Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na Azerbajian wakubaliana ujumbe kuelekea eneo la Karabakh

Wakimbizi huko Goris nchini Armenia wakisubiri kwenye kituo cha usambazaji kupokea vifaa vya nyumbani.
© UNHCR/Karen Minasyan
Wakimbizi huko Goris nchini Armenia wakisubiri kwenye kituo cha usambazaji kupokea vifaa vya nyumbani.

UN na Azerbajian wakubaliana ujumbe kuelekea eneo la Karabakh

Msaada wa Kibinadamu

Serikali ya Azerbaijan na Umoja wa Mataifa wamekubaliana juu ya ujumbe wa kwenda eneo la Karabakh mwishoni mwa wiki hii kujionea hali halisi wakati huu ambapo watu wanakimbia kwa hofu ya usalama wao kwenye eneo hilo linalozozaniwa kati ya Azerbaijan na Armenia, nchi ambazo zamani zilikuwa chini ya Muungano wa Kisovieti.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema utaongozwa na Mratibu Mkazi wa UN nchini Azerbaijan, Vladanka Andreeva,  na Mkurugenzi wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa masuala ya kibinadamu, OCHA,  Ramesh Rajasingham. Timu ya ufundi kutoka OCHA, halikadhalika wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa watajumuika kwenye msafara huo. 

UN inafanya nini Armenia 

Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Armenia, ikiongozwa na Kaimu Mratibu Mkazi Nanna Skau, inashirikiana na serikali kusaidia wimbi la wakimbizi wanaovuka mpaka na kuingia nchini humo kutoka eneo la Karabakh. Takwimu za hivi punde zaidi zinasema takribani watu 93,000 wamevuka mpaka na kuingia Armenia. 

UNFPA na huduma kwa wanawake 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, (UNFPA) linasaidia maelfu ya wanawake walio katika vituo vya mpito, kwenye mikoa ya kusini-mashariki ya Syunik na Vayots Dzor kwa kuwapatia vikasha 8,000 vya kujisafi, vikiwa na maji safi ya kunywa, taulo za kike, sabuni na vifaa vingine.  

UNFPA inasaidia pia mamlaka za Armenia kupatia wakimbizi na wenyeji wao kwa kuwapatia vifaa 150,000 vya afya. 

UNICEF na eneo salama kwa watoto 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, (UNICEF) limeanzisha eneo salama kwenye mji wa kusini-mashariki wa Goris, eneo ambalo linahudumia watoto 300 kila siku pamoja na wazazi wao, wakiwa na kitengo pia cha kutoa huduma za kiutuni. 

Shrika hilo pia limepatia mamlaka za afya za Armenia dawa muhimu na vifaa vingine kwa ajili ya watoto. 

WFP na jiko tembezi 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani, (WFP) limeweka bohari mbili tembezi kwenye mji wa Goris zikiwa zimehifadhi vifaa visivyo vyakula, halikadhalika jiko tembezi linalohudumia watu 3,000 kila siku. 

Halikadhalika shirika limegawa vifurushi 4000 vya vyakula kusaidia watu 16,000 wenye mahitaji mkoani Syunik. 

UNDP 

Kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, (WHO) na UNICEF, shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) linandaa uzinduzi wa mfumo wa usaidizi wa kisaikolojia na kijamii kukidhi mahitaji ya watu zaidi ya 12,000. 

Timu ya Umoja wa Maitafa iko ‘chonjo’ kuongeza usaidizi kwa kuzingatia ombi la serikali ya Armenia. 

Bofya hapa kufahamu kinachozozaniwa Karabakh.