Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP28 iwe na majibu mujarabu ya kukabili mabadiliko ya tabianchi- UN

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed akihutubia mkutano wa maandalizi kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP28) utakaofanyika Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.
UN/Zumrad Normatova
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed akihutubia mkutano wa maandalizi kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP28) utakaofanyika Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

COP28 iwe na majibu mujarabu ya kukabili mabadiliko ya tabianchi- UN

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa mwezi ujao wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi huko Falme za Kiarabu, UAE, unapaswa kupatia majibu ya pengo lililopo kwenye jamii ya kimataifa kwa hatua dhidi ya tabianchi, amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed siku ya Jumatatu.

Bi. Mohammes alikuwa akihutubia ufunguzi wa kikao cha maandalizi cha mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP28, uliofanyika Abu Dhabi, mji mkuu wa Falme za kiarabu.

Amesisitiza kuwa mkutano ujao wa tabianchi unafanyika wakati muhimu wa vita dhidi ya janga la tabianchi.

Kinatakiwa majibu ya matokeo ya tafiti za wanasayansi

Matokeo ya mkutano huo wa viongozi yanatokana na kile kinachoitwa Kupitia yaliyofanyika duniani, na mkutano huo unahitaji kupatia majibu ya uhakikka matokeo ya tafiti za kisayansi, pengo la hatua kwa tabianchi, hatua za kuhimili mabadiliko ya tabianchi, bila kusahau kujenga mnepo, amesema Naibu Katibu Mkuu wa UN.

Kupitia yaliyofanyika duniani au The Global Stocktake ni jina lililopatiwa msururu wa mikutano iliyowezeshwa na Umoja wa Mataifa na matukio yaliyofanyika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kuwezesha nchi na wadau kuona kile walichofanya au ambacho hawajafanya katika kufika malengo ya Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Nchi ziibuke na mwelekeo mmoja

Mkutano huo tangulizi au Pre-COP huko Abu Dhabi unalenga kusaidia nchi kuweka msingi wa mashauriano na majadiliano katika COP28

Kwa mujibu wa waandaaji wa mkutano huo, ambao ni wa mwisho kwa ngazi ya mawaziri kuelekea COP28, mkutano huo tangulizi ni fursa ya kipeke kwa dunia kuungana na kuwa na mwelekeo mmoja wa kubadili hatua za kimataifa dhidi ya tabianchi.

Mkutano huo wa siku mbili huko Abu Dhabi unaleta pamoja nchi ikiwa ni mwezi mmoja Kabili kabla ya kuanza kwa COP28 huko Dubai, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba.