Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria ya ukimbizi ya Uingereza-Rwanda: Viongozi wa UN waonya juu ya madhara yake

Moja ya mitaa ya mji mkuu wa Rwanda, Kigali
UN/Rick Bajornas
Moja ya mitaa ya mji mkuu wa Rwanda, Kigali

Sheria ya ukimbizi ya Uingereza-Rwanda: Viongozi wa UN waonya juu ya madhara yake

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Turk na Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Filippo Grandi hii leo wametoa wito kwa serikali ya Uingereza kufikiria upya mpango wake wa kuwahamishia nchini Rwanda wasaka hifadhi wanaofikia nchini humo.

 

Badala ya kufanya hivyo viongozi hao waandamizi wa UN wameishauri Uingereza kuchukua hatua zote za kivitendo kushughulikia suala la wahamiaji kukimbilia nchini Uingereza kwa kuzingatia ushirikiano wa kimataifa na kuheshimu sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Mswada wa usalama wa Rwanda unatarajiwa kuwasilishwa katika bunge la Uingereza pamoja na mkataba wa ushirikiano wa ukimbizi baina ya Uingereza na Rwanda baada ya hapo mwaka jana mahakama kuu nchini Uingereza kueleza kuwa mapendekezo ya kuwahamisha wasaka hifadhi yatakiuka sheria za kimataifa na za Uingereza. 

Kamishna wa haki za binadamu Bwana Garandi amesema sheria hii mpya itaenda mbali kabisa na utamaduni wa muda mrefu wa Uingereza kutoa kimbilio kwa wakimbizi “Kulinda wakimbizi kunahitaji nchi zote - sio tu zile maeneo jirani ya mgogoro - kutekeleza wajibu wao. Mpangilio huu unalenga kuhamisha jukumu la ulinzi wa wakimbizi, kudhoofisha ushirikiano wa kimataifa na kuweka mfano wa kimataifa unaotia wasiwasi.”

Ameeleza kuwa Uingereza ina historia nzuri ya kujivunia ya kufanya uchunguzi mzuri na huru wa mahakama na kwamba bado inaweza kuchukua hatua zinazofaa na kuweka hatua za kusaidia kushughulikia mambo yanayowasukuma watu kukimbia katika nchi zao na kushirikiana katika kusaka majawabu kwa wenye uhitaji wa ulinzi, na washirika wa Ulaya na wengine wa kimataifa.

Viongozi hao pia wameeleza wasiwasi wao mkubwa kuwa miongoni mwa changamoto za kuwahamishia wakimbizi nchini Rwanda kutoka Uingereza ni kwamba sheria hiyo inazingatia tu hali zao binafsi au hatari zozote za ulinzi. Wametoa wito kwa uingereza kufuata hatua za kivitendo na kupanua njia salama na za kawaida za ulinzi. 

“Kwa kubadilisha uwajibikaji kwa wakimbizi, kupunguza uwezo wa mahakama za Uingereza kuchunguza maamuzi ya kuondolewa, kuzuia upatikanaji wa masuluhisho ya kisheria nchini Uingereza na kupunguza wigo wa ulinzi wa haki za binadamu wa ndani na kimataifa kwa kundi maalum la watu, sheria hii mpya inazuia sana utawala wa sheria nchini Uingereza na unaweka mfano wa hatari duniani kote,” alisema Bwana Türk.

Watapelekwa Rwanda bila matarajio ya kurejea Uingereza

Sheria hiyo mpya ni ya tatu katika msururu wa sheria za Uingereza zinazoendelea kuweka vikwazo ambazo zimepunguza ufikiaji wa ulinzi wa wakimbizi nchini Uingereza tangu mwaka 2022, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku upatikanaji wa hifadhi au aina nyingine za ruhusa ya kukaa nchini Uingereza kwa wale wanaofika kinyume cha sheria kupitia nchi ya tatu. 

Iwapo itatekelezwa, itafungua njia kwa wanaotafuta hifadhi, ikiwa ni pamoja na familia zenye watoto, kupelekwa nchini Rwanda, kuwasilisha maombi yao ya kusaka hifadhi, bila matarajio ya kurejea nchini Uingereza. 

Pia itapunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wa wanaotafuta hifadhi kupinga au kukata rufaa kwa maamuzi ya kuondolewa, huku watoa maamuzi na majaji wakitakiwa kuichukulia Rwanda kama nchi "salama" katika suala la kuwalinda wanaotafuta hifadhi - bila kujali ushahidi wowote kinyume chake, sasa au katika siku zijazo. 

Taarifa ya viongozi hao waandamizi wa Umoja wa Mataifa imesema hali hii inatia mashaka zaidi kwani sheria inaidhinisha waziwazi Serikali kupuuza masuluhisho yoyote ya muda ya ulinzi kutoka kwa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.