Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yawashika mkono wasichana Afrika kuingia katika sayansi ya kilimo

Bernice Armelle Bancole ni mwanasayansi katika Sayansi ya Kilimo. Anatoka Benin. Anataka kusaidia kutokomeza matumizi makubwa ya viua wadudu katika nchi za Afrika.
UNESCO/OWSD
Bernice Armelle Bancole ni mwanasayansi katika Sayansi ya Kilimo. Anatoka Benin. Anataka kusaidia kutokomeza matumizi makubwa ya viua wadudu katika nchi za Afrika.

FAO yawashika mkono wasichana Afrika kuingia katika sayansi ya kilimo

Wanawake

Katika kuelekea siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi itakayoadhimishwa Jumapili Februari 11 shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO limesema katika Dunia ya sasa inayobadilika kwa kasi, sayansi na ubunifu vina jukumu muhimu katika kushughulikia changamoto zinazoiandama Dunia.

Hata hivyo licha ya hatua kubwa zilizopigwa katika kuendeleza sayansi wanawake na wasichana wanaendelewa kukabiliwa na vikwazo vingi kuingia katika tasnia hiyo ndio maana shirika hilo limeamua kuchukua hatua kuendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo hususan wasichana katika sayansi ya takwimu katika kilimo ikiwemo nchini Côte D’Ivoire  

Katika kijiji cha Konou wilaya ya Jacqueville kundi la wanafunzi kutoka Taasisi ya kimataifa ya Takwimu na Uchumi ENSEA mjini Abidjan wamewasili kuzungumza na wakulima kuhusu masuala ya kilimo na umuhimu wa takwimu, miongoni mwao ni Mone Désirée Daud ambaye anasema "Nilipokuwa mtoto nilikuwa nashangaa baada ya kumaliza kula chungwa nachukua mbegu na kuifukia ardhini, halafu siku chache baadaye naona majani na maua, kwa kweli nilikuwa najiuliza, je! Nini kinafanyika hata inakuwa hivi?"

Maswali hayo ndio yaliyyomtia hamasa Mone ambaye sasa ana umri wa miaka 27 alipomaliza elimu ya awali kuanza safari ya kusomea sayansi ya usimamizi wa udongo na uzalishaji wa mazao  au agronomy kabla ya kujiunga na masomo ya takwimu za kilimo na kujitolea maisha yake kwa hilo. Leo yeye ndiye mwanatakwimu wa kwanza katika familia yake akiamini kwamba takimu ni muhimu kwa kuboresha uzalishaji wa kilimo na watakwimu wengi hasa wanawake na wasichana kama yeye wanachangia maendeleo endelevu hususan Afrika “Takwimu zinaweza kuwa na manufaa kwa kilimo cha Kiafrika kwa sababu sasa tutakuwa na wataalamu wapya wa takwimu za kilimo waliopatiwa mafunzo ambao, tunaweza kutoa takwimu ambazo zitawawezesha watunga sera wetu kufanya maamuzi sahihi kulingana na hali halisi ya kilimo, ardhi zetu na taarifa tunazokusanya."

Umuhimu wa takwimu katika kilimo

Kwa mujibu wa FAO ukusanyaji wa takwimu ni msingi katika kuelewa changamoto za uhakika wa chakula, na nchi nyingi zinazoendelea hazina takwimu za kutosha na hivyo kusababisha wafanya maamuzi kushindwa kuchukua hatua zinazostahili katika masuala ya kilimo ndio maana shirika hilo limekuwa likiwasaidia vijana na hasa wasichana kwa ufadhili wa elimuya shahada ya pili ya takwimu za kilimo ili kuziba pengo lililopo

Mkulima akifanya kazi katika shamba lake la mbogamboga.
11-12-2023_FAO_Lopit_South Sudan.jpg
Mkulima akifanya kazi katika shamba lake la mbogamboga.

Neli Georgieva Mihaylova, ni Mtakwimu Mkuu wa FAO anasema "Tangu 2012, FAO imekuwa mwenyeji wa mkakati wa kimataifa wa kuboresha kilimo na takwimu  vijijini ili kukabiliana na kushuka kwa mifumo ya takwimu za kilimo katika nchi nyingi zinazoendelea. Mwaka 2023, wanazuoni 48 kutoka nchi 24 za Kiafrika walisoma programu hii na walihitimu kwa mafanikio. Na tunajivunia kuwa asilimia 43 kati yao walikuwa wanawake.”

Wengi wa wanafunzi hao kama Mone ambaye bado hajahitimu wakimaliza mafunzo hurejea katika nchi zao na kuchangia katika kuimarisha sekta ya takwimu za kilimo hivyo kusaidia kukuza uhakika wa chakula.

Mone anaishukuru FAO kwa kumpa fursa hii muhimu ya kutimiza azma yake kama msichana aliyejikita katika sayansi ya kilimo na takwimu.

Maudhui ya siku ya mwaka huu ni "Wanawake na Wasichana katika Uongozi wa Sayansi, Enzi Mpya ya Uendelevu."

FAO inasema ingawa kuna hatua ziimepigwa lanini bado katika ulimwengu wa kisasa unaoendelea kwa kasi, sayansi na uvumbuzi vina jukumu muhimu katika kushughulikia changamoto za kimataifa na wanawake na wasichana wanaendelea kukabiliwa na vikwazo vikubwa vya kutafuta taaluma ya sayansi.