Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunapaswa kuhakikisha kunyonyesha maziwa ya mama kwa mtoto mahali pa kazi inawezekana – UNICEF Rwanda

Banamwana Yvette Mfanyakazi wa Ofisi za Jiji na Kigali.
UNICEF
Banamwana Yvette Mfanyakazi wa Ofisi za Jiji na Kigali.

Tunapaswa kuhakikisha kunyonyesha maziwa ya mama kwa mtoto mahali pa kazi inawezekana – UNICEF Rwanda

Wanawake

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF Rwanda kwa kushirikiana na wadau kama Shirika la Taifa la Maendeleo ya Mtoto nchini humo, NCDA, wanatoa wito kwa sekta binafsi, taasisi za serikali, washirika, asasi za kiraia kuweka mazingira rafiki ya unyonyeshaji mahali pa kazi. Evarist Mapesa anaangazia faida ya moja ya vyumba vya kunyonyeshea mahali pa kazi jijini Kigali Rwanda. 

Katika moja ya maeneo tulivu ya jiji lenye shughuli nyingi za jiji la Kigali-Rwanda kumetengwa chumba eneo maalumu lenye mazingira yote yanayofaa kwa akina mama kuwanyonyesha Watoto wao au hata kukamua maziwa na kuyahifadhi. 

Banamwana Yvette Mfanyakazi wa Ofisi za Jiji na Kigali anasema alikuwa anapoteza muda mwingi njiani kutoka kazini kwenda kumnyonyesha mtoto na kurudi kazini.  

Banamwana Yvette Mfanyakazi wa Ofisi za Jiji na Kigali akiwa na mtoto wake baada ya kumnyonyesha kazinini.
UNICEF
Banamwana Yvette Mfanyakazi wa Ofisi za Jiji na Kigali akiwa na mtoto wake baada ya kumnyonyesha kazinini.

Kayitesi Sophie mwajiriwa wa Benki ya Kigali anasema, “tulikuwa tunakamua maziwa maliwatoni na baadaye kuyamwaga kwa kuwa hatukuwa na pa kuyatunzia.” 

Vick Mujiji, yeye ni mfanyakazi wa kampuni ya Africa Improved Foods anaeleza kwamba kukitumia chumba cha kunyonyeshea kumeongeza tija kazini kwake kwani ofisi yake haiko mbali na hapa na kwa hivyo anaweza kuja muda wowote akakamua maziwa yake na kurejea kazini. 

Ingabire Assumpta ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Maendeleo ya Mtoto Rwanda (NCDA) anasema, “Wengi wa watoto wanaonyonyeshwa katika saa ya kwanza mara tu baada ya kuzaliwa ni watoto wa vijijini kuliko wa mjini. Kwa hiyo ndio hiyo ilifanya tuwawezeshe wazazi kunyonyesha katika maeneo yao ya kazi. Ninawahamasisha mashirika mbalimbali ambao hawajaanzisha vyumba hivi kuanza kwani ni kwa faida yao pindi mama anapokuwa na uhakika kwamba mtoto wake amenyonya vizuri, ana afya na yuko karibu naye, atafanya kazi vizuri na tija inaongezeka.”  

 Baada ya mafanikio haya ya mfano, Mwakilishi wa UNICEF nchini Rwanda, Julianna Lindsey ana ujumbe, “Ujumbe wangu kwetu sote ni kwamba wanawake hawapaswi kuchagua kati ya kazi yao na kuchangia katika uchumi wa Rwanda na utimilifu wa taaluma zao dhidi ya kuhakikisha mtoto anapata lishe muhimu.”