomba na babu yake walimfundisha yote waliyojua kuhusu kutengeneza mizinga ya nyuki na kutunza viumbe hao muhimu.

Ufugaji nyuki ulimpa njia ya kusonga mbele wakati familia yake haikuweza kumlipia karo yake ya shule. “Ilikuwa haiwezekani kwangu kwenda shule. Hilo halikuwezekana. Kwa hiyo, nyuki na asali vikawa nguzo za maisha yangu,” anasema mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 39.

Siku hizi, Patrick anaongoza chama cha ushirika cha wafugaji nyuki 15 huko Huye, kiitwacho Koperative Abavumvu b' Umwuga ba Huye (KOPAHU), ambacho kinanufaika na mradi unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) unaolenga kuifanya sekta ya ufugaji nyuki ya Rwanda kuwa ya kisasa.

Sehemu muhimu ya mradi inahusisha kubadilisha mizinga ya nyuki ya kawaida na miundo 35 ya kisasa, ya umbo la mstatili. Mizinga hii ya kisasa hurahisisha ukaguzi na urinaji wa asali, hivyo kuongeza uzalishaji wa asali na mapato ya wafugaji nyuki.

Patrick na wafugaji nyuki wenzake pia walipata ujuzi mpya katika utunzaji wa mizinga ya nyuki, kudhibiti magonjwa ya nyuki na wadudu, masoko ya mazao yao na kuhakikisha ubora na ufuatiliaji  wa asali kutoka kwenye mzinga hadi kwa mteja.

"Kabla ya mafunzo ya FAO, hatukujua jinsi ya kutunza nyuki," Patrick anasema. "Nilikuwa nikirina kilo 800-900 za asali kwa mwaka, lakini leo naweza kurina zaidi ya tani mbili."

Shirika hilo pia lilipata mashine kadhaa za kuchuja asali, ambazo wanachama wake, (kama vile wafugaji nyuki 120,000 wa Rwanda), hawakuwa wametumia hapo awali. FAO inashughulikia kikamilifu pengo hili kwa kutoa mafunzo ya mbinu na vifaa vya kisasa, ikiwa tayari imetoa mafunzo kwa wafugaji nyuki 9,000 wa Rwanda.

“Tulivutiwa na ufanisi wa teknolojia hiyo mpya,” na kutokana na ongezeko la uzalishaji, Patrick anasema, “niliweza kujenga nyumba kwenye sehemu ya shamba nililonunua kutokana na mapato ya asali. Ninahudumia familia yangu, na ninaweza kulipia ada ya shule ya watoto wangu.”

Sehemu muhimu ya mradi wa FAO nchini Rwanda ilihusisha kubadilisha mizinga ya nyuki ya kawaida na mizinga ya kisasa ya mstatili ambayo hurahisisha uvunaji wa asali, kuongeza uzalishaji wa asali na mapato ya wafugaji nyuki maradufu au mara tatu.
©FAO/Olivier Mugwiza
Sehemu muhimu ya mradi wa FAO nchini Rwanda ilihusisha kubadilisha mizinga ya nyuki ya kawaida na mizinga ya kisasa ya mstatili ambayo hurahisisha uvunaji wa asali, kuongeza uzalishaji wa asali na mapato ya wafugaji nyuki maradufu au mara tatu.

Sehemu muhimu ya mradi wa FAO nchini Rwanda ilihusisha kubadilisha mizinga ya nyuki ya kawaida na mizinga ya kisasa ya umbo la mstatili ambayo hurahisisha urinaji wa asali, kuongeza uzalishaji wa asali na mapato ya wafugaji nyuki maradufu au mara tatu. ©FAO/Olivier Mugwiza

Rwanda inashiriki kikamilifu katika mpango wa FAO wa Bidhaa Moja ya Kipaumbele Nchi Moja (OCOP) na asali ndiyo iliyoteuliwa kama bidhaa ya kipaumbele.

Mpango huu unafanya kazi ili kuimarisha mchakato mzima wa thamani ya bidhaa iliyopewa kipaumbele na taifa. Katika mpango huu, FAO inatoa usaidizi katika kuboresha uzalishaji na mbinu za usindikaji wa asali na kuongeza manufaa kwa wakulima na wengine katika msururu wa usambazaji.

Kama sehemu ya OCOP, FAO inatetea mazoea endelevu ya mazingira yanayolenga kupunguza utegemezi wa kemikali hatari na kukuza mfumo wa ikolojia uliooanishwa. Wakati huo huo, mipango ya uhamasishaji wa jamii inahimiza wale wanaoishi karibu na nyuki kufahamu umuhimu wa nyuki na uchavushaji na kuwazuia watu kuwaangamiza kama wadudu waharibifu.

Tangu mpango wa FAO wa OCOP uanze Septemba 2021, zaidi ya nchi 85 duniani zimejitolea kutangaza bidhaa 54 za kilimo.

Mbali na Rwanda, nchi za Viet Nam, Benin na Chile pia zilichagua asali kuwa bidhaa zao za kipaumbele, huku FAO ikitoa mafunzo sawa na miradi ya usaidizi ili kuimarisha sekta zao za ufugaji nyuki, kuruhusu wazalishaji kukuza asali na bidhaa za asali katika masoko ya kikanda na kimataifa.