Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama la UN lakataa Azimio la Urusi kuhusu Gaza

Baraza la Usalama la UN likikutana 16-10-2023 kuhusu Mashariki ya Kati ikiwemo suala la Palestina
UN /Eskinder Debebe
Baraza la Usalama la UN likikutana 16-10-2023 kuhusu Mashariki ya Kati ikiwemo suala la Palestina

Baraza la Usalama la UN lakataa Azimio la Urusi kuhusu Gaza

Amani na Usalama

Rasimu ya azimio iliyowasilishwa na Urusi na washirika wake kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa usiku wa leo kwa lengo la kusaka sitisho la mapigano huko Gaza, Mashariki ya kati ili misaada ya kibinadamu iweze kufikia wahitaji, limegonga mwamba baada ya kushindwa kupata kura zinazohitajika ambazo n ikura 9 kati ya 15.

Tweet URL

Wajumbe 5 ambao ni China, Gabon, Msumbiji, Urusi na Falme za kiarabu walipiga kura za ndio ilhali wajumbe 4 ambo ni Ufaransa, Japan, Uingereza na Marekani walipiga kura ya hapana.

Wajumbe 6 hawakupiga kura kuonesha msimamo wowote nao ni Albania, Brazil, Ecuador, Ghana, Malta na Uswisi.

Rasimu hiyo ya azimio iwapo ingalipita, ilikuwa inataka sitisho la mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa kipalestina, Hamas huko Ukanda wa Gaza.

Kauli baada ya rasimu kugonga mwamba

Rais wa Baraza alitoa fursa kwa wajumbe kuzungumza na kuelezea mantiki ya upigaji wao wa kura ambapo Urusi ambayo iliwasilisha rasimu hiyo ilipiga kura ya ndio.

Mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Vasily Nebenzya, alisema, “tunasikitika kuwa Baraza, kwa mara nyingine tena, limejikuta mateka wa nia za kibinafsi za kundi la nchi za magharibi. Hii ndio sababu halikuweza kutuma ujumbe dhahiri, thabiti na wa pamoja wenye lengo la kupunguza kuendelea kwa mapigano.”

Nchi za magharibi zimesigina matarajio ya wenye uhitaji- Urusi

Amesema tunazungumzia kuibuka kwa ghasia kubwa zaidi katika miongo iliyopita. Leo hii, dunia nzima inasubiri kwa hamu kuona Baraza la Usalama likichukua hatua ili kumaliza umwagaji huu wa damu.

Balozi Nebenzya amesema badala yake, nchi za magharibi zimekanyaga matarajio hayo.

Kutokutaja Hamas ni unafiki- Marekani

Fursa ya kuzungumza ikaenda kwa Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Linda Thomas-Greenfield, ambaye bila kumung’unya maneno amesema azimio la Urusi limewasilishwa bila mashauriano, halikutaja kabisa Hamas, hakuna kabisa.

Amesema kwa kushindwa kulaani Hamas, Urusi inalinda kundi la kigaidi ambalo linatenda ukatili kwa raia wasio na hatia. “Inashtusha. Ni unafiki na haiwezi kutetewa.”

Rasimu ya pili kuwasilishwa na Brazil Jumanne

Rasimu ya Urusi ilikuwa moja ya rasimu mbili za kujadiliwa na kuzingatiwa.

Brazili ndio iliwasilisha rasimu ya pili ambayo itawasilishwa Barazani kwa ajli ya kupigiwa kura kesho Jumanne Oktoba 17.

Rasimu hiyo inataka sitisho la mapigano kwa misingi ya kiutu , inalaani wanamgambo wa kipalestina, Hamas kwa kushambulia Israel.