Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajenda ya 2030 itashindwa tusipoheshimu haki ya kupata taarifa

Irene Khan, Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.
United Nations
Irene Khan, Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.

Ajenda ya 2030 itashindwa tusipoheshimu haki ya kupata taarifa

Haki za binadamu

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni Irene Khan ametoa wito kwa serikali kuimarisha juhudi za kufunga “mgawanyiko wa kidijitali” na kuondoa vizuizi vyote vya haki ya kupata habari.

“Bila ya kuwa na muunganisho wa watu wote na wenye maana kwa wote, haki ya kupata habari ni ahadi tupu kwa mabilioni ya watu duniani kote,” amesema Bi. Khan katika ujumbe wake wa Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Habari kwa Wote.

Maadhiminisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa kwa Wote yamejikita katika nafasi ya mitandao katika upashanaji wa habari na kuweka mkazo kwa mataifa kuimarisha juhudi zao za kuondoa mgawanyiko wa kidijitali kwa kuondoa vizuizi vyote vya haki ya kupata habari. 

Katika taarifa yake kutoka jijini Geneva Uswisi ameeleza kuwa “Huduma ya mtandao haipatikani kwa usawa au haiwafikii watu wote na hiyo inakuza ukosefu wa usawa uliopo na kuunda ukosefu mpya wa usawa kulingana na jinsia, jiografia, kabila, kipato na ujuzi wa kidijitali, na kuongeza udhaifu kwa wale waliotengwa zaidi katika jamii.”

Ufikiaji wa Mtandao kwa wote na kwa bei nafuu na upatikanaji wa taarifa zote ni shabaha ya wazi ya kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs. “Ninahimiza Mataifa yote kutafsiri ahadi walizotoa hivi majuzi katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Maendeleo Endelevu kuwa hatua madhubuti.”

Mitandao kufungwa

Katika zaidi ya nchi 74 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, serikali zimefunga au kupunguza kasi ya Mtandao, au kuzuia mawasiliano ya simu kwa muda mfupi au kwa muda mrefu, na kuathiri upatikanaji wa habari na kutatiza afya, elimu na huduma nyingine muhimu.

“Haki ya kupata habari ni ‘oksijeni’ ambayo bila hiyo hakuna demokrasia wala maendeleo yatakayoweza kustawi.” Amesema Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa akitilia mkazi umuhimu wa watu kupata taarifa ili waweze kushiriki vyema kwenye kufanya maaamuzi, kuboresha maisha yao na hatimaye maendeleo ya taifa kwa ujumla. 

Katika ripoti yake aliyowasilisha mwezi Julai mwaka huu katika baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Bi. Kan alieleza habari njema kwamba Mataifa mengi yamepitisha sheria za upatikanaji wa habari na baadhi hata kutambua upatikanaji wa mtandao kama haki ya kisheria. 

Hata hivyo ripoti hiyo ilikuwa na habari mbaya kwamba sheria hizi mara nyingi hazitekelezwi ipasavyo, na mbinu mbalimbali kutumika kuzuia au kunyima ufikiaji wa habari, mtandaoni na nje ya mtandao, kwa waandishi wa habari wa uchunguzi, watetezi wa haki za binadamu na watendaji wengine wa mashirika ya kiraia. 

Kupata taarifa, uhuru wa kujieleza na kushiriki kikamilifu mtandaoni na nje ya mtandao, kwa vijana, mashirika ya kiraia na vyombo vya habari huru ni muhimu, iwe lengo ni kukabiliana na changamoto za kimataifa, kama vile mabadiliko ya tabianchi na magonjwa ya milipuko au kuvunja mifumo ya zamani ya ubaguzi, kutengwa na vurugu.