Guterres: Acha watu zaidi wasikie sauti za waathirika na manusura wa ugaidi
Guterres: Acha watu zaidi wasikie sauti za waathirika na manusura wa ugaidi
Ikiwa leo tarehe 21 Agosti ni Siku ya Kimataifa ya Kuwakumbuka na Kuwaenzi Waathirika wa Ugaidi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake mahususi kwa ajili ya siku hii amewasihi watu wote ulimwenguni kuhakikisha kwamba wale waliofariki au kukumbwa na athari za muda mrefu za ugaidi hawasahauliki kamwe.
“Tunakusanyika pamoja kuwakumbuka waathirika na manusura wa ugaidi. Kusimama na familia zilizobadilika daima. Na kuazimia kujenga mustakabali wenye amani zaidi - pamoja.” Amesema.
Kauli mbiu ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu na Heshima kwa Waathirika wa Ugaidi ni: "Urithi: Kupata Matumaini na Kujenga Mustakabali wa Amani."
Bwana Guterres anasema katika Siku hii, “tunatoa heshima zetu kwa wale wote waliofarik au kujeruhiwa kupitia mashambulizi ya kigaidi duniani kote.”
“Tunatambua kazi iliyotukuka ya wale waathiriwa na walionusurika ambao wameamua kutumia uzoefu wao kuleta mabadiliko.” Anasema Guterres akiongeza, “Na tunakaribisha uzinduzi wa Mradi wa Urithi, ambao unasaidia ushuhuda wao kusikika kote ulimwenguni.”
Katibu Mkuu Guterres anatoa wito kwa ulimwengu kwamba, “Sote tujitolee kuunga mkono waathirika na walionusurika, kupaza sauti zao, kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha kwamba maisha yaliyotwaliwa na kubadilishwa na ugaidi hayasahauliki kamwe. Na kujenga maisha bora ya baadaye kwa ajili yetu sote.”
Maonesho ya kumbukumbu
Kama sehemu ya kuadhimisha Siku hii, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kukabiliana na Ugaidi (UNOCT) kupitia Kampeni ya Kumbukumbu, kwa njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii inasambaza kumbukumbu za karibu za waathirika wa ugaidi kupitia filamu na picha.
Mmoja wao ni Nigeel Namai alikuwa na umri wa miezi 4 baba yake alipouawa katika shambulio la mwaka 1998 kwenye Ubalozi wa Marekani mjini Nairobi, Kenya.
Wakati wowote Nigeel anapovaa suti, inaleta kumbukumbu na simulizi kuhusu baba yake, ambaye kila mara alikuwa nadhifu.
“Kila wakati ninapovaa suti inarejesha kumbukumbu ya simulizi ambazo mama alikuwa ananisimulia kuhusu baba. Ningependa baba yangu ajivunie. Popote alipo aangalie aseme: “Oo, ingawa siwezi kuwa naye kimwili ninajivunia yeye kama mvulana mdogo na pia mwanaume mdogo.”