Wakati watu milioni 811 wanalala njaa, dunia inapoteza asilimia 17% ya chakula inachozalisha:UN

Kupunguza upotevu na utupaji wa chakula kungechangia uhakika wa chakula, kuimarisha ubora wa chakula na kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.
Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO linataoa wito wa kupambana na tabia hii, ambayo sio haki ya nchi tajiri, kama wengi wanavyofikiria.
Shirika hilo limeonya leo kwamba “Uhaba wa chakula, njaa na utapiamlo huathiri kila nchi duniani,” na limetoa ombi la haraka kupunguza idadi hiyo ya chakula kinachopotea.
Kwa mujibu wa takwimu za FAO, “tani milioni 931, au asilimia 17% ya chakula kilichozalishwa mwaka 2019, kiliishia kwenye mapipa ya taka ya kaya, wauzaji, migahawa na wadau wengine wa chakula.”
Wakati huo huo, watu milioni 811 wana njaa na milioni 132 leo hii wanakabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula na lishe kutokana na janga la COVID-19.
Kwa upande wa fedha FAO inasema, upotezaji wa chakula wa kila mwaka unakadiriwa kuwa ni wa gharama sawa na dola bilioni $ 400.
Takwimu hizi zimetolewa leo wakati dunia ikiadhimisha Siku ya kimataifa ya uhamasishaji kuhusu upotezaji na utupaji wa chakula ambayo itakuwa ikiadhimishwa kila mwaka Septemba 29.
Shirika hilo limeongeza kuwa chakula kisichotumiwa hupoteza rasilimali kama vile ardhi, maji, nishati, udongo, mbegu na pembejeo zingine zinazotumika kwa uzalishaji wake.
Mkurugenzi msaidizi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii wa FAO ameumbia mkutano na waandishi wa habari huko Geneva Uswis hii leo kwamba changamoto ya kutupa taka za chakula ni ya dunia nzima na sio tu kwa mataifa tajiri.
“Ukosefu wa chakula, njaa na utapiamlo huathiri kila nchi duniani, hakuna iliyonusurika. Duniani kote watu milioni 811 wanateseka na njaa, bilioni 2 wanakabiliwa na upungufu wa lishe inayohitajika, yaani vitamini na madini, na mamilioni ya watoto wanakabiliwa na tatizo la kudumaa na kupoteza uzito, aina mbaya za utapiamlo, "amesema mkurugenzi huyo msaidizi Nancy Aburto.
Ameonya kwamba kwa sababu ya gharama kubwa, lishe bora haiwezi kufikiwa na idadi kubwa ya watu katika sehemu zote za dunia, ikiwa ni pamoja na Ulaya.
Nancy Aburto ameomngeza kuwa nchi zinahitaji kugeukia nyenzo mpya bunifu za kupunguza utupaji wa chakula, akitoa mifano kama vifungashio vipya ambavyo vinaweza kuongeza muda wa kuhifadhi vyakula vingi au apu za simu zinazowaleta pamoja watumiaji na wazalishaji, na hivyo kupunguza muda wa kati ya mavuno na ulaji wa chakula.
Kupunguza upotevu na utupaji wa chakula kutaboresha mifumo ya chakula, kuchangia uuhakika wa chakula na kuhakikisha ubora wa chakula, ambao unaonekana katika lishe.
Pia ingechangia "kwa kiasi kikubwa kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na shinikizo kwa rasilimali za ardhi na maji".
FAO imetaka hatua za haraka zichukuliwe ili kufanikisha lengo la maendeleo endelevu namba 12, ambalo linakusudia kuhakikisha matumizi endelevu na kupunguza nusu ya chakula kinachotupwa kwa kila mtu ifikapo 2030.
Kwa mujibu wa FAO hii inahitaji kujitolea na ushiriki wa jamii nzima kwa ujumla, mamlaka za kitaifa na za mitaa, wafanyabiashara na watu binafsi, ili kuweka kipaumbele katika hatua za mwelekeo huu.
Miezi mitatu kabla ya kumalizika kwa mwaka wa kimataifa wa matunda na mboga, FAO imekumbusha kuwa bidhaa za kilimo zinahakikisha lishe na uhakika wa chakula.
"Kuchagiza lishe bora ili kuimarisha mfumo wetu wa kinga ya mwili ni suala muhimu na sahihi ukizingatia changamoto kubwa ya kiafya inayoikabili dunia hivi sasa ," amesema mkurugenzi mkuu wa FAO Qu Dongyu wakati wa uzinduzi wa mwaka.
Amesisitiza pia kwamba upotezaji na utuapaji wa matunda na mboga ni tatizo lenye athari kubwa na akataka kuingia kwenye teknolojia za ubunifu na mbinu za kuongeza muda wa kudumu wa mazao kama mbogamboga na matunda.
Hatua nyingine iliyopendekezwa ni kuiiozesha taka za chakula na kuzigeuza mbolea badala ya kuzitupa jalalani.