Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama Kuu Tanzania katika kuimarisha haki sasa ‘kuziba nyufa,badala ya kujenga ukuta’

Mkuu wa mkoa wa Morogoro nchini Tanzania, Fatma Mwassa (kushoto) akiwa na baadhi ya viongozi wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria mkoani humo.
UN News
Mkuu wa mkoa wa Morogoro nchini Tanzania, Fatma Mwassa (kushoto) akiwa na baadhi ya viongozi wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria mkoani humo.

Mahakama Kuu Tanzania katika kuimarisha haki sasa ‘kuziba nyufa,badala ya kujenga ukuta’

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Nchini Tanzania maadhimisho ya Wiki ya Sheria yakiwa yanaendelea, mashariki mwa taifa hilo Mahakama Kuu imesema imeweka kipaumbele cha kutumia elimu kuimarisha haki badala ya kusubiri hadi tatizo litokee na kufikishwa mahakamani.

Hatua hiyo inaenda sambamba na lengo namba 16 la malengo ya maendeleo endelevu SDGs yaliyopitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 2015 likisisitiza amani, haki na taasisi thabiti.

Uvunjivu wa amani utokanao na migogoro kwenye jamii ni moja ya maeneo yanayomuikwa ili kuhakikisha amani inakuweko na hivyo kuwezesha kufikia SDGs mwaka 2030.

Amani iweze kupatikana kwa ueledi badala ya amri za mahakama

Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Morogoro Paul Ngwembe akihutubia tukio hilo kwenye  viwanja vya jeshi la Zimamoto na Uokoaij mjini Morogoro amesema wanatekeleza hilo kupitia kauli mbiu ya mahakama kwa mwaka huu wa 2023 ambayo ni ‘umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu, wajibu wa mahakama na wadau,’”

Amesema kauli mbiu hiyo “ina lengo moja la kuhakikisha amani katika nchi inapatikana kwa usahihi na kwa ueledi. Kwamba tutatembea kwa kiasi kikubwa kwenye suala zima la usuluhishi badala ya umalizaji wa mashauri kwa njia za amri au DECREE za mahakama.”

Soundcloud

Tutaandaa vipindi vya kuelimisha wananchi

Hatua hiyo ya mahakama ikaungwa mkono na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa ambaye akaanza kuweka mikakati ya kufanikisha hatua hiyo akisema, “tutawakusanyia hao wenyeviti na watendaji wa vijiji na kata ili wapate somo. Na katika mikutano hiyo tutakuwa na wananchi ili nao wapate uelewa.”

Kwa mujibu wa Jaji Mfawidhi Ngwembe mwaka 2022 kituo cha utoaji haki Jumuishi kimefanikiwa kutoa Elimu ya Sheria kwa wananchi 26,386 ndani ya Mkoa wa Morogoro.

Na ili kuongeza idadi ya uelewa, Mkuu wa Mkoa Bi. Mwassa akaendelea kuelezea hatua zaidi akisema, “mikutano yetu itakuwa na watu wasiopungua 1,000 kila mmoja. Lakini pia tutarekodi vipindi ambavyo mnatoa masomo na sisi tutatumie vipindi hivyo kwenda kufanyia mikutano ya vijiji kwa kutumia magari ya sinema ambayo huwa tunatumia kutoa elimu kwa wananchi wetu.”

Bi. Mwassa amesema ni dhahiri kuwa faida za mapatano ni nyingi katika migogoro kuliko hasara. “Lakini pia taifa linapiga hatua za maendeleo kama kuna amani na watu wake wakiwa na muda mrefu wa kuzalisha mali.”

Wananchi wa Morogoro nao wapaza sauti

Baadhi ya wakazi wa Morogoro ambao mwandishi wa habari amezungumza nao hawakusita kutoa maoni yao kuhusu hatua hii ambapo mmoja wao Sijali Saidi amesema, “hii itasaidia kwa kiwango kikubwa kwa sababu wananchi wengi hawana ufahamu na sheria. Kwa hiyo wanavyopita kuelimisha wananchi kidogo mtu atakuwa na kitu cha kuzungumzia. “

Ramadhani Selemani akawa na ombi kwa serikali akisema, “kama imekuwa na wazo hili la kufikia wananchi ni jambo jema na naomba iendelee nalo kwa sababu wananchi wengi sio siri hawafahamu haki zao za msingi za kisheria. Tunaona mtaani watu wanabaka. Kwa hiyo rai wangu wananchi wasifanye makosa ambayo wanajua wanaweza kuchukuliwa hatua mbalimbali. Kwa mfano kuhusu kubaka, kufanya mapenzi na mwanafunzi. Wananchi wasichukue sheria mkononi wanaweza kufungwa.”

Kilele cha Wiki ya Sheria nchini Tanzania ni tarehe Mosi mwezi Februari mwaka 2023.