Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upokonyaji silaha na kutozieneza sio tu muhimu kwa amani bali pia kwa uwepo wetu: Guterres

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akiwa na bunduki au silaha zilizokusanywa kutoka kwa wanamgambo nchini Côte d'Ivoire.
UN Photo/Ky Chung
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akiwa na bunduki au silaha zilizokusanywa kutoka kwa wanamgambo nchini Côte d'Ivoire.

Upokonyaji silaha na kutozieneza sio tu muhimu kwa amani bali pia kwa uwepo wetu: Guterres

Amani na Usalama

Katika maadhimisho ya pili ya Siku ya kimataifa ya upokonyaji silaha na uelimishaji wa kutozizalisha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema yamekuja katika wakati hatari, unaoashiria kuongezeka kwa viwango vya matumizi ya kijeshi, kuongezeka kwa mivutano ya kisiasa ya kijiografia na kuongezeka kwa migogoro ya ghasia kote ulimwenguni.

Katika ujumbe wake wa siku hii Antonio Guterres amesema “Wakati huo huo, baadhi ya viongozi wanatumia maneno ya imani za mwisho wa dunia kutoepukika juu ya matumizi ya silaha za nyuklia.”

Pia amesema kuna ongezeko la silaha haramu ndogo ndogo na silaha nyepesi, matumizi ya vifaa vya milipuko katika maeneo yenye watu wengi, na kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia mpya za kijeshi na zinazoibukia, ikiwa ni pamoja na akili mnemba au bandia, hali ambayo inazusha wasiwasi mkubwa.

Umuhimu wa upokonyaji silaha na kutozizalisha

Katibu Mkuu amesema siku hii “inatukumbusha kuwa kupokonya silaha na kutozalisha na kueneza silaha ni muhimu sio tu kwa mustakabali wa amani, lakini kwa uwepo wetu.”

Ameongeza kuwa viongozi wa kimataifa lazima wawekeze katika amani kwa kuimarisha mifumo na zana zinazozuia kuenea na matumizi ya silaha hatari ikiwa ni pamoja na kutekeleza Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia na kwa kuunda suluhu za upokonyaji silaha.

Amehitimisha ujumbe wake kwa kusema kuwa ajenda mpya ya amani iliyopendekezwa inajumuisha mikakati na mbinu mpya za kuondoa vitisho vinavyoletwa na silaha za nyuklia, kemikali na kibayolojia na hatari nyingine zinazojitokeza, kama vile mifumo ya silaha zinazojiendesha.

Hivyo amesema “Katika siku hii muhimu, tuzungumze kwa kauli moja kuu, ya wazi na ya umoja. Ni wakati wa kuacha uendawazimu. Tunahitaji upokonywaji silaha sasa.”