Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bei za bidhaa za chakula zilipungua Desemba 2023 - FAO

Wanawake wakiwa wamekaa juu ya magunia ya mchele na mahindi huko Wajir, Kenya. (Maktaba)
FAO/Ami Vitale
Wanawake wakiwa wamekaa juu ya magunia ya mchele na mahindi huko Wajir, Kenya. (Maktaba)

Bei za bidhaa za chakula zilipungua Desemba 2023 - FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Kiwango cha bei za bidhaa za chakula duniani kilipungua mwezi Disemba 2023 ikilinganishwa na mwezi uliopita, huku kukiwa na kushuka kwa kasi kwa bei ya sukari ya kimataifa, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO.

Katika taarifa yake iliyotolewa hii leo kutoka Roma nchini Italia fahirisi ya bei ya chakula ya FAO, ambayo hufuatilia mabadiliko ya kila mwezi ya bei za kimataifa za bidhaa za chakula zinazouzwa kimataifa, ilifikia wastani wa pointi 118.5 mwezi Desemba, ikiwa ni chini ya asilimia 1.5 kutoka Novemba na kushuka kwa asilimia 10.1 kutoka mwezi Desemba mwaka 2022.

Kwa mwaka wa 2023 kwa ujumla, bei ilikuwa chini kwa asilimia 13.7 kuliko thamani ya wastani katika mwaka uliotangulia, na fahirisi ya bei ya sukari pekee ya kimataifa ilikuwa juu katika kipindi hicho.

Mazao mbalimbali 

Fahirisi ya Bei ya Nafaka iliongezeka kwa asilimia 1.5 kutoka mwezi Novemba, huku bei ya ngano, mahindi, mchele na shayiri ilipanda, kwa sehemu ikionesha usumbufu wa vifaa ambao ulizuia usafirishaji kutoka nchi kuu zinazouza nje.

Fahirisi ya Bei ya Mafuta ilipungua kwa asilimia 1.4 kutoka mwezi Novemba, ikionesha ununuzi hafifu wa mawese, soya, rapa na mafuta ya alizeti, huku mafuta ya soya yakiathiriwa. Kwa mwaka 2023 kwa ujumla, fahirisi hii ilikuwa asilimia 32.7 chini ya kiwango cha mwaka uliopita.

Fahirisi ya Bei ya Sukari ilipungua kwa asilimia 16.6 kutoka mwezi Novemba, na kufikia kiwango cha chini cha miezi tisa ingawa bado imepanda asilimia 14.9 kuanzia Desemba 2022. Kushuka kwa bei ya sukari kulichangiwa zaidi na kasi kubwa ya uzalishaji nchini Brazili, pamoja na kupungua kwa matumizi ya sukari ya miwa kwa uzalishaji wa ethanol nchini India.

Fahirisi ya Bei ya Nyama ilipungua kwa asilimia 1.0 kuanzia mwezi Novemba, na kufikia kiwango cha asilimia 1.8 chini ya ile ya mwezi Desemba 2022, nah ii iliathiriwa na mahitaji duni ya kuagiza kutoka barani Asia kwa nyama ya nguruwe.

Ili kukabiliana na mwelekeo huo, Fahirisi ya Bei ya Maziwa ya FAO iliongezeka kwa asilimia 1.6 kuanzia Novemba, ingawa bado imesimama kwa asilimia 16.1 chini ya thamani yake ya Desemba 2022. 

Ongezeko hilo la kila mwezi liliongozwa na nukuu za bei za juu za siagi na jibini, zikichagizwa na mauzo makubwa ya ndani barani Ulaya Magharibi kabla ya msimu wa likizo za mwisho wa mwaka. Wakati huo huo, mahitaji makubwa ya uagizaji wa kimataifa yalisababisha unga wa maziwa kuongezeka.

Kusoma zaidi bofya hapa