Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe wa UN Mashariki ya Kati amelaani mashambulizi ya anga huko Gaza Israel

Tor Wennesland, Mratibu Maalum wa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati, akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza la Usalama kuhusu hali katika eneo hilo.
UN Photo/Manuel Elías
Tor Wennesland, Mratibu Maalum wa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati, akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza la Usalama kuhusu hali katika eneo hilo.

Mjumbe wa UN Mashariki ya Kati amelaani mashambulizi ya anga huko Gaza Israel

Amani na Usalama

Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa anayehusika katika mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati leo ameelezea hofu yake kufuatia operesheni ya kijeshi ya Israel ambayo inaripotiwa kuwaua zaidi ya Wapalestina kumi, wakiwemo makamanda watatu wa kundi la wanamgambo la Islamic Jihad.

Tor Wennesland, mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa wa mchakato wa amani Mashariki ya Kati, amesema, "Nimesikitishwa sana na matukio ya Gaza baada ya Israel kuanzisha operesheni ya kijeshi asubuhi ya leo ikiwalenga wanachama wa vuguvugu la Palestina la Jihad Islamic.”

Mashambulizi ya anga ya Israel ndani ya Gaza yamesababisha mauaji ya Wapalestina 13, wakiwemo wanachama watatu wa PIJ, daktari mmoja, wanawake watano na watoto wanne, na zaidi ya watu 20 kujeruhiwa, amesema, huku akilaani tukio hilo.

Tor amesisitiza kuwa "Hii haikubaliki,",na kuzitaka pande zote kujizuia na kuepuka kuongezeka kwa mvutano na machafuko.

Mratibu huyo maalum, ambaye anafanya kazi na pande zinazohusika na mchakato wa amani kusongesha maendeleo katika kufikia suluhu ya Serikali mbili, amesema ofisi yake inaendelea "ikishirikiana kikamilifu na pande zote katika jaribio la kuepusha mzozo mkubwa zaidi wenye matokeo mabaya kwa wote".

Kwa mujibu wad uru za habari, mashambulio mengi ya anga ya Israeli yalifanywa mapema asubuhi ya leo Jumanne.

Ukiukaji mwingine lazima ukomeshwe

Kauli yake imekuja siku moja baada ya kulaani ubomoaji wa shule ya msingi inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya katika Ukingo wa Magharibi.

Vichochezi vinavyoendelea vya migogoro, ikiwa ni pamoja na kubomolewa kwa shule, "vinazalisha hali ya kutoaminiana na mvutano kati ya Wapalestina na Waisraeli na kudhoofisha matarajio ya kupata suluhu ya kisiasa," amesema katika taarifa iliyotolewa Jumatatu kufuatia ubomoaji uliofanywa na  mamlaka ya Israel tarehe 7 Mei.

Shule ya msingi ya Wapalestina inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya ilikuwa inahudumia kijiji cha Jubbet adh Dhib, mashariki mwa Bethlehem, katika eneo C la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, na kuathiri moja kwa moja elimu ya watoto 40.

Shule 58 zinakabiliwa na ubomoaji kinyume cha sheria

Ubomoaji huo ulifuatia amri ya mahakama ya Israel iliyoeleza wasiwasi wa usalama katika kujibu ombi la shirika la walowezi.

Kwa sasa, shule 58, zinazohudumia watoto 6,500, zinakabiliwa na tishio la kubomolewa kutokana na ukosefu wa vibali vya ujenzi ambavyo ni vigumu kwa Wapalestina kupata, amesema Wennesland .

"Haki ya mtoto ya kupata elimu ni lazima iheshimiwe," amesema, akitoa wito kwa mamlaka ya Israel kusitisha ubomoaji na kufukuzwa, ambayo ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa, na kuidhinisha mipango ya jumuiya za Wapalestina kujenga kisheria katika eneo C ili kushughulikia mahitaji yao ya maendeleo ikiwa ni pamoja na shule.

Ameongeza kuwa "Vitendo kama hivyo ambavyo vinaathiri vibaya utoaji wa huduma za msingi kwa Wapalestina, vinatishia utulivu, na kudhoofisha Mamlaka ya Palestina.”