Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Simulizi: Kusaidia kutibu afya ya akili nchini Madagascar, mtu mmoja baada ya mwingine

Mwanamke anahudhuria mashauriano na daktari wa neva anayeungwa mkono na Shirika la Afya Ulimwenguni.
© WHO Madagascar/Flora Dominique Atta
Mwanamke anahudhuria mashauriano na daktari wa neva anayeungwa mkono na Shirika la Afya Ulimwenguni.

Simulizi: Kusaidia kutibu afya ya akili nchini Madagascar, mtu mmoja baada ya mwingine

Afya

Migogoro ya kibinadamu inayoendelea kusini mwa Madagascar imezidisha hali ya watu kupata matatizo ya afya ya akili, lakini Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO limekuwa likiwasaidia wagonjwa kwa kutoa ushauri wa kiakili.

Henrielle Emasignavy anafanya kazi na WHO huko Ambovombe, kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Androy.  Amezungumzia juu ya wanavyotoa huduma kwa watu ambao wanapambana na shida za afya ya akili.

"Katika mji wa Ambovombe, tunaona hali kadhaa za watu kuugua afya ya akili ikiwa ni pamoja na matukio ya kisaikolojia, skizophrenia na kuwa na huzuni."

Kumekuwa na ongezeko la vijana wanaosumbuliwa na matatizo ya afya ya akili. Tunafikiri kwamba miongoni mwa wanaume vijana inaweza kuhusishwa na matumizi ya bangi, na miongoni mwa wasichana wa umri wa kati ya miaka 13-18 sababu inaweza kuwa kuvunjika kwa mahusiano au huzuni baada ya kujifungua.

Mojawapo ya sababu zinazochangia wote wanaume na wanawake ni wasiwasi wa kuishi katika hali zenye mkazo unaosababishwa na majanga ya kibinadamu yanayoendelea kusini mwa Madagaska.

Hivi karibuni tumekumbwa na ukame na vimbunga katika maeneo tofauti ya kusini ambayo yameongeza athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na maendeleo duni. Hii imewaacha watu wengi walio hatarini ambao wanaishi kote kusini wakihangaika kuishi. Mazao yanaposhindikana kuota , watu huwa hayana kitu cha kuwasaidia kuwapa uhakika wa kupata chakula na mara nyingi hukumbwa na njaa. Upatikanaji wa huduma za afya na ulinzi wa kijamii pia unaweza kuwa tatizo.

Henrielle Emasignavy wa WHO katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Androy.
UN News/Daniel Dickinson
Henrielle Emasignavy wa WHO katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Androy.

Waathirika wa Imani za kishirikiana

Nilikutana na mwanamke mmoja anayeitwa Elodie ambaye aliugua ugonjwa wa afya ya akili baada ya kujifungua, hii ilitokea baada ya kujifungua akiwa na umri wa miaka 20 na kumpoteza mtoto wake miezi sita baadaye.

Nilipokutana naye, niliona alikuwa amefungwa mnyororo kwenye kifundo cha mguu.

Mama yake aliniambia kuwa ni kwa ajili ya usalama wake mwenyewe kwani binti yake alikuwa akijaribu kutoroka. Kuna unyanyapaa mwingi unaohusishwa na watu wanaougua magonjwa ya akili. Wanasemekana kuwa "wamemilikiwa" na waathirika wa Imani za kichawi.

Matatizo ya afya ya akili yanatibika kwa mtazamo wa kimatibabu lakini kuongezeka kwa ujinga na umaskini kunawalazimu watu kuchukua hatua kali kama vile kuwafunga wagonjwa, jambo ambalo linazidisha ugonjwa ya akili kwa wanaougua.

Kupata huduma

Kupata matibabu ni changamoto kubwa kwa wagonjwa. Hospitali maalum iliyo karibu kwa ajili ya matibabu ya afya ya akili iko umbali wa kilomita 600, kwa hivyo ili kukidhi mahitaji yanayozidi kuongezeka ya huduma, WHO inaleta timu za matibabu kwa huduma ya wagonjwa wa nje.

Mama (katikati) wa Elodie (kulia) anasema ameitikia vizuri dawa.
UN News/Daniel Dickinson
Mama (katikati) wa Elodie (kulia) anasema ameitikia vizuri dawa.

Katika kipindi kimoja cha siku tatu, kulikuwa na jumla ya mashauria ya bure 93; Asilimia 67 ya wagonjwa hao walikuwa wanawake, akiwemo Elodie ambaye alionwa na daktari wa neva. Baada ya kuzungumza na daktari na kufanya mashauriano naye, alipewa dawa ambazo mama yake anasema zimesaidia kuboresha hali ya afya yake ya akili. Elodie anajitunza vizuri zaidi; kwa mfano, sasa anaweza kufanya usafi wake wa kibinafsi.

WHO ingependa kuwe na huduma zaidi zinazopatikana kwa watu kama Elodie, na ingawa ni wazi kwamba daktari wa akili anayetembelea hawezi kufanya kila kitu, ninafurahi kwamba tunaweza kusaidia wagonjwa wengine kwenye safari yao ya kupata nafuu.

Elodie anaungwa mkono na mama na dadayake, lakini cha kusikitisha sana kwamba wanafamilia wengine wote walimkataa na hivyo yeye na mama yake walilazimika kutoka nje ya nyumba ya familia.

Mama yake anatarajia binti yake atapona kabisa hivi karibuni, kwa hivyo Elodie anaweza kuishi maisha ya kawaida tena na hivyo aweze kupata pesa na kuchangia familia ya wanawake watatu.