Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo ya Viwanda Afrika yajumuishe wanawake - UN

Wanafunzi wawili wa zamani wa Chuo cha Mafunzo ya Viwanda cha Zambia, kilichoanzishwa kwa usaidizi wa UNIDO na wadau wake, wanafanya kazi leo katika kampuni ya uhandisi.
UNIDO
Wanafunzi wawili wa zamani wa Chuo cha Mafunzo ya Viwanda cha Zambia, kilichoanzishwa kwa usaidizi wa UNIDO na wadau wake, wanafanya kazi leo katika kampuni ya uhandisi.

Maendeleo ya Viwanda Afrika yajumuishe wanawake - UN

Ukuaji wa Kiuchumi
  • Ujumuishaji wanawake utapanua wigo wa wanufaikaji 
  • Juhudi za ukuaji viwanda zijengewe mnepo 
  • UN imejizatiti kusaidia Afrika kufanikisha SDGs na Ajenda 2063 ya AU 

Kupanua wigo wa mbinu za kukuza uchumi, kuongea ajira n kutokomeza umaskini ni mambo yanayoweza kufanikiwa barani Afrika iwapo kasi ya ukuaji wa viwanda barani humo itaongezwa, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo ikiwa ni siku ya kukuza viwanda barani Afrika. 

Guterres kupitia ujumbe wake wa siku hii uliochapishwa kwenye wavuti wake anasema hatua hizo ziende sambamba na kukabili umaskini na kujenga mnepo, akimaanisha kwamba hata majanga yanapotekea waafrika waweze kuendelea kujipati kipato kupitia viwanda ambavyo vinaweza kuhimili mitikisiko. 

Hata hivyo Katibu Mkuu anasema ili harakati za kukuza viwanda Afrika ziweze kuwa na mafanikio ni lazima ziwe endelevu na jumuishi. 

Amerejelea ujumbe wa mwaka huu wa siku hii ya viwanda barani Afrika unaosema kuwa kuchochea kasi ya ukuaji viwanda barani Afrika kunategemea uwezeshaji wa mwanamke wa Afrika. 

Ajira za wanawake kwenye uzalishaji viwandani ziongezwe 

“Kuongeza idadi ya wanawake wanaoshiriki kwenye ajira za uzalishaji bidhaa ni jambo muhimu na la uhakika katika kuongeza tija na vile vile kuhakikisha manufaa ya uzalishaji kwenye viwanda yanafikia familia na wafanyakazi wa kwenye jamii,” amesema Katibu Mkuu. 

Hivyo anataka kila mtu katika siku hii aongeze juhudi maradufu kuvunja mipaka na kuondoa vikwazo vinavyozuia wanawake kushiriki na kunufaika na maendeleo ya viwanda na ubunifu wa kiteknolojia. 

Wafanyakazi wanatekeleza jukumu lao katika kiwanda cha uzalishaji nchini Ethiopia.
ILO Photo/Marcel Crozet
Wafanyakazi wanatekeleza jukumu lao katika kiwanda cha uzalishaji nchini Ethiopia.

Tumejizatiti kusongesha Ajenda 2063 ya AU 

Guterres anasema Umoja wa Mataifa kwa upande wake umejizatiti kwa uthabiti kabisa kuchochea juhudi hizo kwa kushirikiana na bara la Afrika katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, halikadhalika Ajenda ya Afrika ya 2063. 

“Kwa pamoja tunaweza kufiki dira ya kuwa na amani na ustawi kwa Afrika nzima,” ametamatisha Guterres kwenye ujumbe wake huo. 

Siku ya maendeleo ya viwanda barani Afrika imekuwa ikiadhimishwa tangu mwaka 2018 ikiambatana na matukio ya wiki nzima ambapo mwaka huu wa 2023 matukio hayo yamefanyika Cairo nchini Misri kuanzia tarehe 9 hadi 15 Novemba.