Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Griffiths na mambo 3 anayotaka kusikia kutoka Gaza

Wafanyakazi wa uokoaji wakiwa kwenye jengo la makazi lililobobolewa baada ya mashambulizi huko kusini mwa Israel
© Magen David Adom Israel
Wafanyakazi wa uokoaji wakiwa kwenye jengo la makazi lililobobolewa baada ya mashambulizi huko kusini mwa Israel

Griffiths na mambo 3 anayotaka kusikia kutoka Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura Martin Griffiths, ameeleza wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa mzozo wa kibinadamu huko Gaza, Mashariki ya Kati, kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya Israel na wanamgambo wa kipalestina, Hamas, halikadhalika hatma ya mateka wa Israel, huku pia akieleza matarajio yake ya kupokea habari njema za misaada kuruhusiwa kuingia Gaza. 


 

Akihojiwa jijini Geneva nchini Uswisi hii leo na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, Mkuu huyo wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA amezungumzia hali inayoendelea huko Mashariki ya Kati na kutaja mambo matatu.

Mateka wa Israel waachiliwe huru

Mosi, ametaka mateka wa Israel wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto waliochukuliwa na wapiganaji wa Hamas waachiliwe mara moja.

Sheria za kimataifa za kibinadamu ziheshimiwe

Pili, ametaka kuheshimiwa kwa sheria za kibinadamu kwenye vita akieleza kuwa “huwezi kuwaeleza watu wahame kutoka kwenye hatari bila ya kuwasaidia kwenda mahali wanapotaka, ambako wanataka kuwa salama na kuwapa misaada ya kibinadamu ikayofanya safari yao hiyo kuwa salama.

Akifafanua suala la misaada ya kibinadamu Griffiths amesema kwa sasa hospitali hazina nishati ya kujiendeesha, na wanakabiliwa na upungufu wa misaada hivyo watu hawawezi kuhama kutoka Gaza Kaskazini Kwenda Gaza Kusini bila ya Msaada.

Njia ya kupitia kivuko cha Rafah ifunguliwe

“Suala la tatu tunahitaji misaada”, amesisitiza Griffiths akieleza kuwa wanaendelea na mazungumzo na nchi za Israel, Misri na nyinginezo huku wakitarajia kupata habari njema.

“Na ninatumai kusikia habari njema asubuhi ya leo kuhusu misaada kuruhusiwa kuingia huko Gaza kupitia kivuko cha Rafah, (kilichoko kati ya Misri na Israel) kusaidia watu milioni moja waliohamia eneo hilo wakitokea Kaskazini pamoja na wakazi wa eneo hilo la kusini waliokuwepo muda wote. Na kumesisitiza katika hili “sheria za vita, misaada, na kuruhusiwa kupita” lazima zizingatiwe.

Mkuu huyo wa kuratibu misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa hapo kesho yeye mwenyewe ataenda Mashariki ya Kati ili kusaidia kwenye mazungumzo pamoja na kuonesha mshikamano na wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu ambao wamesalia kuendelea kutoa usaidizi kwa watu. 

Kuna maisha baada ya vita

Amehitimisha mahojiano yake kwa kueleza kueleza kuna maisha baada ya vita. 

“Ninataka kuwaacha na wazo moja la mwisho. Historia inatuambia kwamba kitendo cha vita vina athari ambazo mara nyingi hazizingatiwi wakati watu wakiingia vitani. Tumeona filamu hii kwa mara nyingi sana. Tunahitaji kuwa na wasiwasi na kuunda hali ambayo kwa sasa itaonekana kama ya kipuuzi - ambapo Waisraeli na Wapalestina wanaweza kuishi kama majirani, kama marafiki, kwa hakika, kama wanaoingiliana, ambapo hawahitaji kupeana mafunzo kupitia vita. Asante.”