COVID-19 yaongeza mahitaji ya Oksijeni, WHO na wadau wachukua hatua

Pichani, Antonina mwenye umri wa miaka 58, akihaha kupumua huku homa ikiwa juu wakati alipogundua kuwa ana COVID-19. Mitungi ya oksijeni iliyosambazwa na UNICEF Ukraine iliokoa maisha yake.
UNICEF
Pichani, Antonina mwenye umri wa miaka 58, akihaha kupumua huku homa ikiwa juu wakati alipogundua kuwa ana COVID-19. Mitungi ya oksijeni iliyosambazwa na UNICEF Ukraine iliokoa maisha yake.

COVID-19 yaongeza mahitaji ya Oksijeni, WHO na wadau wachukua hatua

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO na wadau wake leo wamezindua kikosi kazi cha kuhakikisha nchi za kipato cha chini na cha kati, LMICs zinapata mitungi ya hewa ya Oksijeni ambayo mahitaji yake yameongezeka hivi sasa kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Taarifa ya pamoja ya WHO na wadau hao wakiwemo kampuni ya Wellcome , mpango wa nchi za G-20 wa kufanikisha chanjo dhidi ya Corona ACT Accelerator na UNITAID iliyotolewa leo Geneva, Uswisi inasema hatua hiyo imezingatia kuwa "zaidi ya wagonjwa 500,000 wa COVID-19 katika nchi hizo wanakadiriwa kuhitaji hewa ya Oksijeni kila siku. Tathmini yaonesha kuwa dola milioni 90 zahitajika haraka kufanikisha upatikanaji wa hewa hiyo kwa nchi 20 za kipato cha chin ina kati.

Kwa mantiki hiyo wadau hao watashirikiana kupima mahitaji na kushirikiana na wahisani wa fedha na kupata mitungi hiyo ya gesi na ushauri wa kiufundi kusaidia nchi zilizoathirika zaidi.

Wadau hao wanasema kuwa COVID-19 imeongeza shinikizo katika mifumo ya afya ambapo hospitali nyingi katika nchi za kipato cha chini na kati zimeishiwa oksijeni, na hivyo wagonjwa kufariki dunia kufariki dunia kwa magonjwa yanayozuilika huku familia za wagonjwa zikigharimika kupita kiasi kulipia mitungi ya gesi.

"Oksijeni ni tiba muhimu, na licha ya kuwa ni tiba muhimu kwa wagonjwa waliolazwa kwa sababu ya COVID-19, bado upatikanaji wake katika nchi za kipato cha chini na kati ni mdogo kutokana na gharama kuwa juu. Hospitali hazina uwezo wa kupata mitungi ya kutosha kutokana na gharama kubwa na hivyo matokeo yake ni vifo vya wagonjwa ambavyo vingalizuilika," imesema taarifa hiyo.

Mtungi wa oksijeni unaotumika hospitalini kwa ajli ya wagonjwa.
Samuel Ramos on Unsplash
Mtungi wa oksijeni unaotumika hospitalini kwa ajli ya wagonjwa.

Mahitaji ya Oksijeni kwa siku

Taarifa hiyo inakadiria kuwa watu 500,000 wanahitaji mitungi milioni 1.1 ya oksijeni kila siku ambapo nchi 25 zinaripoti ongezeko la mahitaji, hususan barani Afrika. Upatikanaji huo ulikuwa bado ni changamoto hata kabla ya COVID-19 na mahitaji yameongezeka zaidi wakati huu wa janga la Corona.

Dkt. Philippe Duneton, Mkurugenzi Mtendaji wa UNITAID amesema, "dhahura hii ya dunia inahitaji hakika hatua za kidunia au kimataifa kutoka mashirika ya kimataifa na wahisani. Nchi nyingie zimeshuhudia ongezeko la mahitaji hata kabla ya janga ili kukidhi mahitaij yao. HIvi sasa ni muhimu kuliko wakati wote tushirikiane kuendeleza kile ambacho kimeshafanyika na kuazimia kusaidia nchi zenye uhitaji zaidi haraka iwezekanavyo."

Kikosi kazi hicho kimebaini uhitaji wa dola milioni 90 kushughulikia upatikanaji wa hewa ya Oksijeni kwa nchi 20 ikiweo Malawi, Nigeria na Afghanistan. Hizo ni nchi za awali ambazo zimebainika kuwa na uhitaji wa haraka kufuatia tathmini ya mradi wa dharura waWHO.

Unitaid na Wellcome watatoa mchango wa haraka wa dola milioni 20 katika dharura hiyo huku tathmini zaidi ikiendelea kwa nchi nyingine.

Mkurugenzi Mtendaji wa Programu ya dharura WHO Dkt. Mike Ryan, amesema "oksijeni inaokoa maisha na ni muhimu kuharakisha suluhu za kumpatia ahueni mgonjwa ili kuboresha matokeo ya kitabibu."

Kwa mujibu wa WHO, hata kabla ya COVID-19, ugonjwa wa vichomi au numonia ulikuwa ni ugonjwa wa maambukizi unaoongoza kwa vifo miongoni mwa watu wazima na watoto, ukiua watu milioni 2.5 mwaka 2019. Ujio wa COVID-19 umeongeza tatizo hilo la kupumua hasa kwa nchi ambazo zinakabiliwa na janga la Corona na Numonia.