Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Midahalo ya vijana itawasaidia kushiriki masuala ya kisiasa: UNMISS

Mjumbe wa Vijana wa Katibu Mkuu wa UN alipotembelea Torit nchini Sudan na kukutana na vijana. (Picha ya Maktaba)
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Mjumbe wa Vijana wa Katibu Mkuu wa UN alipotembelea Torit nchini Sudan na kukutana na vijana. (Picha ya Maktaba)

Midahalo ya vijana itawasaidia kushiriki masuala ya kisiasa: UNMISS

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS kwa kushirikiana na Umoja wa wanafunzi wa nchini humo wanaendesha midahalo ya wanafunzi lengo likiwa ni kuchagiza vijana waweze kushiriki kikamilifu katika masuala ya siasa kuelekea uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba 2024

Midahalo hii inaendeshwa ndani ya vyuo na inahusisha timu tatu za wanafunzi kutoka taaluma tofauti wanaotakiwa kupambana kwa hoja katika maeneo matatu, Mosi Uwakilishi wa kijinsia katika Serikali, Pili, Utawala wa kikatiba, na tatu Jukumu la Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo. 

Maswali ya mdahalo ni, je Uwakilishi wa kijinsia serikalini uwe suala la lazima au hiari?, Je Sudan Kusini itakuwa na serikali ya shirikisho? na je UNMISS katika utendaji wake ina upendeleo katika kuwalinda raia? 

Kundi litakaloibuka na ushindi basi litapata fursa ya kuwakilisha chuo chao katika mjadala mkubwa kabisa baina ya vyuo utakaofanyika hapo baadae jijini Juba ukiratibiwa na UNMISS. 

Ndubisi Obiorah ni Afisa mwandamizi wa masuala ya kisiasa wa UNMISS na anasema midahalo hii inatoa fursa ya vijana sio tu kutambua masuala yanayoendelea katika siasa ndani ya nchi yao bali pia inawapa fursa ya kujadiliana masuala tata, na uvumilivu kwa maoni kinzani.

“Tunapoelekea kwenye shughuli za uchaguzi Mkuu mnamo mwezi Desemba 2024 ni muhimu vijana ambao ni viongozi wa baadaye wa Sudan Kusini waweze kujifunza jinsi ya kujadili masuala ya utawala bora wa kikatiba na ujenzi wa amani kama maandalizi ya uchaguzi wa mwakani.”

Vijana walioshiriki katika mdahalo huo kutoka chuo kikuu cha Juba waliishukuru UNMISS kwakuratibu mazungumzo hayo muhimu. 

Mabil James Madit alisema vijana ndio kundi kubwa la wananchi hivyo wanajukumu kubwa.  “Sisi ndio kundi kubwa sana la wananchi, asilimia 72 ya Sudan Kusini ni vijana maana yake ni kwamba sauti zetu ni za msingi sana, sisi ndio tunajihusisha na vita, sisi ndio tunarubuniwa na vyama, na ina maana ni jukumu zito sana la vijana kujenga jamii yenye amani na isiyoleta mapigano pale inapotokea mabishano.”

Naye Stella Paullily akaeleza umuhimu wa vijana kuchagua wawakilishi wao. “Kwa wakati huu inabidi tuhakikishe sauti zetu zinasikika, tujaribu kwa njia zote kupaza sauti zetu, hata kama si kwa ujumla lakini tunawapa wawakilishi, tunawapa watu wetu wanaoweza kuwakilisha sauti zetu huko nje ili itakapofika wakati ambao sisi ndio tunashika nchi, tunahakikisha tunakuwa na maendeleo endelevu yenye amani na maendeleo ndani ya nchi.” 

Takriban wanafunzi 400 wameshiriki katika midahalo hiyo.