Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Angola: Asante UN sasa jamii inaniheshimu- Mnufaika wa SAMAP

Mashamba darasa kwa wakulima nchini Angola
©FAO/C.Valencia
Mashamba darasa kwa wakulima nchini Angola

Angola: Asante UN sasa jamii inaniheshimu- Mnufaika wa SAMAP

Ukuaji wa Kiuchumi

Hivi sasa jamii inaniheshimu kwani mimi si tegemezi tena, anasema Albertina Cemente, mnufaika wa mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD nchiin Angola ambao umenusuru vijana kama yeye kukimbilia mijini kusaka maisha bora. 

Albertina mwenye umri wa miaka 24, na mama wa watoto watatu anakumbuka kuwa awali kabla ya mradi wa IFAD kuanza alikuwa tegemezi kwa wazazi wake kwa kila kitu.

Hata hivyo Albertina ambaye ni mkulima alinusurika kuwa sehemu ya vijana hao wanaokimbilia  mjini baada ya IFAD kubisha hodi kijijini kwao na kuwawezesha kuanzisha chama cha ushirika cha wakulima wakikipatia jina la WeiWei.

Albertina anasema “tulipata fursa ya kupata mkopo kupitia chama hicho cha ushirika, kabla ya kupata mkono uzalishaji ulikuwa mdogo, lakini baada ya kupata mkopo uzalishaji umeongezeka na hivyo tukivuna tunauza na kurejesha mkopo.”

Nchini Angola kilimo kinachangia asilimia 10 tu pato la ndani la taifa, kwani taifa hilo linategemea zaidi sekta yake ya mafuta na gesi

Kwa hivyo basi ili kuongeza mapato na ustawi wa wakulima wadogo wadogo na wafanyakazi kwenye sekta hii, IFAD inashirikiana na serikali ya Angola, kutekeleza mradi wa SAMAP ambao unahusisha kuanzisha mashamba darasa ya wakulima, vikundi vya kuweka na kukopa, na pia kuwawezesha kununua pembejeo za kilimo kama vile mbegu. 

Kutoka kilo 20 kwa siku hadi kilo hadi 500 kwa siku za unga wa mahindi

 Kupitia mradi huo wa SAMAP, Albertina na wanakikundi wenzake wakanunua mashine ya kusagisha mahindi.

Ujio wa mashine ya kisasa, kwa mujibu wa Albertina ulileta mabadiliko kwnai, “kabla ya kununua mashine hii, tulikuwa tunasagisha mahindi kwa kutumia mashine ya kuzungusha kwa mkono.  Tulitumia nguvu sana. Kwa siku tulisagisha mahindi na kupata kilo 20 tu za unga. Lakini baada ya kupata mashine hii inayotumia moto, kwa siku tunasagisha na kupata hadi kilo 300, 400 au hata 500 kwa siku. “

Maisha ya familia yamekuwa bora, watoto wanakwenda shuleni

Uzalishaji wa mazao kwa wakulima katika kikundi hiki cha Weiwei umeongezeka mara tatu, na maisha yamekuwa bora.

Ernesto Cassinda, Mtathmini Msaidizi wa Mradi wa SAMAP anathibitisha akisema kuwa “nyumbani mazingira ya familia yamekuwa mazuri. Hivi sasa wazazi wanapeleka watoto wao shuleni. Zamani ilikuwa vigumu kupata usafiri wa kuwapeleka shuleni. Lakini kutokana na ongezeko la uzalishaji wameweza kununua pikipiki.”

IFAD inasema simulizi hizo zinawafurahisha mno kwa kuona kuwa mradi wa SAMAP umeleta mabadiliko chanya kwenye maisha ya watu.

Sasa kwenye video anaonekana Albertina na watoto wake wakitembea bila hofu kwani kwa mara ya kwanza,  Albertina anaweza sio tu kujisaidia yenye mwenyewe na familia yake, bali pia mtazamo wa jamii kwake yeye umebadilika kwani wanajamii wanamheshimu.