Majengo marefu ya vioo , kaburi la ndege wanaohamahama
Majengo marefu ya vioo , kaburi la ndege wanaohamahama
Jumamosi ya tarehe nane mwezi Mei 2021 dunia imeadhimisha siku ya kimataifa ya ndege wanaohama ikiwa ni njia mojawapo ya kutambua faida zao katika maisha ya binadamu na sayari dunia. Maudhui ya mwaka huu ni Imba, paa, Ruka Zaidi Angani kama ndege.
Kukujengea uelewa mpana wa ndege wanaohamahama Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, UN News Kiswahili, amezungumza na mtaalamu wa ndege hao David Maige kutoka Hifadhi za taifa Tanzania- TANAPA.
Bwana Maige anaanza kwa kueleza, "ndege wahamao huonekana katika Tanzania katika miezi ya Septemba na April, mwezi wa Tisa ndio wanaanza kuingia Tanzania na mwezi April ndio wanaanza kurudi kwa ajili ya kwenda kuzaana katika nchi wanazotoka. Na wanapotoka ni katika bara la Ulaya na Asia kaskazini, kwa wale wanaotoka ulaya tunawaita Paliatic Migrants na pamoja na wale wanaotoka bara la Asia kaskazini . Lakini kuna ndege wanaohama ndani ya bara la Afrika wao tunawaita Afrotropical migrants au intra Africa Migrants."
Ndege husafiri bila pasi ya kusafiria
Ndege hawa kweli ni wa ulimwengu mzima na huzunguka vile watakavyo bila pasi ya kusafiria wala kibali cha kuingia nchi nyingine, hali ya hewa ikibadilika tuu nao huanza safari kutoka bara moja kwenda jingine ambapo mtaalamu huyo wa TANAPA anasema, "wanapohama ndege wanaotoka katika bara la ulaya hupitia Gibraltar katika nchi ya Hispania huingia Afrika kaskazini na hutawanyika kuelekea magharibi mwa Afrika na katikati ya Afrika. Wanaopita Katikati ya Afrika hupitia bonde la mto Nile na wale wengine wanaokuja wengine Afrika hupitia Magharibi mwa Afrika kandokando ya bahari ya Atlantiki."
Akizungumzia wale watokao Asia kaskazini amesema, " wao hupitia Bosphoras na Misinga katika bara la Uarabuni. Wanapovuka tuu huingia katika mkondo wa bonde la ufa na milima iliyopo kando kando ya bonde la ufa hapa Tanzania. Na wale wanaotokea Gibraltar wengine hupita katika ziwa Victoria ambapo ndipo maenoe mengine ambapo wanapata chakula na kuendelea na safari yao kwenda kusini mwa bara la Afrika."
Lakini ni wapi mtu anaweza kuwaona ndege hawa wanaohamahama? Bwana Maige anasema, "Maeneo ambayo wanaonekana kwa urahisi sana ni katika maeneo yaliyohifadhiwa , kama hifadhi za taifa Tanzania na maeno ya mapori ya akiba, pori tengefu, maziwa , ufukweni mwa bahari na katika visiwa mbalimbali katika nchi ya Tanzania. Lakini wengine huonekana katika mito mikubwa na hata mito midogo na wengine huonekana katika mbuga wazi ambazo sio hifadhi
Ndege hawa wana faida!! " Faida ya utalii, kwakweli watalii wengi huja Tanzania kwa ajili ya kuangalia ndege hawa wanaohama na pamoja na ndege wenyeji. Lakini pia ndege hawa huwaleta pamoja watafiti mbalimbali kwa pamoja, kwa maana ya watafiti wengine kutoka mabara mengine ya ulaya, amerika na maeneo mengine wakati mwengine hukutanikia hapa kwa ajili ya kujadili masuala yanayohusu ndege na hasa ndege wanaohama."
Faida nyingine ya ndege hawa husaidia sana kukutanisha watu kutoka mataifa mbalimbali. Ndege pia wana faida katika jamii zetu katika mikoa mingine huko huwa wanaamini kuwa ndege wanaotoka Ulaya na Asia kaskazini wanapoonekana kama korongo Ulaya pamoja na korongo Abdini, hasa katika mashamba makubwa wanaashiria vipindi vya mvua ya vuli vimekaribia, " na nikweli kabisa mvua hunyesha baada ya hao ndege kuonekana.Lakini pia katika mikoa ya Kagera na Geita wanaamini kuwa ndege hawa wameleta sebebe kwa sababu ndiko wakati wa neema ya senene."
Ndege wanaohama huua wadudu waharibifu
"Ndege hawa pia hula ndege waharibifu kama viwavi ambavyo vinaharibu mazao mbalimbali lakini hula viumbe mbalimbali , kwa wale wanaokula nyama hula panya ambao ni waharibifu katika maeneo yetu ya mazao na majumbani mwetu .Lakini pia ndege hawa husaidia kuchavusha maua ya mimeo mbalimbali , mimea ya maporini na mazao ya mashambani," amesema mtaalamu Maige.
Janga la Covid19 halijakuwa na athari kwa binadamu tu hata ndege hao wameathirika akisema, "shughuli nyingi zinazohusiana na utafiti wa ndege, mikutano mbalimbali na utalii ziliathirika kabisa, kwa sababu ya covid19 kwa hofu ya watu kuambukizwa covid 19"
Shughuli za binadamu nazo zinakuwa kikwazo kwa ndege hawa ambapo "changamoto zinazowapata ndege hao ni uharibifu wa makazi yao, kuhadimika kwa chakula kutokana na uharibifu wa mazingira lakini pia ujenzi wa nyumba ndefu ambapo zimetengenezwa kwa vioo kwahiyo ndege hujigonga kwasababu kama vile wanaona ni njia yakupita lakini pia ndege hawa wanapata matatizo mbalimbali ya kujigonga katika minara ambayo inajengwa ambayo ni ndefu kwelikweli. "
Elizabeth Mrema ni Katibu Mtendaji wa sekretarieti ya mkataba wa kimataifa wa kulinda bayonuai, yeye anaeleza namna ndege wanaohama wanaweza kuleta furaha husasani katika kipindi hiki cha janga la Covid19.
"Ndege hawa tukiamka asubuhi unasikia sauti zao nyororo, tunawapenda kwasababu ya rangi zao lakini pia wana manufaa makubwa katika binadamu hasa katika wakati huu wa covid19, ukisikiliza sauti tuu zile sauti zao zinaondoa ujogofu wote tulionao unasaabishwa na madhara mbalimbali."
Ndege wana manufaa makubwa hasa ukiangalia kile chakula tunachokula kwasababu wao ndio wanaotengeneza mazingira pia ya ulimwengu, wanadhibiti wadudu, huchangua mimea, hueneza mbegu, hubadilisha mandhari na kuchangia michakato pamoja na uundaji wa mchanga wa baianoai.
"Kwa hiyo tunawahitaji hawa ndege wanania njema sana kwetu sisi na hatunabudi kuendeleza kuwalinda na wawe na ustawi wa dunia hii dunia ambayo tunashirikiana kwa pamoja sisi binadamu na ndege tunatumia dunia hii hii moja," ametamatisha Bi. Mrema.