Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tathmni yaanza Gaza, misaada kuanza kusambazwa tena leo usiku

WAtoto wakijaza maji ya kunywa kwenye madumu huko kitongoji cha Al-Shaboura, eneo la Rafah, kusini mwa Gaza
UN News/Ziad Taleb
WAtoto wakijaza maji ya kunywa kwenye madumu huko kitongoji cha Al-Shaboura, eneo la Rafah, kusini mwa Gaza

Tathmni yaanza Gaza, misaada kuanza kusambazwa tena leo usiku

Msaada wa Kibinadamu

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wameanza ziara ya tathmini huko Gaza na mashirika yao yataanza tena usambazaji wa misaada baadaye Alhamisi usiku baada ya sitisho la saa 48 kufuatia kitendo cha Israel kuua watumishi 7 wa kiutu kutoka shirika la World Central Kitchen kwenye eneo lililozingirwa la Gaza.

“Hali ukanda wa Gaza inatisha,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, Dkt. Tedros Ghebyresus.  “Kwa mara nyingine tena, WHO inataka sitisho la mapigano, mateka wote waachiliwe huru bila masharti na kuweko na amani ya kudumu.”

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric naye akizungumza na waandishi leo Alhamisi amesema kwamba kutokana na kile kilichotokea kwa World Central Kitchen “tulilazimika kusitisha usambazaji misaada na kujipanga upya na kufanya upya tathmini,” akiongeza kuwa msafara utaanza leo usiku “tuna matumaini msafara utafika kaskazini.”

Maafisa wa juu wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakionya hatari ya baa la njaa kaskazini mwa Gaza wakati huu ambapo Israel inaendelea kuzuia na kuchelewesha kuingia kwa misaada hasa kaskazini mwa Gaza.

Hadi leo hii, jeshi la Israel limeua zaidi ya watu 30,000 huko Gaza, kwa mujibu wa mamlaka za afya Gaza, kufuatia tukio la Hamas kushambulia Israel tarehe 7 Oktoba mwaka 2023 na kusababisha vifo vya watu 1,200 na wengine 240 kutekwa nyara.

Msemaji wa UN ameeleza kuwa timu za WHO zimefika hospitali mbili Gaza na kufanya tathmini pamoja na kuzipatia misaada ya vifaa vya kuokoa maisha.

Timu hizo zimeripoti kuweko kwa hali mbaya kwenye hospitali hasa ya Al- Shifa ambayo kwa wiki mbili imekuwa imezingira na jeshi la Israel.

Bwana Dujarric amesema kuwa timu hiyo iliweza kuzungumza pia na wagonjwa walioweza kuondoka hospitalini hapo ambapo mmoja wao amesesma “madaktari wameamua kutuwekea chumvi na siki kwenye vidonda kutokana na ukosefu wa dawa za kuzuia maambukizi.”