Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuingie ng’we ya pili ya SDGs bila kuacha nusu ya timu nje ya uwanja – Bi. Amina

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed akihutubia washiriki wa tamasha la raia wa dunia, Global Citizen Festival, katika bustani ya Central Park jijini New York, Marekani 23 Septemba 2023
UN News/Nathan Beriro
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed akihutubia washiriki wa tamasha la raia wa dunia, Global Citizen Festival, katika bustani ya Central Park jijini New York, Marekani 23 Septemba 2023

Tuingie ng’we ya pili ya SDGs bila kuacha nusu ya timu nje ya uwanja – Bi. Amina

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mvua kubwa iliyonyesha jijini New York, Marekani siku ya jumamosi, haikuzuia takribani watu 60,000 wakiwemo wachechemuzi, wasanii, washawishi na raia wengine, kujitokeza katika bustani ya aina yake ya Central Park, kusikiliza wito thabiti kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuhamasisha mabadiliko.

“Inyeshe mvua, litoke jua, tuko hapa kwa sababu tumejitoa kwa dhati kwa ajili ya sayari yetu,” alisema Amina Mohammed akihutubia Tamasha la Raia wa Dunia au Global Citizen, ambalo hufanyika wakati wa wiki ya vikao vya ngazi ya juu vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kila mtu achukue hatua ng’we ya mwisho

Amegusia mbio za sasa za kutimiza malengo 17 ya maendeleo endelevu, SDG, kumaliza janga la tabianchi na kusongesha usawa halisia wa kijinsia.

“Kile kinachofanyika leo kinaakisi kile ambacho viongozi wetu wamekutana wiki nzima, ahadi walizopitisha miaka 7 iliyopita, na leo tunaazimia kile ambacho Al Pacino alisema sema kama ilivyo: Ni muda wa kupasha misuli kumaliza ng’we ya mwisho, na tuko nyuma lakini hatujashindwa.”

Aliuliza umati wa watu waliokusanyika kwenye bustani hiyo iliyosheheni ukijani ambayo iko katikati ya kitongoji cha Manhattan iwapo wanajihisi kama wanaleta mabadiliko duniani: “Ni kwamba katika Umoja wa Mataifa, tunaungana nanyi, tunahamasisha watu duniani kote.”

Lengo la tamasha hilo la Global Citizen au Raia wa Dunia ni kutokomeza umaskini uliopindukia kupitia malenog ambayo yanaendana kwa kina na Umoja wa Mataifa na SDGs.

Katika tamasha hilo, viongozi wa dunia waliahidi dola milioni 240 kwa ajili ya Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, (IFAD), waliahidi kulinda ekari nyingie 900,000 za ardhi kwenye msitu mnene wa mvua wa Amazon nchini Brazil, na kupata ahadi kutoka kwa wajumbe 9 wa Baraza la Kongresi la Marekani, na kiongozi wa chama cha Labour nchini Uingereza Kier Starmer kufuatilia ahadi za kitaifa kuhusu tabianchi.

Shaka katika kutimiza ahadi

Naibu Katibu Mkuu ametambua kuwa watu wengi duniani wanaumizwa kimwili na kifikra kutokana na vita vinavyoendelea huku sayari ikiwa sio tu inaongezeka joto bali inatokota.

“Viongozi kwa kweli wanahaha kutumia nguvu na mamlaka kutekeleza ahadi ya SDGs na wako hatarini kushindwa kutimiza ahadi kwa mabilioni ya watu,” amesema Bi. Mohammed.

Hata hivyo habari njema ni kwamba miaka 7 imesalia kufikia 2030, na kwamba kuna fursa ya kupata Ushindi kipindi cha pili, lakini “hatuwezi kushinda bila kuzuia dunia yetu kuendelea kutokota.”

Ziba pengo

“Sisi viongozi tunahitaji kuzima pengo la kidijitali– kwa sababu  hatuwezi kushinda iwapo mabilioni ya watu hasa wasichana hawako mtandaoni.

Amesema iwapo wanawake na wasichana wataacha pembezoni kwenye juhudi za pamoja, hiyo ina maana nusu ya timu haiko uwanjani.

“Kwa hiyo wakazi wa New York, huu ni wakati wa kazi. Na wakati wa kazi ndio mabingwa wanatengenezwa,” amesema.

“Hebu na tuungane  na tupambane pamoja – inchi kwa inchi – kutimiza ahadi ya kufanikisha SDGs ifikapo mwaka 2030.”