UNEP na CITES wawalinda farua walio hatarini kutoweka Kenya
UNEP na CITES wawalinda farua walio hatarini kutoweka Kenya
Mkataba wa marufuku ya biashara ya pembe za faru inayotekelezwa kupitia mkataba wa kuwalinda wanyamapori walio katika hatari ya kutoweka, CITIES, umepata msukumo mpya.
Hii ni baada ya Kenya kuhamisha faru 21 kutoka hifadhi na mbuga za wanyama 3 hadi Loisaba kaunti ya Laikipia. Mkataba huo unaushirikisha Umoja wa mataifa kupitia shirika lake la mazingira, UNEP.
Kina Mama ambao ni wakaazi wa Koija eneo lililo jirani ya hifadhi ya wanyama ya Loisaba katika kaunti ya Laikipia walifika kwa wingi kujumuika na jamii baada ya operesheni ya kuwahamisha faru kukamilika.
Kwenye hafla maalum ya kusherehekea mafanikio ya operesheni ya kuwahamisha faru 21, wadau wa serikali na jamii walijumuika pamoja.
Jamii na wanyama waishi kwa amani
Operesheni hiyo ilianza katikati ya Januari mwaka huu kwa kuwahamisha faru wa kike na kiume kutokea mbuga 3 tofauti za wanyama.
Safari hiyo ilianza kwa kuwaandaa faru kwa kuwachoma sindano ya usingizi Kabla ya kuwapakia kwenye makasha maalum yaliyobebwa kwa malori.Faru 21 walisafirishwa kutoka Mbuga za Nairobi, Ol Pejeta na Lewa. Hifadhi ya Loisaba ndiyo makaazi yao mapya.
Thomas Silvester ni afisa mkuu mtendaji wa hifadhi ya Loisaba iliyoko kaunti ya Laikipia na amefurahishwa sana na hatua hiyo ya uhamisho kwani, “Ile sehemu ambayo imetengewa faru kwa nchi hii imekuwa ndogo kwani idadi imeongezeka. Kwahiyo sisi kama Loisaba tuliomba nafasi hii kwa idara ya wanyamapori, KWS, kuwaeleza kwamba Tuko tayari kutenga hifadhi na kuwekeza hapo ili tuwe tayari kupokea faru hapo. Na ni kitu muhimu kuongeza sehemu ya kuhifadhi faru kwani wanahitaji nafasi ili wazaane. Pia madume yamekuwa yakipigana.”
Makaazi ya jadi ya Faru
Hifadhi ya Loisaba ina ukubwa wa ekari alfu 58 na nusu yake imetengewa faru hao 21.
Wataalam wa wanyamapori waliteua faru 11 wa kike na 10 wa kiume kuhamishwa kutoka mbuga ya Nairobi, Lewa na Ol Pejeta.
Idadi kubwa ya faru hao waliohamishwa wametokea mbuga ya Lewa na Ol Pejeta ambazo ziko kaunti ya Laikipia.
Ifahamike kuwa takwimu rasmi za serikali zinaashiria kuwa Kenya ilikuwa na faru elfu 20 katika miaka ya sabini Kabla ya majangili kuwafyeka karibu wote katika muda wa miaka 50. Idara ya wanyamapori nchini Kenya, KWS, iliasisiwa mwaka 1989 wakati ambapo idadi ya faru ilikuwa imepungua hadi 400 kwasababu ya ujangili.
Faru mweusi yuko kwenye orodha ya mkataba unaolinda wanyama na mimea iliyo katika hatari kubwa ya kutoweka, CITES. Kufikia sasa, juhudi za uhifadhi wa faru zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Idadi ya faru imefikia 1004 zinaeleza taarifa rasmi za serikali. Jee wakaazi wa Laikipia wana mtazamo upi kuhusu operesheni hii?
