Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa nini kuzuia upotevu na utupaji wa chakula ni muhimu na jukumu la kila mtu: FAO

Upotevu na utupaji wa chakula unahitaji kupunguzwa ili kulisha kwa ufanisi zaidi idadi ya watu inayoongezeka ulimwenguni.
© FAO/Heba Khamis
Upotevu na utupaji wa chakula unahitaji kupunguzwa ili kulisha kwa ufanisi zaidi idadi ya watu inayoongezeka ulimwenguni.

Kwa nini kuzuia upotevu na utupaji wa chakula ni muhimu na jukumu la kila mtu: FAO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika siku ya kimataifa ya uhamasishaji kuhusu uelewa wa Upotevu na utupaji wa chakula, shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO linataka kila mtu atambue ni kwanini kuzuia na kupumguza upotevu na utupaji wa chakula ni muhimu hasa katika kuchangia mabadiliko ya mifumo ya chakula na utimizaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs.

Siku yam waka huu ambayo imebeba mauadhui “Komesha upotevu na utupaji wa chakula kwa ajili ya watu na sayari” inaadhimishwa huku kati ya watu milioni 691 na 783 walikabiliwa na njaa mmwaka 2022 limesema shirika hilo.

Likisisitiza jinsi hali inavyohitaji kubadilika haraka shirika hilo linasema wakati njaa na kutokuwa na uhakika wa chakula kukiendelea duniani mwaka 2022 inakadiriwa kuwa asilimia 13 ya chakula duniani ilipotea kwenye mnyororo wa thamani kuanzia baada ya kuvunwa na kabla ya kufika sokoni, na asilimia 17 nyingine ilitupwa majumbani, kwenye sehemu za utoaji huduma za chakula na kwenye masoko ya chakula.

Hivyo FAO inatatoa mwito wa kuchukua hatua kwa mashirika ya umma, sekta binafsi, na kila mtu ili kupunguza upotevu na utupaji wa chakula (FLW) na kuelekea kubadilisha mifumo ya kilimo kwa ajili ya kuweza kuchangia katika mafanikio ya utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya 2030. 

Kwani limesema Kupunguza upotevu na utupaji wa chakula kunaweza kuwa na jukumu muhimu katika sio tu kwa mabadiliko ya mifumo ya chakula ya kilimo bali pia kwa kuongeza upatikanaji wa chakula, kuchangia uhakika wa chakula, lishe bora, na kujenga mnepo. 

Upunguzaji wa upotevu na utupaji wa chakula kwa mujibibu wa FAO pia hutumika kama mkakati muhimu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi (GHGs). 

Kwa hivyo unaweza kusaidia nchi na biashara kuongeza hamasa ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, huku zikihifadhi na kulinda mifumo yetu ya ikolojia na maliasili ambayo mustakabali wa chakula huitegemea.

FAO inasema hivi sasa, mifumo mingi ya kilimo ya chakula duniani sio endelevu, kwani inaharibu ardhi ya kilimo, inachangia uzalishaji wa gesi chafu na upotevu wa bioanuwai na hutumia maji mengi ya ardhini. 

Mifumo ya chakula pia iko hatarini kwa majanga ya hali ya hewa na mishtuko mingine, kwa sababu ya athari kwa mazingira.