Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uturuki na Syria: Manusura wa matetemeko ya ardhi bado wako taabani- UN

Hatay, Türkiye. Vifusi vya majengo vilivyosababishwa na tetemeko la ardhi
© WFP/Film ıcabı
Hatay, Türkiye. Vifusi vya majengo vilivyosababishwa na tetemeko la ardhi

Uturuki na Syria: Manusura wa matetemeko ya ardhi bado wako taabani- UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Mwaka mmoja baada ya matetemeko makubwa ya ardhi yaliyokumba Uturuki na Syria, Umoja wa Mataifa unasema hali ya  mamilioni ya manusura waliokumbwa na matetemeko hayo pamoja na wenyeji waliowapatia hifadhi inazidi kudorora.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na lile la afya, WHO yametoa tathmini hiyo kupitia wasemaji wake jijini Geneva, Uswisi wakati wakizungumza na waandishi wa habari.

Shabia Mantoo ambaye ni msemaji wa UNHCR amesema “Uturuki ni moja ya nchi zinazoongoza duniani kwa kuhifadhi wakimbizi, ilhali Syria nayo ambako mamilioni ya watu wamefurushwa makwao kutokana na janga la miaka 13 sasa hata kabla ya tetemeko, inakumbwa na janga kubwa la kiuchumi.”

Ameongeza kuwa, “nchini Syria, takribani asilimia 90 ya watu ni mahohehahe, milioni 12.9 hawana uhakika wa kupata chakula ilihali milioni 7.2 ni wakimbizi wa ndani."

Matetemeko hayo ya ardhi yalikumba eneo la mpakani mwa nchi mbili hizo alfajiri ya tarehe 6 Februari mwaka 2023, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 50,000 nchini Uturuki, na zaidi ya 5,000 kaskazini-magharibi mwa Syria na maelfu wengine walijeruhiwa.

Uharibifu ulikuwa mkubwa,  kwani maelfu ya majengo, yakiwemo ya miundombinu muhimu kama vile shule na hospitali yaliporomoka kutokana na ukubwa wa tetemeko.

“Uturuki inahifadhi wakimbizi milioni 3.4, na tetemeko la ardhi limeathiri eneo ambalo ni makazi ya wakimbizi milioni 1.75,” amesema Bi. Mantoo.

Licha ya hatua za kutia moyo na jumuishi za Uturuki kwa suala la kiutu, kwa usaidizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa, bado madhara ya matetemeko yako dhahiri kwa wakimbizi na wenyeji wao, amesema afisa huyo wa UNHCR.

Ameongeza kuwa kutokana na ongezeko la mahitaji, wakimbizi wengi wanaamua kutumia mbinu mbadala za kuishi ikiwemo kpunguza mlo na kukopa fedha zaidi.

“Janga hili tayari limekuwa na madhara kwenye afya ya akili na ustawi wa jamii husika. Watu wengi wamepoteza familia na marafiki,” amesema Bi. Mantoo.

Kwa upande WHO imesema madhara ya tetemeko hilo yatadumu kwa miaka kadhaa ijayo ambapo watu wengi wataendelea kuishi kwenye makazi ya muda.

“Nchini Uturuki, tetemeko limesababisha uwepo wa mahitaji mapya na ya dharura ya kiafya kwenye jamii zilizoathiriwa, ikiwemo kwa wakimbizi na wenyeji,” amesema Tarik Jasarevic, msemaji wa WHO.

Ameongeza kuwa janga hilo lilivuruga ufikiaji wa huduma za afya kama vile kwa wajawazito na watoto wachanga, chanjo, usimamizi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, afya ya akili, na  huduma kwa watu wenye ulemavu.

Kwa zaidi ya muongo mzima ,Syria imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo mzozo uliodumu muda mrefu, ukosefu wa utulivu kiuchumi, janga la afya kama vile coronavirus">COVID-19, kipindupindpu na sasa tetemeko la mwaka jana la ardhi.

 Kutoka ofisi ya Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, OSE, Jenifer Fenton, ambaye ni msemaji wa ofisi hiyo amesema, “baada ya matetemeko ya ardhi tumeshuhudia kiwango cha chini kabisa cha uhasama, na mwelekeo mpya wa kidiplomasia katika janga la Syria. Hii,  hata hivyo, haikuleta maendeleo halisi. Kwa kusikitisha, mwaka 2023 umeshuhudia kuibuka upya na kwa kiasi kikubwa kwa mapigano, na hivyo kufanya hali ya kibinadamu kuwa mbaya zaidi na ukosefu wa mchakato wa maana wa kisiasa.”