Ellie Modestar ni mkaazi wa Koija iliyo nje ya hifadhi ya Loisaba na anaamini huu ni mwanzo mzuri, ”Faru ni mnyama muhimu sana kwa jamii na sisi kama Kina mama. Ni kama ndoto kwetu sisi. Miaka hamsini iliyopita tulielezwa na mababu zetu kuwa faru walikuwa wakizurura vijijini na msituni lakini maajabu sisi wenyewe hatujawaona. Faru kama mnyama mwengine ni muhimu na tunahifadhi na tunawapenda. Kabla ya faru kuja tulikuwa tumeelimishwa na Loisaba kuhusu umuhimu wa wanyama. Walipoongezea faru tumepata mafunzo kuhusu umuhimu na uhifadhi Wake.”
Faru weupe wawili waliosalia duniani
Barani Afrika, Kenya ni ya tatu baada ya Afrika Kusini na Namibia kwenye orodha ya mataifa yaliyo na faru wengi duniani. Rose WAMBUI ni mkaazi wa Kimanjo eneo la karibu na Mbuga ya Ol Pejeta wanakohifadhiwa faru 2 weupe wa kaskazini waliosalia duniani na anahisi safari ndefu huanzia Kwenye hatua ya kwanza nayo ni,
”ndege ndio zilianza tukashangaa nini kinaendelea. Unajua sisi maasai tu naogopa kuvurugaba na Wasamburu. Tukajiuliza kwani Wasamburu wamefanya kitu? Tukaona magari ya polisi yaliyo na ving’ora yakifuatana. Hapo ndipo tulipoona malori yaliyosheheni makasha makubwa tukaambiwa ni faru. Vile tumelelewa tunaona faru ni muhimu kwani serikali inapata pesa pale watalii wanapokuja kuwaona. Wanapenda kuona wanyapori wakubwa. Wakija ndio Kenya inapata fedha za kigeni kisha watoto wetu watasoma. Pia ajira inapatikana kama Mimi nilifanya kazi kwenye hoteli za watalii kwa muda. Tunawapenda sana.”
Jamii inahitaji uhamasisho
Idadi kubwa ya faru weusi waliohamishiwa Loisaba walitokea hifadhi ya Lewa. Josephine NDIRIAS anasimamia Kina Mama kwenye eneo la Mukogodo lililoko karibu na hifadhi ya Lewa na anaamini kuwa, ”ni Pato kubwa sana kwa nchi kwani watu wengi wameajiriwa kwenye hoteli za watalii. Lakini wakati mwengine nahisi jamii zinazoishi kwenye maeneo hayo hazifahamu haswa kinachoendelea. Hawana shughuli na kinachoendelea.”
Kenya inashirikiana na jamii ya kimataifa kuhifadhi faru. Operesheni ya kuhamisha faru ilifanikishwa na wafadhili kama San Diego Zoo Wildlife Alliance, shirika la The Nature Conservancy, hoteli ya kifahari ya Elewana na walezi wa wanyamapori Space for Giants. Dkt. Max Graham ni afisa mkuu mtendaji wa Space for Giants na anaamini huu ndio mkondo mwafaka wa kufuata, "Wanachohitaji faru ni mahala salama Pa lipo na chakula na maji ya kutosha na idadi yao itaongezeka tu. Kwasababu ya kitisho cha ujangili, sisi kama wahifadhi kwa Pamoja na serikali ya Kenya ikiongozwa na idara ya wanyamapori wamelazimika kuwahifadhi faru kwenye sehemu salama zilizo na ulinzi mkubwa. Mkakati huo umeleta fanaka. Ni ushahidi halisi kwa nchi hii.”
Kwa mujibu wa UNEP operesheni ya kuwarejesha faru kwenye hifadhi ya Loisaba ni hatua muhimu katika juhudi za kuwahifadhi na kuiongeza idadi. Yote hayo yanafanikiwa kwa ushirikiano na jamii zinazoishi ndani ya Loisaba ambao wamekuwapo hata Kabla ya eneo hilo kuwa hifadhi ya wanyama.