Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali katika Hospital ya El-Najar Gaza iko nje ya uwezo wetu – Wahudumu wa afya

Mhudumu wa afya akimpatia matibabu mmoja wa watoto aliyejeruhiwa huko Ukanda wa Gaza. (Maktaba)
© WHO
Mhudumu wa afya akimpatia matibabu mmoja wa watoto aliyejeruhiwa huko Ukanda wa Gaza. (Maktaba)

Hali katika Hospital ya El-Najar Gaza iko nje ya uwezo wetu – Wahudumu wa afya

Msaada wa Kibinadamu

Ukanda wa Gaza, hospitali nyingi hazina wahudumu wa kutosha kwani wafanyakazi wa sekta ya afya wameondoka kwa sababu ya maagizo ya kuhama au ukosefu wa usalama. Wakati huo huo, njia ambazo zingetumiwa na wagonjwa kufika katika vituo vya afya zimetatizwa na hali mbaya ya usalama.

Bila huduma ya afya ya kutosha, mateso katika Gaza yanaongezeka kila saa, linasema shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni.

Hebu kwa leo tuangazie hospitali ya El-Najar iliyoko Rafar. Hali mbaya inayoonekana hapa ni karibia sawa na hospitali nyingine nyingi katika ukanda wa Gaza. Nje ndani, kote katika eneo la hospitali ni kadamnasi. 

Huyu ni Dkt. Munther Abu Sharkh, anasema, "Tunapokea idadi isiyoweza kufikirika, kando ya watu waliojeruhiwa pia tunapokea idadi kubwa ya wagonjwa. Hospitali haiwezi kubeba idadi hii ya wagonjwa. Katika siku za kawaida tulikuwa tukipokea idadi ya juu zaidi ya wagonjwa 300 kwa siku sasa tunapata elfu moja na vitanda 9 tu vinavyopatikana hospitalini na vitanda 9 haviwezi kushughulikia wagonjwa elfu moja kwa siku."

Anayoyasema Dkt. Munther yanaonekana wazi, anapitishwa mtu akiwa amelazwa kwenye kitanda cha magurudumu katikati ya watu wanaosaka huduma. 

Dkt. Munther sasa anaomba usaidizi akisema kwamba “Hali sasa iko nje ya uwezo wao na kwamba wanatoa wito kwa mtu yeyote, chombo chochote kinachoweza kuwapatia huduma za matibabu kuharakisha na kufanya hivyo kwa haraka kwani hali ni janga na iko nje ya uwezo.”

Bwana mmoja yuko hapa, yeye mwenyewe kwa bandeji amefunga tumbo na kidole lakini pia anamwangalia mpwa wake Yousef ambaye alikuwa anapatiwa huduma kwingine lakini sasa wamekimbilia hapa. Ahmed anaeleza, 

“Tulipokuwa hospitali ya Al-Aqsa mambo yalikuwa sawa, tulipata matibabu na waliohitaji kufanyiwa upasuaji wamefanyiwa, pia mpwa wangu Yousef alifanyiwa upasuaji na kukatwa mguu, pia Yousef alitakiwa kila siku kusafishwa jeraha. Hadi muda huu tunakaa hapa katika zahanati hii, hata sio mahali rasmi, kimsingi tuko kwenye shoroba, na mimi na dada zangu tulilala hapa, ilikuwa usiku mgumu sana. Kwa sababu wanafamilia yangu wamejeruhiwa na wanahitaji matibabu na dawa za kutuliza maumivu, lakini hakuna kinachopatikana hapa si dawa zao wala ganzi.”

Katika mazingira kama haya kila kitu kimevurugika. Hakuna hata faragha tena. Hilo linamgusa sana Dkt. Areej, 

"Kusema kweli, matabibu wote wanajaribu kutoa faragha hasa kwa wanawake, kwa sababu  hali ya hospitali na idara zake zimejaa, ni ngumu kuwa na faragha kwa kweli. Kusema ukweli hali kwa wanawake ni ngumu sana katika hali hizi."