Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatoa mwongozo mpya kupunguza maambukizi kwenye matumizi ya katheta

Muhudumu wa afya akimuhudumia mgonjwa katika kituo cha matibabu ya kipindupindu Malawi
© UNICEF
Muhudumu wa afya akimuhudumia mgonjwa katika kituo cha matibabu ya kipindupindu Malawi

WHO yatoa mwongozo mpya kupunguza maambukizi kwenye matumizi ya katheta

Afya

Je wajua kuwa matumizi yasiyo sahihi ya katheta hospitalini yanaweza kusababisha kifo cha mgonjwa? Pengine wajiuliza katheta ni nini? Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, linafafanua kuwa katheta ni neli au bomba dogo linaloingizwa kwenye mshipa mdogo wa damu wakati wa tiba au uchunguzi wa mgonjwa.

WHO sasa kwa kutambua hilo limetoa mwongozo mpya hii leo ikiwemo mafunzo ya matumizi ya neli na usafi wa mikono ili kuepusha uwepo wa damu au maambukizi mengine yanayosababishwa na matumizi ya kifaa hicho kwa mgonjwa.

Maambukizi hutokea vipi?

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema kuingizwa au kutolewa vibaya kwa neli hiyo mwilini au kutoitunza vema kunaweza kusababisha vijiumbe maradhi kuingia moja kwa moja kwenye damu na hivyo mgonjwa kupata maambukizi kwenye damu au magonjwa ya figo na ubongo ambayo ni changamoto kuyatibu.

“Hadi asilimia 70 ya wagonjwa huhitaji matumizi ya neli aina ya PIVC kuingizwa kwenye mishipa ya vena au ateri na wakati mwingine wakiwa wamelazwa hospitalini,” imesema WHO.

Wagonjwa wanaotumia kifaa hicho mara nyingi wanakuwa wako taabani au wana kiwango kidogo cha king ana hivyo hatarini kupata maambukizi.

Kiwango cha vifo kutokana na matumizi  yasiyo sahihi ya katheta

WHO inakadiria kuwa kati ya mwaka 2000 na 2018, wastani wa vifo vitokanavyo na huduma ya afya ihusianayo na maambukizi yad amu ilikuwa asilimia 24.4 na iliongezeka hadi asilimia 52.3 miongoni mwa wagonjwa waliokuwa wanapatiwa matibabu kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi.

“Maambukizi yanayohusiana na utoaji wa huduma za afya ni janga kubwa linaloweza kuzuilika na linatishia ubora na usalama wa huduma za afya,” amesema Dkt. Bruce Aylward, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa WHO akihusika na Huduma ya Afya kwa Wote.

 “Kutekeleza mapendekezo ya huduma safi na kuzuia maambukizi ni muhimu ili kuokoa maisha na kuondokana na machungu wapatayo watu wengi duniani kote, machungu yanayoweza kuepukika.” Amesema.

Mapendekezo ni yapi?

Mwongozo huo mpya unajumuisha kanuni bora 14 na mapendekezo 23 kwenye maeneo muhimu ya wahudumu wa afya ikiwemo:

Mosi, elimu na mafunzo; pili mbinu za kuepusha maambukizi kwenye damu na kanuni bora za usafi wa mikono; tatu uingizaji, utunzaji, upatikanaji na uondoaji wa katheta; na nne, uchaguaji wa katheta inayofaa kwa mgonjwa.

WHO imesema kwa upande wake itaendelea kushirikiana na serikali kuandaa na kutekeleza kanuni bora za kupunguza matukio ya maambukizi kwenye damu na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma salama na ya uhakika.

Soma mapendekezo yote hapa.